Tuesday, December 24, 2024
spot_img

NONDO: MUSWADA WA MABADILIKO YA SHERIA YA UCHAGUZI- Wafungwa, mahabusu wapige kura

ABDUL NONDO

Miswada mitatu imesomwa kwa mara ya kwanza kwenye mkutano wa 13 wa bunge uliomalizika Novemba, 2023 Jijini Dodoma. Miswada hiyo ni wa sheria ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani; sheria ya tume ya taifa ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa.

Hii inatoa fursa kwa wananchi, vyama vya siasa, wadau na wana demokrasia kuchambua, kujadili na kubainisha maeneo yenye upungufu kabla ya Januari/ Februari 2024 ambapo itasomwa kwa mara ya pili.

Nimejaribu kupitia maeneo kadhaa machache yenye upungufu katika miswada miwili, muswada wa sheria ya tume ya uchaguzi na muswada wa sheria ya uchaguzi. Naendelea  na muswada wa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi;

MUSWADA WA MABADILIKO YA SHERIA YA UCHAGUZI.

Sheria hii inakuja kufuta sheria ya uchaguzi wa udiwani, sura 292 na sheria ya uchaguzi sura 343. (sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985 na sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa nambari 4 ya  mwaka 1979.)

Sheria hii ilipaswa iingize pia uchaguzi wa serikali za mitaa, yaani kuwe na sheria moja ya uchaguzi wa urais, ubunge , udiwani na serikali za mitaa.

Kwa sababu uchaguzi wa serikali ya mtaa (Neighborhood Election), hauna sheria bali kanuni ambazo Waziri wa TAMISEMI amepewa mamlaka kuzitunga chini ya sheria ya serikali za mitaa (mamlaka ya miji) sura 288 na sheria ya serikali ya mitaa (mamlaka ya wilaya) sura 287 (R.E 2019).

Kanuni hizo za uchaguzi wa serikali za mitaa zinatungwa na Waziri wa TAMISEMI bila ulazima wa kuchukua maoni ya wadau wa vyama vya siasa au kushirikisha.

Kulipaswa kuwe na sheria moja ya uchaguzi wa rais, ubunge, udiwani na serikali ya mitaa. Chaguzi zote zisimamiwe na tume ya uchaguzi na sio TAMISEMI (uchaguzi wa serikali za mitaa).

Kama nilivyogusia juu, kifungu cha 6(1) cha muswada wa sheria hii ya uchaguzi bado sheria na tume ya uchaguzi inaendelea kuwatambua wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi.

Hawafai kusimamia uchaguzi, ni makada wa CCM. Hawawezi kuwajibishwa na tume wakifanya makosa kwa sababu mamlaka ya uteuzi na nidhamu hayapo kwa tume ya uchaguzi bali  kwa rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM.

Uandikishaji wapiga kura serikali ya mtaa (picha ya mtandaoni)

Sheria hii imeendelea kuweka zuio kwa asiyeridhika na maamuzi ya tume kutokwenda mahakamani. (Finality clauses, exclusionary clauses, ouster clauses).

Kwamba maamuzi ya tume ndio ya mwisho.  Hii ipo kwenye uteuzi wa mgombea wa urais, kifungu cha 37(6) cha muswada wa sheria ya uchaguzi. Ikiwa tume ikikataa uteuzi wa mgombea wa urais, maamuzi ya tume ndio ya mwisho, hakuna rufaa.

Pia kifungu cha 137 ya muswada huu wa sheria ya uchaguzi kinakataza matokeo ya urais kupingwa mahakamani isipokuwa ubunge tuu.

Vifungu hivi juu vya muswada wa sheria hii ya uchaguzi msingi wake upo kwenye katiba ya 1977, ibara ya 74(12) na  41(7). Ibara hizi zinapinga matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani na tume kutoshtakiwa mahakamani .

Uhuru wa tume ya uchaguzi msingi wake ni uwajibikaji, kuzuia matokeo kupingwa mahakamani au tume kushtakiwa tafsiri yake uwajibikaji hauwezi kuwepo.Watumishi wa tume wanaweza kutenda makosa kwa uzembe au makusudi wakiamini hawawezi kuwajibishwa kwa uzembe na makosa yao 

Lakini pia ni kinyume pia na katiba ya 1977, ibara ya 107 (A) inasema mahakama ndio chombo cha maamuzi ya mwisho katika utoaji haki ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia ibara ya 13(6a) ya katiba inatoa fursa kwa mtu ambaye hajaridhika na maamuzi kutafuta haki yake mahakamani.

Raia anayetafuta haki yake kwa amani kwa njia ya mahakama anazuiwa kwenda mahakamani, watawala wanataka haki yake akaitafute msituni?

Huu ndio mwanzo wa machafuko. Haki na mifumo imara ya demokrasia hudumisha amani.

