RIPOTA PANORAMA
SERIKALI imesema Benki ya Biashara ya DCB inayoimiliki; hesabu zake hazijapata kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa sababu sheria iliyokuwapo awali iliwaruhusu wanahisa kuchagua mkaguzi wa mwaka husika kwenye mkutano mkuu wao wa mwaka.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Gerson Msigwa ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akiieleza Tanzania PANORAMA Blog sababu za kutokaguliwa kwa hesabu za benki hiyo na CAG tangu kuanzishwa kwake, zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Msigwa amesema hesabu za Benki ya Kibiashara ya DCB kwa mwaka 2022 zilikaguliwa na mkaguzi aliyemtaja kwa jina la PWC, na kwamba mkaguzi huyo huwa anatumiwa pia na CAG kukagua mabenki kwa niaba yake.
“Kwa mwaka 2022, hesabu zake zimekaguliwa na PWC ambaye wakati mwingine CAG humtumia kukagua mabenki kwa niaba yake,” amesema Msigwa.
Hata hivyo, CAG katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/22, anaandika akiishauri Serikali kupitia Hazina kuhusu hesabu za Benki ya DCB, kutekeleza uzingatiaji wa kifungu cha 30(b) na (e) cha sheria ya ukaguzi wa umma ya mwaka 2008 ambacho kinazitaka taasisi zote ambazo Serikali imewekeza fedha zake na zile ambazo ni mwanahisa mkubwa kuwasilisha hesabu zao kwake kwa ajili ya kukaguliwa.
Kwamba benki hiyo ilipata usajili Septemba 6, 2001 na Aprili, 2002 ilianza biashara kama taasisi ya kifedha ya kanda hadi Juni12, 2003 ilipopewa leseni ya kufanya biashara ya benki ikijulikana kwa jina la Dar es Salaam Community Bank (DCB).
CAG anaeleza kuwa benki hiyo hivi sasa inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 63, ingawa awali ilianzishwa kama benki binafsi iliyosajiliwa chini ya sheria ya makampuni na kwa hiyo hakuna sheria ya Bunge ya kuanzishwa kwake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kibiashara ya DCB, Isdoru Msaki.
Kwenye ripoti yake, CAG anasema ni matakwa ya kisheria kwa mujibu wa ibara ya 143 kifungu cha 9(a) iii & iv cha sheria ya ukaguzi wa umma; taasisi ambazo Serikali imewekeza fedha zake na zile ambazo ni mwanahisa mkubwa kuwasilisha taarifa zake za fedha ofisini kwake kwa ajili ya kukaguliwa.
Msigwa ameiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa wanahisa wa Benki ya Kibiashara ya DCB wameishakubaliana kuwa hesabu za benki hiyo kwa mwaka unaoishia Disemba 2023 zikaguliwe na CAG.
Amesema Serikali tayari imekwishazijulisha benki zote ambazo ina hisa zizingatie matakwa ya sheria ya ukaguzi wa umma kama ilivyorekebishwa ili hesabu zao zikaguliwe na CAG mwenyewe au taasisi atakayoichagua kukagua hesabu zao kwa niaba yake.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kibiashara ya DCB, Isdori Msaki ambaye Mei 22, 2023 pamoja na mambo mengine, aliulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu mwenendo wa benki anayoiongoza kukinzana na matakwa na Katiba ya Nchi, naye aliahidi kulizungumzia hilo lakini mwishowe alisema hayo ni mambo ya kiserikali na kwamba mwenye majibu ya kutokaguliwa kwa hesabu za benki hiyo na CAG ni CAG mwenyewe.
Serikali ina umiliki wa asilimia 63 ya mtaji wote kwenye Benki ya Kibiashara ya DCB kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni yenye hisa mbili, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo yenye hisa asilimia 2.96, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni yenye hisa asilimia 5.74 na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke yenye hisa asilimia 3.49.
Umiliki wa Serikali kwenye benki hiyo, pia unapitia Mfuko wa Taifa wa Bima Afya (NHIF) ambayo ina hisa asilimia 6.12, Halmashauri ya Jiji la Ilala ina hisa asilimia 8.12, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ina hisa asilimia 10.65, Mfuko wa Uwekezaji (UTT) una hisa asilimia 23.69 huku wanahisa wengine wakiwa na hisa asilimia 36.89.