RIPOTA PANORAMA
KAMPUNI ya M/S Grumeti Reserve Ltd imeitia hasara Serikali ya jumla ya Shilingi milioni 241.23.
Hasara hiyo kwa Serikali imesababishwa na uamuzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyapori (TAWA), kusamehe ada za Serikali kwa Kampuni ya M/S Grumeti Reserve Ltd kinyume na kanuni ya 16 (1) na (2) (a) I-XX za kanuni za uhifadhi wanyamapori za mwaka 2016, zinazoelekeza shughuli yoyote inayofanyika katika eneo la uhifadhi kulipiwa ada.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), katika ripoti yake ya 2021/22 anasema, ukaguzi wake kwa TAWA ulibaini kuwapo kwa waongozaji watalii 2,053 wanaoshirikiana na kampuni hiyo kuingia ndani ya Hifadhi ya Pori la Akiba la Grumeti lililopo Serengeti bila kulipa ada ya kuingia.
CAG anasema TAWA ilieleza kuwa kikao chake cha menejimenti kilichofanyika Septemba 16, 2020 kiliamua kusamehe ada za Serikali kwa kampuni hiyo wakati akifanya shughuli zake ndani ya eneo la hifadhi.
Anasema uamuzi huo wa Menejimenti ya TAWA unakiuka kanuni za uhifadhi wanyapori za mwaka 2016 na uliisababishia hasara Serikali ya mamilioni hayo ya fedha.
“Wakati wa ukaguzi wa TAWA nilibaini kuwa kuna Kampuni iitwayo M/S Grumeti Reserve Ltd, imekuwa ikifanya shughuli za utalii ndani ya Hifadhi ya Akiba ya Grumeti iliyopo Serengeti. Hata hivyo, baada ya ukaguzi wa kina nilibaini kuwa waongoza watalii 2,053 wanaoshirikiana na M/S Grumeti Reserve Ltd wamekuwa wakiingia ndani ya pori la akiba bila kulipa ya kiingilio, ambayo ni jumla ya Shilingi milioni 241.23,” anasema CAG.
Anatoa ushauri kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya uchunguzi wa kina kuhusu uamuzi huo wa TAWA kusamehe mapato ya Serikali na pia kutambua mapato yaliyopotea tangu kuanza kwa shughuli za kampuni hiyo kisha kuchukua hatua stahiki za kurejesha fedha hizo.
Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta bila mafanikio Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamedi Mchengerwa ili kupata kauli ya Serikali kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa kutokana na hasara hiyo na utekelezaji wa ushauri wa CAG.