Francis Fukuyama katika kitabu chake ‘End of history and last man (1992),’ anasema nchi yenye misingi imara ya demokrasia haingii katika machafuko. Pia Emmanuel Kant anathibitisha hili kupitia dhana yake ya democratic peace theory – perpetual peace (1795).

Ndio maana madai ya chama chetu, TCD, wadau na wananchi wengi tunasema ni muda muafaka sasa kufanyia marekebisho madogo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (minimum reforms) katika ibara zinazohusu chaguzi hasa ibara ya 74 (12) na 41(7) huku mchakato wa katiba mpya ukipaswa kuanza sasa. Bila marekebisho haya hakuna tume huru wala uchaguzi huru utakaotokea.

Abdul Nondo

Tume ya uchaguzi haiwezi kuwa huru kama itaendelea kuazima azima watumishi wa Umma.

Katika muswada huu wa sheria ya uchaguzi kuna vifungu vingi  kama 6(2),6(4) vimeipa mamlaka tume ya uchaguzi kuteua watumishi wa umma kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kiuchaguzi. Swali la kujiuliza sifa za watumishi hao ni zipi? uadilifu wao ni upi? watu waombe, wateuliwe kwa sifa kuliko kutumia watumishi wa umma.

Kifungu cha 14 (1) na 85(1) cha muswada huu wa sheria ya uchaguzi kinazuia mtu kupiga kura katika eneo ambalo hakuandikishwa. Kuna haja ya nchi yetu kwenda na kasi ya teknolojia, mtu aruhusiwe kupiga kura popote. Hii ndio inachangia idadi ndogo ya watu kupiga kura (low voter turnout).

Mtu kukosa sifa ya kuandikishwa kupiga kura. Kifungu cha 10(1)C cha muswada wa sheria ya uchaguzi. Kifungu kinazuia mtu aliyetiwa hatiani kwa kifungo kinachozidi miezi sita na kifungo cha maisha kupiga kura.

Hii ni kinyume kabisa na ibara ya 5(1) na 21 ya katiba ya mwaka 1977 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara hii inatoa fursa kwa mtu aliyefikisha umri wa miaka 18 kupiga kura.  

Lakini pia kuna kesi nambari 3 ya mwaka 2022 iliyofunguliwa na Mwanaharakati Tito Magoti, chini ya Jaji Elinaza Luvanda kupinga kifungu cha sheria ya uchaguzi kinachozuia wafungwa kupiga kura na hukumu ya kesi hii imetoka.

Kifungu cha sheria ya uchaguzi kinachozuia wafungwa au mahabusu zaidi ya miezi sita kuandikishwa kupiga kura kimebatilishwa na Mahakama. Hivyo wafungwa na mahabusu ruhusa kupiga kura kwa sababu hata huko gerezani walipo wanaathirika na siasa na maamuzi ya viongozi huku nje hivyo ni lazima washiriki kuchagua viongozi wanaona wanafaa.

Sasa kwanini serikali imeendelea kuweka kifungu hiki katika muswada huu wa sheria ya uchaguzi badala ya kutii hukumu ya Mahakama? 

Muswada wa sheria ya uchaguzi, kifungu cha 45(10 ) kinasema mshindi katika uchaguzi wa rais, ubunge au udiwani ni aliyepata kura halali nyingi kuliko mwingine, (winner takes all /plurality/post-past the post). 

Kuna haja muswada huu wa sheria ya uchaguzi na mabadiliko madogo ya katiba kufanyika ili mshindi wa ngazi ya urais apate 50.1%. (majoritarian electoral system) ili kuongeza uhalali (legitimacy) ya ushindi wa kiongozi kutoka kwa wananchi.

Fedha za Tanzania

Kupotea na kuharibika kwa kadi ya kupiga kura ili kupewa kadi nyingine. Kifungu cha 20(1)(2) cha muswada huu wa sheria ya uchaguzi kinasema ikiwa mtu atapoteza kadi au kadi kuharibika basi ikithibitishwa na mwandikishaji, mtu huyu atapewa kadi mpya baada ya kulipa ada.

Hakuna haja ya malipo ya ada ili kupata kadi nyingine ya kupiga kura, hiyo inapaswa kuwa huduma ili kufanikisha mwananchi kutimiza haki yake ya kupiga kura na kuchagua kiongozi kwa mujibu wa katiba Ibara ya 5 (1) na 21. Kifungu hiki ni informal disfranchisement ya kuzuia mtu kuandikishwa kupiga kura, hakifai.

Mpiga kura kupata kadi mpya katika eneo jipya la makazi au kituo cha kupigia kura kipya tofauti na cha awali.

Kifungu cha 19(1)(a)(b) kinasema mpiga kura aliyehamia eneo jipya tofauti na awali atapewa kadi tu kama atarudisha kadi ya awali, kama atathibitishwa ni mkazi wa eneo hilo.

