Tuesday, December 24, 2024
spot_img

BILIONI 5.8 ZA ELIMU BILA MALIPO ZAPELEA – CAG

RIPOTA PANORAMA

SERIKALI haikutoa Shilingi bilioni 5.8 za ruzuku ya kugharamia elimu bila malipo zinazohitajika katika mamlaka 25 za Serikali za Mitaa, mwaka wa fedha 2021/22.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2021/22, inaeleza kuwa kiasi hicho cha fedha kilipungua kwenye Shilingi bilioni 33.07 zinazohitajika kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya kugharamia elimu bure.

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, upungufu wa fedha za ruzuku ya elimu bila malipo unaathiri matokeo ya wanafunzi kitaaluma kwa sababu shule nyingi hazina mahitaji muhimu, ikiwemo miundombinu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

“Aya ya kwanza na pili za waraka wa ruzuku kwa shule za sekondari kuhusu utoaji elimu bila malipo, wenye kumb. Na. DC.297/507/01/39 kwa shule za msingi na kumb. Na. DC.297/507/01/40 kwa shule za sekondari, uliotolewa disemba 28, 2015 unataka Serikali kutoa fidia ya Shilingi 10,000 na Shilingi 25,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka kwa shule za msingi na sekondari mtawalia.

“Katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali haikutoa ruzuku ya fedha za kugharamia elimu bure, Shilingi bilioni 5.8 kati ya Shilingi bilioni 33.07 zilizohitajika katika mamlaka 25 za Serikali za mitaa,” inasomeka ripoti ya CAG.

Sambamba na hilo, CAG anaeleza katika ripoti yake kuwa tathmini yake kwenye miundombinu mashuleni ilibaini kuwa shule za msingi na sekondari katika mamlaka 45 za Serikali za Mitaa zilikuwa na upungufu wa miundombinu.

Anataja uhaba wa miundombinu uliopo katika shule za msingi kuwa ni madawati 158.066, vyoo vya wanafunzi 56,530, nyumba za walimu 35,684, viti na meza 29,829, madarasa 27,316, ofisi za walimu 2,266 na vyoo vya walimu 622.

Kwa upande wa elimu ya sekondari, CAG anaeleza kuwa kuna upungufu wa viti na meza za wanmafunzi 31,608, nyumba za walimu 13,566, viti na meza za walimu 11,975, vyoo vya wanafunzi 8,360, maabara 2,460 na mabweni 986.

Anataja pia kuwepo kwa uhaba wa ofisi na majengo ya utawala 966 kwa shule za sekondari, vyoo vya walimu 892, madarasa 783, maktaba 390, vyumba vya chakula 244, vyumba vya kompyuta 131 na majiko 111.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, CAG anasema Serikali, Hazina na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zinapaswa kuhakikisha fedha zinazoidhinishwa kwa ajili ya kugharamia utoaji wa elimu; zinatolewa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuimarisha utoaji wa elimu bora nchini.

Aidha, CAG anaeleza zaidi kuwa ufaulu wa kitaaluma unategemea mazingira mazuri ya kujifunzia hivyo zinahitajika juhudi kushughulikia uhaba wa miundombinu katika shule za msingi na sekondari.

“Vilevile uhaba wa vyumba vya madarasa huwalazimu wanafunzi kusomea katika madarasa yenye msongamano wa wanafunzi, jambo ambalo linadumaza uwezo wa kujifunza na walimu kufundisha kwa ufanisi hivyo kuingilia kati mara moja kushughukia uhaba huu wa miundombinu ya shule ni jambo lisiloepukika.

“Ninashauri Hazina kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoa fedha kwa mujibu wa bajeti iliyoidhinishwa na kuendelea kuboresha miundombinu ili kuondoa au kupunguza upungufu wa miundombinu kwenye shule za msingi na sekondari kwa ajili ya kuimarisha utoaji elimu bora,” inasomeka ripori ya CAG.

Jitahada za Tanzania PANORAMA Blog kumpata Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda kuzungumzia kupelea kwa fedha za elimu bila malipo na uhaba wa miundombinu mashuleni hazijaa matunda.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya