*Jaji Mutungi atajwa kuibeba kwa vitendo falsafa ya R4 za Rais Samia
RIPOTA PANORAMA
OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imefungua ukurasa mpya wa mwenendo wa majadiliano ya kistaarabu wa masuala ya kisiasa unaoshirikisha wawakilishi wa makundi yote ya jamii nchini. Tanzania PANORAMA inaripoti.
Hayo yameelezwa na washiriki wa Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia ya vyama vingi ulioketi kwa siku tatu mapema wiki hii katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), uliopo Jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliofunguliwa Septemba 11, 2023 na Rais Samia Suluhu Hassan na kufungwa Septemba 13 na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman uliandaliwa na Baraza la Vyama vya Siasa chini ya uratibu wa moja kwa moja wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na ulikuwa mahususi kwa ajili ya kutathimini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi cha Rais Samia na hali ya kisiasa nchini.
Akizungumza katika mkutano huo, mwanasiasa mkongwe na mwanachama wa Chama cha NCCR Mageuzi, Joseph Selasini ambaye kwanza aliwasifu watoa mada kwa elimu waliyoitoa kwa washiriki, aliisifu pia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuratibu vizuri utekelezaji wa agizo la Rais Samia la kuitisha mkutano huo.
Selasini alisema watoa mada walitoa somo kubwa kuhusu falsafa ya R nne za Rais Samia alizopendekeza zifundishwe kwa viongozi wote ili waziishi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema ubunifu wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu namna ya kushirikisha makundi yote katika jamii kwenye mkutano huo umefungua ukurasa mpya kwa Watanzania wanaotofautiana kimtizamo na kiitikadi kuketi pamoja na kujadili mustabali wa kisiasa wa Taifa lao.
“Pili, nimejifunza Katiba ni maridhiano ya wananchi. Na kwa hili, niseme sasa wanasiasa tuache kufikiria kwamba Katiba ni mali yetu, Tume ya Uchaguzi ni mali yetu,” alisema Selasini.
Selesini alitoa rai kwa wanasiasa kujenga utamaduni wa kumuamini Rais Samia kwa sababu mchakato wa Katiba lazima usimamiwe na Serikali ambayo yeye ni kiongozi wake.
Ocheki Msuva wa Taasisi ya Youth for Change ambaye naye alipata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imefungua ukurasa mpya wa siasa za kistaarabu kwa kuwakutanisha wanasiasa, viongozi wa dini, wawakilishi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, vijana, watu wenye ulemavu na waandishi wa habari kujadiliana hali ya kisiasa ya Taifa lao.
Alishauri vijana wawe sehemu ya michakato yote inayoendelea badala ya kushirikishwa kwenye kutoa maoni tu huku akitoa mfano wa namna Ofisi ya Msajili ilivyowashirikisha katika mkutano huo uliojadili mambo muhimu ya kitaifa.
Mwakilishi kutoka Shirika la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Fatma Didia Chesa yeye alipendekeza Katiba Mpya itakayoundwa iwe na kipengele cha ufikiwaji watu wenye ulemavu huku naye akiomba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kuandaa mikutano ya aina hiyo ambayo inatoa fursa kwa Watanzania wa makundi yote kukutana pamoja na kuzungumza mambo yao.
Alisema funzo kubwa katika mkutano huo ni namna ulivyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ukiwakutanisha pamoja Watanzania wenye itikadi, misimamo na malengo tofauti.
Mwakilishi wa Shirika la Usawa wa Kijinsia Tanzania, Msafiri Mwajuma Mariam aliitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuandaa mikutano mingi ya aina hiyo na katika majadiliano ya aina hiyo, siasa ziwekwe pembeni.
Kiongozi Rai ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima, yeye alirejea hoja ya mmoja wa wachokoza mada, Deus Kibamba kuhusu mkwamo wa upatikanaji wa Katiba Mpya kwa kusema kuwa alikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba na wakati baadhi ya wajumbe waliposusa alikuwa mmoja wa waliowasihi wasisuse.
“Naipongeza sana Ofisi ya Msajili kwa hili jambo, hakika mmemsaidia sana Rais Samia na hata uratibu wa mkutano wenyewe hakuna anayeondoka akilalamika hapa, kila kitu kiko vizuri.
“Ninyi ni mfano wa kuigwa na naomba msichoke wala kuishia hapa, endeleeni kuliunganisha Taifa kwa mikutano kama hii inayotuleta pamoja kuzungumza mambo yetu, hakika historia utakukumbuka Jaji Mutungi na watendaji wako,” alisema.
Aliomba Rais Samia aungwe mkono na elimu ya Katiba itolewe ili changamoto ya watu kususia majadiliano kwenye uundwaji wa Katiba Mpya isiwepo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Dk. Joseph Mhagama alisema muundo wa Bunge hauna tofauti na muundo wa mkutano huo wa Baraza la Vyama vya Siasa.
“Composition ya Bunge ni copy ya Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa na replica ya jamii ya Watanzania. Ina akinamama, akinababa, ina vijana hivyo ajenda zote zinazohusu maeneo hayo zina uwakilishi mzuri hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi kuhusu maamuzi ya Bunge.
“Ina watu wenye ulemavu, imani tofauti, uwakilishi wa vyama vya siasa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali hivyo ina uwakilishi ulio kamilika unaoakisi muundo wa Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia ya vyama vingi na jamii ya Watanzania,” alisema Dk. Mhagama.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba yeye alimshukuru Rais Samia kwa kuwezesha shughuli za Taasisi ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambacho ni mwenyekiti wake kufanya kazi vizuri tangu alipoingia madarakani na kwamba sasa kimepata uhai mpya.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi alimshukuru Rais kwa jinsi ambavyo amekuwa akigharamia mikutano ya Baraza la Vyama vya Siasa na kurejea alichokisema Rais Samia akiwa Jijini Dodoma kuwa mambo ya msingi ya Taifa yatumie fedha za ndani na kwamba hilo amelithibitisha kwa vitendo kwa kugharamia mkutano huo kwa asilimia 100.
Alisema mikutano ya aina hiyo inasaidia kufungua fursa za wadau ambazo zimeminywa za kukaa pamoja kueleza changamoto zinazowatatiza na kwamba inasaidia kuondoa nyufa zilizopo.