Utaratibu uwe wazi na vigezo  vya kuthibitishwa kama ni mkazi mpya wa eneo viwe wazi. Sheria itamke kuwe na barua ya serikali ya mtaa huo kumtambulisha pamoja na saini za majirani watatu wa eneo hilo ili kudhibiti asiye mkazi wa eneo hilo kupiga kura au mkazi halali kutozuiwa kupiga kura.

Lakini kuna haja ya mifumo yetu iwe ya kisasa kutambua kama mtu ni mkazi wa eneo jipya kwa kuangalia historia ya uandikishwaji wake wa awali aliandikishwa wapi na kadi ya awali ifutwe ili iwe kigezo cha mtu huyo kupewa kadi mpya bila mlolongo mrefu.

Fidia ya pingamizi. Kifungu cha 28(1) hadi (5) cha muswada wa sheria ya uchaguzi kinazungumzia pingamizi.

Mtu anaweza kuweka pingamizi kwa afisa muandikishaji dhidi ya mtu ambaye anakisiwa sio mkazi wa eneo hilo ili asiandikishwe. Kifungu cha 28(5) kinasema baada ya uchunguzi, kama afisa muandikishaji kwa maoni yake ataona pingamizi halina msingi ataagiza kwa maandishi aliyeweka pingamizi kumlipa fidia ya fedha aliyewekewa pingamizi.

Hii sio sahihi, fidia ya fedha kwanini? Kuna njama ya kuweka hofu ili wasiokuwa na sifa ya kupiga kura eneo fulani waandikishwe bila kuzuiwa na waenyeji 

Kukata rufaa mahakamani kwa dhamana ya fedha. Mtu ambaye hakuridhika na maamuzi ya afisa muandikishaji anaweza kwenda mahakama ya wilaya kukata rufaa kwa mujibu wa muswada wa sheria ya uchaguzi, kifungu cha 30(1) baada ya kulipa kiasi cha fedha kama dhamana na kifungu cha 30(4) kinasema mahakama ikiona madai hayakuwa na msingi wowote kiasi cha fedha kama dhamana kilichowekwa kitataifishwa kwa serikali.

Kwanini iwe lazima kuwe na dhamana ya fedha katika kupata huduma ya haki ya mahakama? Kifungu hiki hakifai kinakiuka katiba, ibara ya 107 (A) na ibara ya 13(6 a), ibara zinatoa uhuru wa mtu kwenda mahakamani asiporidhika na maamuzi kwa sababu mahakama ndio chombo cha mwisho cha utoaji haki.

Maboksi ya kuhifadhi kura

Mgombea kuweka dhamana kwa msimamizi wa uchaguzi. Sheria hii kifungu cha 35(1)(2) na 51(1) muswada wa sheria ya uchaguzi, katika uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani inahitaji mgombea kuweka dhamana ya fedha baada ya uteuzi na fedha hizo zitataifishwa ikiwa atapata kura 1/10 ya kura zote halali zilizopigwa.

Hii ni kinyume na ibara ya 21(1)(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ambayo inaruhusu mtu yeyote kushiriki katika masuala ya kiuongozi na maamuzi. Hakuna haja ya kuweka dhamana kama mtu amepitishwa na chama chake huyo anapaswa kuaminika.

Kifungu cha 76(a,b,c) cha muswada wa sheria ya uchaguzi kinatoa fursa kwa msimamizi wa uchaguzi kuandika orodha ya wasimamizi wasaidizi wa vituo. Je, hao wasimamizi wasaidizi wa vituo wanapatikana vipi?

Kwa sababu tumeshudia wengi ni watumishi na makada wa CCM. Kuna haja hata upatikanaji wa wasimamizi wasaidizi wa vituo wapatikane kwa mchakato wa wazi wa kuomba.

Kifungu cha 85(5) cha muswada wa sheria ya uchaguzi kinaruhusu msimamizi wa kituo kutoa amri kumuondoa mtu yeyote kutoka kwenye kituo cha kupiga kura kwa sababu ya utovu wa nidhamu. Utovu upi wa nidhamu?.

Hiki kifungu kinaweza kutumika vibaya dhidi ya mawakala wa vyama vya upinzani. Haya yamewahi kutokea kwenye uchaguzi wa marudio wa Mbarali.

Kifungu kisitoe nguvu ya namna hii kwa msimamizi wa kituo lakini pia kifungu kioneshe njia ya kumpata wakala mwingine mbadala wa chama ikiwa ni wakala wa chama fulani ndio ameondolewa kwenye kituo.

Sheria haijaweka utaratibu wa kumuwajibisha, msimamizi wa uchaguzi wala msimamizi wa kituo ambaye anakiuka taratibu wakati wa uchaguzi. Kifungu cha 114 kimejikita zaidi kwenye adhabu kwa mpiga kura.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya