Thursday, March 13, 2025
spot_img

NANI MHUJUMU SEKTA YA UTALII TANZANIA? (2)

 

Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Allan Kijazi

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Allan Kijazi ndiye kiongozi mwandamizi wa serikali aliyeulizwa na Tanzania PANORAMA blog kuwa ni nani anaihujumu Sekta ya Utalii Tanzania akakaa kimya.

Dk. Kijazi ameamua kukaa kimya bila kujibu maswali 10 aliyoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, amefumba mdomo na ni kama ameweka kalamu yake chini kwani hata alipoandikiwa maswali kwa maandishi, takriban mwezi mmoja sasa hajapata kujibu chochote.

Kama ilivyo kwa Dk, Kijazi, mwanasheria mkuu wa zamani ambaye sasa ni mwanasheria wa Kampuni ya Hotel and Lodges, Jaji Frederick Werema naye hakujibu maswali aliyoulizwa licha ya kuahidi kutoa ushirikiano hapo awali.

Jaji Frederick Werema
 

Katika mawasiliano yake na Tanzania PANORAMA Blog, Jaji Werema badala ya kujibu maswali aliyoulizwa, aliandika ujumbe mfupi kwenye simu ya mkononi na kuutuma kwa njia ya whatsapp.

Aliandika; ‘Kampuni ya mawakili ninayoiwakilisha siyo washauri wa kampuni unayoizungumzia. Sisi tuliajiriwa kwa ajili ya kuishauri na kuiwakilisha mahakamani. Hatuna maagizo kutoka kwao ya kuwasemea katika uwekezaji wao.

‘Kwa hiyo hatuna ruhusa ya kujibu maswali hayo. Unashauri kuwatafuta mwenyewe au mawakili wao wa ndani kujibu hojaji zao.’ Jaji Werema aliandika ujumbe huo Okotoba 9, 2021. 

Baada ya kupokea ujumbe huo wa maandishi wa Jaji Werema, Tanzania PANORAMA Blog ilimwandikia hivi; ‘Sawa mheshimiwa. Nilikuomba contact zao na uliahidi kunipatia, naomba ili niwasiliane nao.’

Jaji Werema alijibu, ‘Nadhani unaweza kupata mawasiliano hayo. Bila shaka umekwenda Brela na mawasiliano hayo yapo kwenye kumbukumbu hizo.’

Tanzania PANORAMA Blog ilimwandikia tena Jaji Werema kumueleza hivi; ‘Sawasawa, mimi nilizingatia mazungumzo yetu ya jana ndiyo maana nikabaki na matumaini kutoka kwako.’ Jaji werema aliusoma ujumbe huo na kukaa kimya.

Oktoba 25, 2021 Tanzania PANORAMA Blog ilimtumia Jaji Werema ‘link’ yenye habari kuhusu sakata la nani anaihujumu Sekta ya Utalii Tanzania, alisoma na kukaa kimya hadi Oktoba 26, 2021 alipotuma ujumbe kupitia simu yake ya kiganjani akiomba nakara ya gazeti lenye habari hiyo, aliandika; ‘ninaomba nakara ya gazeti hili.’

Hoteli Lobo
 

Kwa upande mwingine, Tanzania PANORAMA Blog iliwasiliana na Katibu Mkuu, Dk. Kijazi kwa mara ya kwanza kuhusu sakata hili Septemba 27, 2021 kwa kumtumia ujumbe wa maandishi kwenye simu yake ya kiganjani baada ya simu yake kutopokelewa mara kadhaa.

Tanzania PANORAMA Blog iliandika ikiomba kupata kauli ya Dk, Kijazi kuhusu hotel tatu zilizo chini ya TANAPA ambayo imempa mwekezaji, Kampuni ya Hotel and Lodges kuziendesha lakini anatuhumiwa kuzitelekeza na kuhujumu jitihada za serikali kukuza sekta ya utalii.

Iliandika zaidi kuwa, ‘na zaidi kucheza mchezo mchafu na viongozi wa wizara na TANAPA ili iendelee kuziendesha wakati kuna wawekezaji wenye uwezo wa kuziendesha wanazihitaji.’

Dk. Kijazi alisoma ujumbe huo lakini hakujibu chochote hivyo jitihada za kumpigia simu ziliendelea lakini hazikufanikiwa.

Oktoba 8, 2021, Tanzania PANORAMA Blog ilimuandikia maswali 10 Dk. Kijazi. Maswali hayo haya hapa.

Dk. Kijazi

 

Mosi; Kampuni ya Hotel and Lodgers, pamoja na kufanya biashara nyingine imekabidhiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), kuendesha hotel zake tatu ambazo ni Manyara, Lobo na Soronera, pamoja na Hoteli ya Ngorongoro Wild Life inayomilikiwa na NCAA. Naomba kufahamu kutoka kwako katibu mkuu ambaye wakati kampuni hiyo inakabidhiwa hoteli hizo ulikuwa Kamishna Mkuu wa TANAPA.

A)       Vigezo vilivyotumika kuipa kampuni hiyo uendeshaji wa hotel hizo?

B)        Mkataba wa uendeshaji hoteli hizo ni wa muda gani?

C)        Kuna ukaguzi wowote unaohusu utolewaji wa huduma, matunzo na ukarabati wa hoteli hizo?

D)      Kuna kampuni nyingine zilizoonyesha nia ya kuendesha hoteli hizo?

E)        Kampuni nyingine zilizoonyesha nia ya kuziendesha hoteli hizo zinazidiwa kwa kiwango gani cha vigezo vilivyowekwa vya uendeshaji wa hoteli hizo na Kampuni ya Hotel and Lodges?

Pili; Kampuni ya Hoteli and Lodges imetajwa kuwa moja kati ya makampuni yanayojihusisha na vitendo vya uhujumu uchumi na kuikosesha nserikali mapato yatokanayo na fedha za kigeni baada ya kubainika kuziua kibiashara kwa kutozifanyia matengenezo na kutoa huduma mbovu zisizokidhi viwango vya biashara kwa hoteli za kitalii iliyokabidhiwa kuziendesha na TANAPA na NCAA. Jambo hili unalizungumzije?

3) Kampuni ya Hotel and Lodgers imeajiri menejimenti ya kigeni kutoka taifa la Kenya ambalo ni washindani wakubwa wa biashara ya utalii na Tanzania na zipo taarifa kuwa menejimenti hiyo ya kigeni ni mhusika mkuu wa uhujumu wa hoteli hizo. Wewe kama katibu mkuu na pia uliyekuwa Kamishna Mkuu wa TANAPA kwa muda mrefu unafahamu kuwa menejimenti ya hoteli hizo ni ya kigeni?

B) Na je menejimenti hiyo ya kigeni imekuwa ikitekeleza wajibu wake sawasawa?

C) Ukiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, ni nini mtizamo wako kuhusu jambo hili kwa kuzingatia maslahi mapana ya Sekta ya Utalii Tanzania?

4) Ofisi za menejimenti inayoendesha hoteli hizi ipo nchini Kenya na si Tanzania? Kwa faida ya wasomaji wa Blog ya PANORAMA na watanzania wote, naomba kujua ni kwanini ofisi za menejimenti inayoendesha hoteli hizi ipo nchini Kenya?

5) Mwezi Mei mwaka jana, iliundwa tume ya kuchunguza matatizo ya hoteli hizo baada ya kubainika kuwa zipo kwenye hali mbaya na watalii wanazikimbia. Tume hiyo ilibaini upungufu mwingi kwenye hoteli hizo na baada ya kuwasilisha ripoti katika mamlaka za serikali, Kampuni ya Hotel and Lodges iliagizwa kuzifanyia ukarabati ndani ya siku 90.

A) Jambo hili unalifahamu?

B) Na je maelekezo hayo mahususi ya serikali yalitekelezwa kwa kiwango gani?

6) Serikali ilitoa muda zaidi hadi kuwa mwaka mmoja kwa Kampuni ya Hotel and Lodges kukarabati hoteli hizo.

A) Jambo hili unalifahamu?

B) Maelekezo hayo ya serikali yalitekelezwa kwa kiwango gani?

7) PANORAMA Magazine na Tanzania PANORAMA Blog zina taarifa kuwa hadi sasa Kampuni ya Hotel and Lodges imekaidi maelekezo ya serikali ya kuzikarabati hoteli hizo kwa kiwango cha kuzirejesha kwenye ubora wake wa awali wa kuhudumia watalii. Ni hatua gani zilichukuliwa na TANAPA na Wizara ya Maliasili na Utalii kutokana na ukaidi wa kampuni hiyo?

8) Tanzania PANORAMA blog na PANORAMA Magazine zinafahamu kuwa Septemba 22, 2021, Kampuni ya Hotel and Lodges ilinyang’anywa Hoteli ya Ngorongoro Wild Life kwa sababu ya kukaidi maelekezo ya serikali ya kukarabati hoteli hiyo. Hili inalifahamu? Na unalizungumziaje?

9) Kampuni hii pia imenyang’anywa hoteli mbili zilizoko Zanzibar baada ya kubainika kushindwa kuziendesha sambamba na kujihusisha na vitendo vya uhujumu uchumi wa Zanzibar. Hili unalifahamu? Na unalizungumziaje?

10) Watanzania wengi wamekosa ajira katika hoteli hizo kutokana na kuwa chini ya menejimenti ya kigeni inayoendesha hoteli hizo kutokea nje ya nchi. Wewe ukiwa mmoja wa viongozi wanaoheshimika hapa nchini uliyepata kuwa na jukumu zito la Kamishana Mkuu wa TANAPA na sasa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasilia na Utalii, una kauli gani kuhusu hilo?

naomba ushirikiano wako.

D

Dk Kijazi

Dk, Kijazi aliyasoma maswali hayo lakini hakujibu chochote.

Oktoba 25, 2021 baada ya Dk Kijazi kusoma habari iliyoripotiwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu sakata la hoteli hizo, kwa kutumia simu yake ya kiganjani alituma ujumbe wa viganja vya mikono vilivyoshikana kuashiria kushukuru.

Dk. Kijazi ndiye mtu anayedaiwa kuwa katikati ya sakata hili na mwenye majibu sahihi ya maswali yanayoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu madai ya kuwepo vitendo vya hujuma katika sekta ya utalii.

Aidha, uamuzi wake wa kukaa kimya ulielezwa mapema na vyanzo vya habari kuwa hataweza kujibu maswali hayo na ipo shaka kuwa hilo linasababishwa na mkutano wake na wajumbe wa Kampuni ya Hotel and Lodges iliomfikia ikiwa na ujumbe mahususi siku chache kabla ya kuanza kazi kwa tume ambayo ripoti yake ilipendekeza Kampuni ya Hotel and Lodges kunyang’anywa hoteli hizo.

RIPOTI HII INAENDELEA.

  

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya