RIPOTA PANORAMA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), mwezi huu litaanza kudaiwa na Kampuni ya Pan African Energy Tanzania (PAET), riba kubwa zaidi ya viwango vya riba vinavyotumika duniani (LIBOR).
Riba hiyo inatokana na deni la Shilingi bilioni 246.74, ambazo Tanesco inadaiwa na PAET kama gharama za mauzo ya gesi ambayo haijalipwa kwa muda wa miaka 10 sasa huku mkataba ukieleza kuwa unapofikia ukomo bila deni kulipwa, riba itaongeza kwa kiwango cha asilimia nne zaidi ya kiwango cha LIBOR, kila mwaka.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya mwaka 2021/22, mkataba wa mauziano ya gesi ambayo inatumika kuzalisha umeme katika vituo vya Ubungo 1, Ubungo 111 na Tegeta, ulisainiwa Juni 17, 2021 na pande zote mbili ambazo ni Tanesco na PAET na unamalizika Juni, 2023.
“Mkataba wa uuzaji gesi kati ya Shirika la Umeme Tanzania na Kampuni ya Pan African Energy Tanzania, ambayo inatumika kwa uzalishaji wa umeme katika Ubungo 1, Ubungo 111 na Tegeta, ulisainiwa tarehe 17 Juni, 2011 na unatarajiwa kumalizika Juni 2023.
“Unabainisha riba itaongezeka kwa kiwango cha asilimia 4 zaidi ya kiwango cha LIBOR, kila mwaka iwapo Shirika la Umeme Tanzania halitalipa kiasi kinachodaiwa kwa Kampuni ya Pan African Energy Tanzania.
“Katika ukaguzi wangu wa wadeni wa Shirika la Umeme Tanzania, nilibaini kuwapo kwa Ankara za Kampuni ya Pan African Energy Tanzania, ambazo hazijalipwa kwa miaka 10, kuanzia 2012/13 hadi 2021/22 zenye thamani ya Shilingi bilioni 246.74, ambayo inajumisha riba ya malipo yaliyocheleweshwa ya Shilingi bilioni 113.84.
“Hii imechangiwa na ukosefu wa fedha za kutosha kuwalipa watoa huduma na kusababisha gharama kuongezeka kwa taasisi,” anaeleza CAG.
Akitoa ushauri kuhusiana na deni hilo ambalo litaiingiza Tanesco kwenye mzigo mkubwa wa kulipa riba kubwa zaidi ya viwango vya riba vinavyotumika duniani, CAG anasema Tanesco ishirikiane na Wizara ya Nishati kutafuta njia mbadala za ufadhili ili kulipa deni hilo.
Anasema Ankara za kila mwezi za deni hilo zinapaswa kulipwa kwa wakati na PAET iitwe kwenye meza ya mazungumzo ili isitishe tozo ya riba kwa malipo yanayofuata.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande ametafutwa na Tanzania PANORAMA Blog ili kuzungumzia deni na riba itakayolipwa na shirika lake ambayo ni kubwa zaidi ya viwango vya riba vilivyowekwa duniani, lakini hakujibu chochote.