RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
MFANYABIASHARA Ugur Gurses anacheza mchezo mchafu wa kibiashara wa kununua uneme wa TANESCO kwa bei ndogo na kuwauzia kwa bei ya ulanguzi wateja walionunua na kupanga nyumba zake.
Gurses ambaye ni raia wa Uturuki anamiliki kampuni ya Adamas Group inayojishughulisha na biashara ya nyumba ikiwa na ofisi zake Kariakoo, Dar es Salaam.
Kampuni hiyo ni mmiliki wa jengo refu la ghorofa lilipo Mtaa wa Livingston, Kariakoo ambalo linapangishwa na baadhi ya ghorofa zake zinauzwa.
Malalamiko dhidi ya vitendo vya ulanguzi vinavyofanywa Gurses yalitolewa jana, jijini Dar es Salaam na Haikal Hassan ambaye amenunua ghorofa moja katika jengo hilo ambaye alisema kuwa Gurses anacheza mchezo mchafu wa ulanguzi wa umeme.
Hassan alisema yeye amenunua moja ya ghorofa katika jengo hilo lakini Gurses amekataa kumruhusu kuweka mita yake kutoka TANESCO na badala yake anamuuzia umeme kwa shilingi kati ya 650 na 500 kwa uniti moja.
^Mimi nimenunua ghorofa hapa, lakini huyu jamaa mpaka leo anatulangua umeme kinyume kabisa na.maelekezo ya Serikali. Tangu niliponunua mpaka mwaka 2020 alikuwa anatuuzia sh 650 kwa uniti moja tukalalamika sana mpaka kwenye vyombo vya Serikali ndiyo akashusha kidogo akawa anatuuzia sh. 500.
“Kikawaida mimi baada ya kununua ghorofa yangu nilipaswa kuwa na mita yangu na ningekuwa nanunua umeme wa TANESCO lakini hapa kuna hizi mita za Bahdea wanatulangua kweli.
“Wameishakuja maafisa wa Serikali hapa na kuelekeza bei ishushwe lakini Gurses aliwakatalia akasema hashushi na kweli hakushusha na hajafanywa lolote,” alisema Hassan.
![]() |
Jengo la ghorofa lililopo Mtaa wa Livingstone Kariakoo ambalo mmiliki wake, Ugur Gurses analalamikiwa kuwalangua wateja wake umeme |
Alipoulizwa Meneja wa jengo hilo, Gibson Gabriel kuhusu ulanguzi huo wa umeme alisema ni kweli kuna tatizo kwenye bei lakini mamlaka za serikali kukosa nguvu ya kusimamia sheria ndiyo kunaumiza wananchi na kuwapa kiburi baadhi ya watu wenye fedha.
“Ni kweli hapa kuna tatizo, ni la siku nyingi.
Hili jengo linamilikiwa na watu wawili. Kuna huyo Gurses na kuna hawa Mar-Kim Chemicals Co. LTD. hizo ghorofa za juu zote wanaziuza na kuna wapangaji.
“Tanesco wana mita yao moja hapa ambayo ndiyo kubwa na wamiliki wamenunua mita ndogo ndogo kwa Kampuni ya Bahdea na kusambaza kila ghorofa. Hivyo wao huwa wanailipa na Tanesco na wanawauzia wakazi wengine wa humu.
“Tatizo ni kwamba bei wanayowauzia ni kubwa sana siyo iliyopangwa kisheria. Wamelalamika mpaka kwenye mamlaka za Serikali na barua zao zipo, hao maofisa wakaja hapa yule Mar- Kim Chemicals Co. LTD akakubali kushusha hadi sh 350 kwa uniti ila huyu Gurses aligoma. Wakaondoka naona hawakuwa na uwezo wa kumfanya chochote ila wanaoumia ni wapangaji maana bei ni kubwa mno,” alisema Gabriel.
Alipotafutwa Gurses kwa simu yake ya kigangani ili kuzungumzia malalamiko anayoelekezewa ya ulanguzi wa umeme alisema yupo kwenye kikao apigiwe baada ya saa moja. Alipopigiwa tena simu yake iliita bila kupokelewa na ilipopigwa tena na tena haikupokelewa.
Alipoulizwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha EWURA, Titus Kaguo kuhusu kadhia hiyo alisema EWURA iliruhusu watu wa majumba makubwa ambapo wamepanga wengi kutumia mita ndogo.
“EWURA iliruhusu kutumia Sub-meters, kwa maana kwamba mita ya Tanesco inawekwa pale unapoingilia umeme ambao kimsingi mara nyingi unakuwa umenunuliwa in bulk(kwa ujumla) then ili mpangaji kulipa kadri anavyotumia anawekea sub mita( mita ndogo) lakini gharama ya umeme haitakiwi kuzidi shilingi 292/- kwa UNIT Kwa T1 ambao unatumika majumbani.
“Therefore, Bahdea anatakiwa kutoza sh 292 kwa unit ambayo ilipitishwa na EWURA kwa matumizi ya majumbani.
Kama sivyo; watu wanatakiwa kuleta malalamiko katika ofisi zetu za Kanda ya Mashariki Kijitonyama PSSSF Ghorofa ya saba,” alisema Kaguo.
Tanzania PANORAMA Blog inaendelea kufuatilia kadhia hii