Wednesday, December 25, 2024
spot_img

KOMPYUTA YA MAPATO YA JESHI LA POLISI HAINA ‘PASSWORD’

RIPOTA PANORAMA

KOMPYUTA ya Jeshi la Polisi yenye mfumo wa mapato ya ulinzi yanayotokana na tuzo na tozo haina nywila (password), hivyo inaweza kutumiwa na mtu yoyote.

Sambamba na hilo, mfumo wa mapato ya ulinzi wa Jeshi la Polisi yanayotokana na tuzo na tozo, haujaunganishwa na mfumo wa ukusanyaji mapato serikalini (GePG), hivyo ni mfumo unaojitegemea.

Haya yamo kwenye Ripoti ya Ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2021/22; ambayo inaeleza pamoja na mambo mengine; Jeshi la Polisi limekuwa likitengeneza ankara za malipo bila ya kuwa na nambari ya malipo (Control number).

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, Jeshi la Polisi lina mhasibu mmoja ambaye ana uwezo wa kuufukia na kuudhibiti kikamilifu mfumo wa mapato ya ulinzi, ikiwa ni pamoja na kutengeneza ankara, kupitisha ankara, kuchapisha ankara na kuhifadhi taarifa za makusanyo.

Ripoti ya ukaguzi maalumu na wa kiuchunguzi ambao CAG aliufanya kwenye Jehi la Polisi baada ya kuombwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, inaeleza kuwa kwa mujibu wa amri za jumla za polisi (PGO), Jeshi la Polisi Tanzania linatakiwa kuanzisha mfuko wa tuzo na tozo ambao unaendeshwa kwa kutoa huduma za ulinzi kwenye taasisi mbalimbali.

Zinatajwa taasisi hizo kuwa ni pamoja na Taasisi za Serikali, benki za biashara, maeneo ya uchimbaji madini na kampuni binafsi na kwamba; fedha zinazopatikana kwa utoaji wa huduma hizo zimelengwa kusaidia familia za maafisa wa polisi waliofariki, kutoa zawadi kwa maafisa wa polisi walioathiriwa na mashambulizi ya silaha na kugharamia matumizi mengineyo yenye manufaa kwa Jeshi la Polisi.

“Hata hivyo, malipo kutoka kwenye mfuko huu yanaweza tu kufanywa kwa idhini ya Mlipaji Mkuu wa Serikali ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

“Katika uchunguzi wangu, niligundua kuwa Jeshi la Polisi (TPF) lina akaunti ya benki katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mahususi kwa ajili ya kukusanya fedha zinazohusiana na tuzo na tozo zinazotokana na huduma za ulinzi,” inasomeka ripoti.

Ripoti inaonyesha kuwa kati ya Julai 2018 na Novemba 2021, akaunti ya Jeshi la Polisi ilipokea jumla ya Shilingi bilioni 38.23 kutoka taasisi 60 zikiwemo 10 ambazo ni za Serikali, benki 30, maeneo 13 ya uchimbaji madini na mashirika binafsi saba.

“Uchunguzi wangu ulibaini kuwa taasisi 31 zilikuwa zimepokea huduma za ulinzi kutoka Jeshi la Polisi lakini mikataba yao ilikuwa imemalizika bila malipo ya Shilingi bilioni 2.26.

“Pia nilibaini kuwa Jeshi la Polisi lilishindwa kukusanya madeni ya huduma za ulinzi yenye jumla ya Shilingi bilioni 1.62 kutoka taasisi 28 ambazo zilikuwa na mikataba halali. Aidha, nilibaini kuwa Jeshi la Polisi lilikuwa limetoa huduma za ulinzi kwa mojawapo ya benki ya kibiashara bila kuwa na mkataba.

“Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa ukusanyaji wa fedha za mfuko wa tuzo na tozo ulikuwa ukifanyika kupitia mfumo wa mapato ya ulinzi ambao haukuunganishwa na mfumo wa ukusanyaji mapato serikalini,” anaeleza CAG katika ripoti yake.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Dabid Misime.

CAG anaeleza zaidi kuwa Jeshi la Polisi lina mhasibu mmoja mwenye uwezo wa kuufikia na kuudhibiti kikamilifu (full Control) mfumo wa mapato ya ulinzi hivyo kuwepo hatari kubwa ya udanganyifu wa makusanyo ya fedha za mfuko huo.

Akiendelea, anasema Jeshi la Polisi lilikosa mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na hivyo kushindwa kukusanya mapato ya ulinzi yenye jumla ya Shilingi bilioni 3.88 kutoka kwa wateja ambao mikataba yao iliisha muda wake na wateja waliokuwa na mikataba halali.

Akihitimisha ripoti yake ya ukaguzi na uchunguzi maalumu kwa Jeshi la Polisi katika eneo hilo, CAG anasema jeshi hilo likusanye madeni yote, lihuishe mikataba iliyoisha muda wake na liunganishe mfumo wa mapato ya ulinzi na mfumo wa ukusanyaji mapato serikalini (GePG).

“Hii itawezesha ufuatiliaji na usimamizi mzuri wa fedha za mfuko wa tuzo na tozo. Aidha, Jeshi la Polisi linapaswa kuanzisha mifumo ya udhibiti kama vile nywila na vikwazo vya upatikanaji wa mfumo (restricted access control) ili kupunguza hatari za udanganyifu na kughushi na hivyo kuimarisha uwazi na uwajibikaji,” anasema CAG.

Tanzania PANORAMA Blog imemuuliza maswali kadhaa Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura kupitia kwa Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime na moja ya maswali hayo linauliza; ni kwanini kompyuta ya jeshi hilo yenye mfumo wa mapato ya ulinzi haina nywila? Hata hivyo maswali hayo hayakupata majibu.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya