Monday, December 23, 2024
spot_img

SERA ZA FEDHA ZACHOCHEA UKOPAJI SEKTA BINAFSI

RIPOTA PANORAMA

UTEKELEZA wa sera za fedha na mpango wa Serikali kuboresha mazingira ya biashara, vimechochea kuongozeka kwa mikopo katika sekta binafsi ambayo sasa imefikia asilimia 22.5.

Hatua hizo, pia zimepunguza mikopo chechefu ambayo Aprili, 2021 ilikuwa asilimia 9.8 na sasa imeshuka hadi kufikia kiwango cha asilimia 5.5.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba aliyasema hayo Juni 15, mwaka huu bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akiwasilisha Bajeti ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/24.

Kwa mujibu wa Dk, Nchemba, utekelezaji huo wa sera umeshusha viwango vya riba za mikopo ya benki kutoka wastani wa asilimia 16.58, mwezi aprili, 2021 hadi kufikia wastani wa asilimia 15.91, mwezi Aprili, 2023.

“Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha pamoja na utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuboresha mazingira ya biashara nchini.

“Utekelezaji wa sera hizo umesababisha kushuka kwa viwango vya riba za mikopo ya benki, ambapo katika kipindi cha mwaka kinachoishia Aprili 2023, kiwango cha riba za mikopo kilipungua na kufikia wastani wa asilimia 15.91, kutoka wastani wa asilimia 16.58 mwezi Aprili, 2021.

“Kupungua kwa viwango vya riba za mikopo kumechangia kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi  ambapo mikopo hiyo imeongezeka kwa asilimia 22.6, Aprili, 2023 ikilinganishwa na asilimia 4.8, Aprili, 2021,” alisema Dk. Nchemba,

Aidha, Dk. Nchemba alisema mapato ya ndani yamekuwa yakiongezeka; kwa 2021/22 yamefikia Shilingi trilioni 24.40 ikilinganishwa na mwaka 2020/21 yalipokuwa Shilingi trilioni 20.59.

Alisema, mwezi Julai, 2022 hadi Aprili 2023, ukusanyaji wa mapato ya ndani ulifikia Shilingi trilioni 21.67 huku mwezi Disemba, 2023 Mamlaka ya Mapato (TRA) ikivunja rekodi kwa kukusanya Shilingi trilioni 2.63, kiasi  ambacho ni kikubwa kuwahi kukusanywa katika historia ya mamlaka hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 1996.

Dk. Nchemba alisema Serikali inatambua umuhimu wa kuwezesha wananchi kiuchumi wakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu hivyo inafanyia kazi changamoyo zilijitokeza katika ugawaji na urejeshwaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

“Utaratibu mpya wa utolewaji na urejeshwaji wa mikopo hiyo utakapokamilika, Serikali itatoa taarifa kwa umma na kuendelea kutoa mikopo hiyo.

“Napendekeza kuweka Shilingi bilioni moja kwenye mfuko wa watu wenye ulemavu kwa ajili ya kusaidia vifaa vinavyohitajika. Fedha hizo pia zitatumika kama mfuko wa wabunge wa kundi la watu wenye ulemavu na mchango kwa watoto wanaolelewa katika vituo maalumu,” alisema Dk. Nchemba.

Pia alitoa wito kwa makampuni na watu binafsi kuchangia katika mfuko huo ili kuyasaidia makundi maalumu sambamba na programu inayotekelezwa na Serikali, chini ya TASAF.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya