TERESIA MHAGAMA
KWA mara ya kwanza tangu aliteuliwe kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri na Nishati, Dotto Biteko amekanyanga ardhi ya kwao akiwa katika ziara ya kikazi.
Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe, mkoani Geita aliwasili jimboni humo Septemba 24, 2023 na kulakiwa kwa shangwe na wananchi na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Bukombe na Mkoa wa Geita.
Akizugumza katika mkutano wa hadhara jimboni humo, Biteko alimshukuru Rais
Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumkasimu madaraka ya Naibu Waziri Mkuu na kuahidi kutekeleza majukumu yake hayo mapya kwa ufanisi.
Alisema chini ya uongozi wa Rais Samia, kila kilichopangwa kufanyika kinafanyika ikiwemo utekelezaji wa miradi ya sekta mbalimbali; na aliitaja kwa uchache kuwa ni mradi wa jenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere litakalozalisha Megawati 2115, ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi, ununuzi wa ndege, ujenzi wa madarasa na vituo vya afya.
Aliwataka watendaji na watumishi kusimamia matumizi ya fedha za Serikali ili lengo la kuleta maendeleo yaliyokusdiwa kwa wananchi liweze kufikiwa.
Viongozi wa Mkoa wa Geita waliopata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo walimshukuru Rais Samia kwa kumuamini Biteko na walieleza imani yao kwa Biteko kuwa ataitendea haki nafasi aliyopewa kwa kuzintgatia historia yake kikazi.
Aidha, viongozi hao waliishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Geita ukiwemo ujenzi wa barabara wilayani Chato, ujenzi wa Chuo cha VETA wilayani Nyang’hwale na usambazaji umeme vijijini.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alimpongeza Biteko kwa kazi aliyoifanya alipokuwa Waziri wa Madini.
Alisema kazi iliyofanywa na Biteko katika wizara hiyo imesaidia kuinua mchango wa Sekta ya Madini katika uchumi wa nchi na aliahidi kuendeleza misingi mizuri aliyoiacha ikiwemo kufanya utafiti wa madini.
Aidha, Mavunde alionya kuwa hatakuwa na mzaha na watu wanaojihusisha na utoroshaji madini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo shule, hospitali na umeme katika Mkoa Geita.