Thursday, March 13, 2025
spot_img

DK. KIJAZI – NIPENI MUDA, NITASEMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Allan Kijazi

 

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

HATIMAYE Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Allan Kijazi ametoa kauli kuhusu maswali magumu yaliyoelekezwa kwenye wizara yake pasipo kupatiwa majibu kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Dk. Kijazi aliwasiliana na Tanzania PANORAMA Blog jana kupitia simu yake ya kiganjani na kueleza kuwa atajibu maswali yote aliyoulizwa baada ya kukamilika kwa taratibu za ndani za serikali, hivyo apewe muda kidogo.

Kauli hii ya Dk. Kijazi iliitoa alipokuwa ikijibu maswali mengine ya ziada aliyoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu sakata hilo. Maswali hayo aliyajibu papo hapo kisha akagusia maswali kumi ambayo hajayajibu.

“Hili suala lipo kwenye majadiliano ya ndani kwenye vyombo vya serikali. Nitalitolea kauli na kujibu maswali yako taratibu za ndani ya serikali zikikamilika. Nipe muda kidogo.” Alisema Dk. Kijazi.

Aidha, Dk Kijazi alikanusha kukutana na kufanya mazungumzo na mwanasheria wa Kampuni ya Hotel and Lodges, Ahmad El Maamry kabla tume iliyoundwa kuchunguza matatizo ya hotel za kitalii zenye hadhi ya nyota tano za Manyara, Lobo, Soronera na Ngorongoro, haijaanza kufanya kazi yake.

Dk. Kijazi alisema alikutana na mwanasheria huyo ofisini kwake alipokwenda kujitambulisha kuwa ndiye mwanasheria ya Kampuni ya Hotel and Lodges, akichukua majukumu ya baba yake ambaye alikuwa mgonjwa, Said El Maamry.

“Mwanasheria El Maamry alikuja kuniona baada ya tume kuwasilisha taarifa, aliwasilisha utetezi wa mteja wake kuhusu taarifa husika. Hilo ni tatizo? Na uelewe pia tume ilipoundwa mimi sikuwa na madaraka niliyonayo sasa wizarani.

“Siyo kweli kwamba alikuja kabla ya tume. Kwangu alikuja kujitambulisha kama mwanasheria wa kampuni, majukumu ambayo amekabidhiwa na baba yake alikuwa mwanasheria wa kampuni na alikuwa anaumwa asingeweza kushughulikia mgogoro huo.

“Fuatilia ujue tume iliundwa lini, ilifanya kazi zake lini, iliwasilisha ripoti lini na yeye alikuja OFISINI, nasisitiza OFISINI kwangu lini. Hatujakutana kwenye baa au hotelini. Naomba niishie hapo,” alisema Dk. Kijazi.

Wakati Dk. Kijazi akieleza kumtambua El Maamry kama mwanasheria wa Kampuni ya Hotel and Lodges, yeye mwenyewe El Maamry, amekanusha zaidi ya mara moja kuwa mwanasheria wa kampuni hiyo.

El Maamry amekuwa na kauli zinazopishana kuhusu sakata hili na mara kadhaa ameeleza kuwa Jaji Frederick Werema ndiye mwanasheria wa Kampuni ya Hotel and Lodges, lakini Jaji Werema naye amekwishasema kuwa yeye aliajiriwa na kampuni hiyo kuisimamia mahakamani tu, hivyo masuala mengine ya kisheria yanashughulikiwa na wanasheria wa ndani ya kampuni hiyo.

Kampuni ya Hotel and Lodges iliyopewa hotel nne za kitalii zenye hadhi ya tano kuziendesha inadaiwa kuzitelekeza pasipo kuzifanyia matengenezo yanayoendana na hadhi yake, kutoa huduma mbovu, kuhujumu mapato ya serikali kwa kuzikosesha hoteli hizo wateja (watalii), kuajiri menejimenti ya kigeni na menejimenti hiyo kufanya kazi ikiwa Kenya, taifa mshindani mkubwa wa biashara ya utalii na Tanzania.

Inaelezwa kuwa hayo yalibainika baada ya aliyekuwa kiongozi mwandamizi katika serikali ya awamu ya tano kuzitembelea na kukuta zina hali mbaya kiasi cha maji ya kuoga na kunawa uso kuchotwa kwenye ndoo na kupelekewa wateja vyumbani.

Kubainika kwa dosara hizo kuliifanya serikali kuunda tume ya kuchunguza matatizo ya hotel hizo na mwenendo mzima wa uendeshaji wake.

Tume hiyo baada ya kukamilisha kazi yake ilitoa mapendekezo kadhaa, ikiwemo Kampuni ya Hotel and Lodges kunyang’anywa hoteli hizo lakini ikaamriwa ipewe muda wa kuzikarabati, jambo ambalo imekuwa ikilifanya kwa kusuasua huku ikikaidi kutekeleza mapendekezo mengine likiwemo la kuhamishia menenjimenti Arusha, Tanzania.

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya