Tuesday, December 24, 2024
spot_img

NI WAZIRI MOHAMED OMARY MCHENGERWA ALIYETOKOMEA NA NISSAN LA MSAADA TANAPA

RIPOTA PANORAMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Omary Mchengerwa ndiye aliyetokomea na gari la kisasa la mradi wa uhifadhi, aina ya Nissan Patrol – Wagon, lenye namba za usajili 02 JU 0480 lililotolewa msaada na Taasisi ya Frankfurt Zoological Society (FZS) kwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Vyanzo vya habari vya uhakika vya Tanzania PANORAMA Blog vimemtaja Waziri Mchengerwa kuwa ndiye kiongozi wa Serikali  aliyefanya ziara ya kikazi kwenye Hifadhi za Taifa kuanzia Juni 18, mwaka huu na kwamba TANAPA walimpatia gari hilo alitumie kwenye ziara yake hifadhini.

Imeelezwa kuwa gari hilo la kisasa, GID V8 Nissan Patrol  Wagon, toleo jipya lilimvutia Mchengerwa hivyo alipomaliza ziara yake alimuagiza dereva wake akalichukue alipeleke kwake na tangu wakati huo amekuwa akilitumia kama mali yake.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa gari hilo limekuwa likionekana sehemu mbalimbali Jijini Dar es Salaam pamoja na Mkuranga mkoani Pwani.

“Ni huyo Waziri Mchengerwa ndiye aliyetokomea nalo, lakini nani ana ubavu wa kumwambia alirudishe? Labda kama hujitaki maana utashughulikiwa na kusahaulika mara moja. Ni jambo la hatari sana kumgusa yule bwana.

“Alilichukua akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii na hata alipohamishwa wizara kwenda TAMISEMI hakulirudisha. Sasa ni zaidi ya miezi mitatu, ni kama amelichukua jumla gari la mradi wa uhifadhi, yapo mambo mengi  sana mbona tena ya kusikitisha?” kimesema chanzo chetu cha habari.

Gari hilo ni kati ya mawili yaliyokabidhiwa kwa TANAPA na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa baada ya kutolewa msaada ya Taasisi ya Frankfurt Zoological Society (FZS) ya Ujerumani kwa ajili ya shughuli za uhifadhi. Hafla ya kukadhi magari hayo pamoja na ya TAWA ilifanyika Disemba 20, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.   

Yeye mwenyewe Waziri Mchengerwa, Septemba 22, 2023, saa 5.30 alipigiwa simu mara kadhaa ili kupata kauli yake kuhusu gari hilo lakini hakupokea. Saa 5.35 alitumiwa maswali kwa maandishi kwenye simu yake ya kiganjani na kuyasoma lakini hakujibu chochote. Leo saa 6.15 alitumiwa ujumbe wa kuombwa kulizungumzia jambo hilo; ujumbe  ambao aliusoma lakini hakujibu chochote.

Septemba 22, 2023, baada ya Waziri Mchengerwa kupigiwa simu mara kadhaa bila kuipokea, Tanzania PANORAMA Blog ilimtumia maswali yaliyosomeka; ‘Juni 18, 2023 ukiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ulipofanya ziara hifadhini, TANAPA walikupa gani, Nissan Patrol Wagon lenye namba za usajili 02 JU 0484 kulitumia kwenye ziara yako hiyo.

‘Ulipomaliza ziara yako hukurudisha gari hilo bali ulitokomea nalo na taarifa zilizopo ni kwamba uliendelea kulitumia kwa shughuli zako binafsi na hata ulipohamishwa wizara kutoka Maliasili na Utalii kwenda TAMISEMI hukulirudisha na sasa ni zaidi ya miezi mitatu.

‘Mosi; PANORAMA inaomba kujua msingi na sababu za wewe waziri kuchukua gari hilo ambalo lilitolewa kama msaada kwa shughuli za uhifadhi na Taasisi ya Frankfurt Zoological Society ni zipi?

‘Pili; Sasa, ukiwa Waziri wa TAMISEMI, gari hilo mali ya TANAPA unalitumia kwa shughuli zipi? Na tatu; Una mpango wa kulirudisha au hapana na kama una mpango huo utalirudisha lini?

‘Nne; Kwa kuzingatia misingi na taratibu za uongozi, PANORAMA inaomba kupata kauli yako kuhusu viongozi wanaochukua magari ya taasisi za umma na kuyatumia kwa shughuli zao binafsi.’

Pia, Tanzania PANORAMA Blog ilimtafuta Mkurugenzi Mkazi wa Tanzania Frankfurt Zoological Society, Dk. Ezekiel Dembe na kumuuliza pamoja na mambo mengine,  iwapo FZS ina utaratibu wa kufuatilia misaada inayotoa ikiwa ni pamoja na magari kama inatumika kwa mujibu wa malengo yanayokusudiwa na iwapo msaada wowote utatumiwa kinyume cha malengo, hatua gani zinaweza kuchukuliwa.

Dk. Dembe aliomba atumiwe maswali kwa maandishi na kuahidi kuyafikisha kwa wataalamu wake Jumatatu (kesho) ili wayatafutie majibu.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya