FLORIAN KAIZA
TANZANIA imepitia simulizi nyingi zenye kusisismua lakini hazisemwi sana kwenye vyombo vya habari hivyo vizazi vya sasa na vijavyo havijui na havitajua mambo mengi yaliyowahi kutokea na kuleta changamoto kubwa kwa baadhi ya viongozi serikalini, sambamba na kutekeleza mambo yao mbalimbali.
Mwaka 1980, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Balozi Joseph Rwegasira alianzisha operesheni maalumu ya kuwaondoa makahaba wote waliokuwa wakifanya biashara ya kuuza miili ndani ya jiji hilo, sambamba na kutumia nguvu kuwaondoa wale wote ambao wangekaidi amri hiyo.
Operesheni hiyo ilikuwa imelenga kuwarudisha makahaba waliopo Dar es Salaam makwao, ili wakaendeleze kazi ya kulijenga taifa kupitia shughuli zao nyingine kama kilimo, ufugaji nk, na hivyo kusaidia kuimarisha vijiji vya ujamaa wakati wa mpango wa taifa wa kuimarisha na kuendeleza vijiji vya ujamaa, maarufu kama operesheni vijiji.
Baada ya uamuzi huo wa Balozi Rwegasira, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alimuita Ikulu, Balozi Rwegasira akamfafanulie utaratibu na madhumuni ya operesheni hiyo.
Alipofika Ikulu, kauli ya kwanza ya Mwalimu Nyerere ilimpa matumaini Balozi Rwegasira kuwa huenda operesheni yake iliungwa mkono pale Mwalimu Nyerere alipohoji; ‘Nasikia umeamua kuwahamisha mama zangu warudi makwao wakalime maharagwe.’

Makahaba
Balozi Rwegasira alijibu haraka kwa kusema; ‘Unajua Mwalimu, hatua yangu hii ni kutekeleza kaulimbiu yetu ya kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu na operesheni ya kilimo cha kufa na kupona, pengine hata kaulimbiu ya awali tuliyoiita siasa ni kilimo, ndipo nikaiona ni muafaka kabisa.
Hapo ndipo hoja ya Mwalimu Nyerere iliyofuata ilimshtua Balozi Rwegasira aliposema; “Nimekuita unieleweshe ni watu wa aina gani ulioteua warudishwe makwao kwa utekelezaji huo, pia nataka kujua utaratibu unaotumika.’
Mwalimu Nyerere akaendelea kwa kuhoji; ‘Kwa hiyo umewahukumu kwa ukahaba wao au kuna sababu nyingine?’ Hapo Balozi Rwegasira alikaa kimya kwa kutokuwa na jibu muafaka.
Hata hivyo, Mwalimu Nyerere aliendelea kudadisi kwa kuhoji; ‘Ikiwa umeamua kuwatimua makahaba, je, mazingira ya kule utakakowahamisha umeyaandaaje?’
Kwa kuwa hoja ya Mwalimu Nyerere ilikuja kinyume na matarajio ya Balozi Rwegasira, isitoshe hakuelewa mwelekeo wa hoja ile, alibaki kimya. Mwalimu Nyerere akamwambia ‘ukiweza kutimiza hilo, njoo unieleze nibariki operesheni yako.’
Na Mwalimu Nyerere hakuishia hapo aliendelea kwa kumwambia Balozi Rwegasira kuwa; ‘Kama usingekuwa mtani wangu, wito wangu ungeishia hapa lakini hebu nikufafanulie chanzo cha ukahaba.
Mwalimu Nyerere akamuuliza Balozi Rwegasira kama anafahamu wateja wa makahaba ni kina nani, akajibu kuwa ni wanaume. Mwalimu Nyerere alicheka kisha akamuuliza tena; ‘Wewe si mwanaume, je, huko waliko makahaba unakwenda?’ Balozi Rwegasira alijibu, ‘hapana.’
Mwalimu Nyerere akahoji tena; ‘Mimi si mwanaume, je huko naenda?’ Balozi Rwegasira alijibu, ‘hapana Mwalimu.’ Ndipo alipoanza kumchambulia kuanzia wanaume wasiojua kumtaka kimapenzi mwanamke, wasiotaka bughudha ya kutunza familia hivyo hawaoi na hata waliobarikiwa nguvu nyingi za mwili wakienda huko kuzipunguza ili wasisumbue wake zao.

Yesu Kristo akiwa na mwanamke myahudi aliyetuhumiwa kwa vitendo vya ukahaba.
Na hapo ndipo Mwalimu Nyerere alifafanua hoja yake kwa Balozi Rwegasira akisema; ‘Nilipotaka nijue mazingira ya huko utakakowaondoa umeyaandaje, nilijua hao wateja wao wasipowakuta, matokeo ni kubakwa mama zetu, wake zetu, wanafunzi wetu, vilema wetu, hata vichaa wetu. Ndiyo maana katika miji yote duniani makahaba wapo.’
Mwalimu alimalizia kwa kumwambia Balozi Rwegasira kuwa hata mataifa yaliyojigamba kuwa na utawala bora na wa sheria yalishindwa kubuni sheria ya kutawala miili ya watu hususani wanawake hivyo kudhibiti ukahaba.
Pia michezo hatari kama ndondi na kareti, ikaishia kuhalalisha biashara zinazohusisha ukahaba kwa namna moja au nyingine, tena zikitozwa kodi ya mapato kwa serikali.
Hatimaye, Mwalimu Nyerere alitaja kuhusishwa kwa ukahaba katika maandiko matakatifu, ambapo makahaba hawakuhukumiwa kwa ukahaba wao isipokuwa walihimizwa wawe na matendo mema, sawa na walivyohimizwa watu wengine.
Alitoa mfano wa kahaba aliyemkimbilia Yesu alipokimbizwa na umati uliotaka wamponde mawe mpaka afe kama mila yao inavyoruhusu. Yesu aliuambia ule umati akisema; ‘Ikiwa miongoni mwenu kuna asiyepata kutenda mnalomtuhumu nalo na awe wa kwanza kumtupia jiwe.’
Yesu alishusha macho kuendelea kuchora kielelezo chake na alipoinua macho sekunde kadhaa baadaye, hakuona mtu hata mmoja. Ndipo alimuamuru yule kahaba akisema, ‘Inuka uende zako, kawe na matendo mema.’
Mwalimu Nyerere alimhoji Balozi Rwegasira akisema; ‘Kwani Yesu alishindwa kumtamkia kahaba yule aache ukahaba?’

Mwanamke kahaba alipanguza miguu ya Yesu Kristo kwa nywele zake
Akaendelea Mwalimu Nyerere kwa kumtaja kahaba mwingine aliyemkuta Yesu mahali akifanyiwa karamu akamuangukia akilia, mpaka alimlowesha miguu na kumpangusa kwa nywele zake, akampaka manukato.
Yesu alimwambia mwenyeji wake akisema; ‘Huyu mwanamke amekuzidi kwa kuniosha miguu kama ilivyo desturi yetu, ambapo wewe hukufanya hivyo.’
Kwa msingi huu, Mwalimu Nyerere alimtamkia Balozi Rwegasira akisema; ‘Kwa kupewa akili na Mwenyezi Mungu, mwanadamu hatahukumiwa kwa dhambi ya mwenziwe, ndipo kwa hali hiyo, litatimilika agizo la Mwenyezi Mungu kuwa; ‘usihukumu mwenzio, ndipo nawe hutahukumiwa.’
MAKALA HAYA YAMEANDIKWA NA FLORIAN KAIZA. MTANGAZAJI WA ZAMANI WA REDIO TANZANIA DAR ES SALAAM (RTD), REDIO DEUTCH WELLE YA UJERUMANI NA REDIO CHINA, IDHAA YA KISWAHILI. KWA MARA YA KWANZA YALICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA RAIA MWEMA.