Wednesday, March 12, 2025
spot_img

DK..KIJAZI ABEBESHWA MZIGO WA LAWAMA

 

Ahmad El Maamry, mwanasheria wa Kampuni ya Hotel and Lodges

 

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

 

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Allan Kijazi sasa anaelekezewa mzigo wa lawama kwa kutochukua hatua stahiki ambazo zingewezesha hoteli zenye hadhi ya nyota nne zilizo chini ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kutoa huduma bora, kutopoteza mapato na kutoendeshwa na menejimenti ya kigeni.

 

Wadau wa sekta ya utalii walioongea na Tanzania PANORAMA Blog pamoja na mwanasheria wa Kampuni ya Hotel and Lodges, iliyokabidhiwa kuziendesha hoteli hizo lakini sasa inadaiwa kuziacha zikioza, Ahmed El Maamry, wameeleza kuwa Dk. Kijazi ndiye anayepaswa kubeba mzigo wa lawama kutokana na mwenendo mbaya wa uendeshaji wa hoteli hizo.

 

Katika mahojiano yaliyofanyika kwa nyakati tofauti na wadau hao, walisema tume uliyoundwa kufanya uchunguzi kuhusu matatizo yanayozikabili hoteli nne za Manyara, Lobo, Soronera na Ngorongoro iliundwa na TANAPA wakati Dk. Kijazi akiwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo na ilifanya kazi chini ya Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa TANAPA, Paul Banga.

 

Mmoja wa wadau wa utalii walioeleza hayo (jina kapuni) alisema hata baada ya tume kumaliza kazi ilikabidhi ripoti kwa Dk. Kijazi na uamuzi wa kuipata Kampuni ya Hotel and Lodges muda wa siku 90 na baadaye kuiongezea muda hadi kuwa mwaka mmoja kuzifanyia ukarabati kinyume na mapendekezo ya tume ulifanyika chini ya Dk. Kijazi.

 

“Yeye atoke aseme kuna nini ndani ya hili dude. Ina maana msingeandika hakuwa na mpango wa kusema? Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu tume hiyo ilipoundwa ikafanya kazi na kuwasilisha ripoti kwake..

 

“Ripoti hiyo aliipokea Dk. Kijazi, uamuzi wa kuwapa muda wa siku 90 tofauti na mependekezo ya tume ulichukuliwa chini yake, uamuzi wa kuwaongezea muda hadi kufukia mwaka mmoja ulichukuliwa chini yake. Hivi anajua kuwa mpaka sasa licha kuwapa hadi mwaka mmoja kutekeleza maagizo ya mamlaka za serikali hawajayatekeleza kikamilifu, sasa anapata wapi kigugumizi cha kusema?

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Allan Kijazi

 

 

“Hoja kwamba kuna majadiliano yanaendelea serikalini ni sawa tu lakini hebu tujiulize hayo majadiliano zaidi ya mwaka sasa tangu tume imalize kazi ni majadiliano gani, maana hata najadiliano ya mikataba mibovu ya madini hayakuchukua muda mrefu hivi na ndiyo yalikuwa magumu hadi wazungu wakubwa wakachukua ndege zao kuja nchini, TANAPA kuna nini?

 

“Dk. Kijazi kwa muda wote aliokaa TANAPA anajua kuwa hoteli hizo zinaendeshwa kutokea Kenya, anaijua vizuri sekta ya utalii na unajua ushindani uliopo kati ya Tanzania na Kenya kwenye sekta ya utalii, kwanini hakuchukua hatua kurekebisha matatizo yaliyopo? Zaidi ya hapo tume ilipendekeza menejimenti ya hoteli hizo ihamishiwe Arusha Tanzania badala ya Kenya ilipo sasa, hao wawekezaji wamegoma mpaka leo menejimenti ipo Kenya, nini kimemshinda kuchukua hatua siku zote hizo?

 

“La muhimu bhana usinitaje kabisa, maisha yangu nayapenda. Hii sekta ina mambo yake ukijifanya unajua sana kuongea hauchukui round. Hata wewe tunashangaa mpaka leo bado unaandika lakini si ajabu rungu likakuangukia wakati wowote. Ila ukweli ni kwamba sisi watanzania tunajimaliza wenyewe halafu tunaitisha vikao kujadili sababu wakati ni sisi wenyewe.

 

“Mwambieni Kijazi aseme ni kwanini Ngorongoro wamechukua hoteli yao kutoka kwa huyu mwekezaji, muulizeni aseme ni kwanini Zanzibar wamechukua hoteli zao, muulizeni aseme kulikoni TANAPA kuna kigugumizi wakati kila kitu kipo wazi na tume yao ilishatoa mapendekezo,” alisema.

 

Mdau mwingine aliyezungumzia hilo kwa sharti lile lile la jina lake kuhifadhiwa, naye alielekeza lawama kwa Dk. Kijazi kwa kukaa kimya huku akijua kuwa hoteli ni moja wapo ya miundombinu muhimu ya kuvutia wawekezaji.

 

Alisema ni jambo lisiloingia akilini kuwa Dk. Kijazi katika kipindi chote alichokuwa bosi wa TANAPA hakujua kuwa hoteli hizo zina matatizo hadi ilipokuja kugunduliwa na kiongozi mwingine. 

 

“Sisi hatukai, serikali ina taratibu zake na tunakubali inaendelea kulifanyia kazi kama alivyosema yeye Kijazi na wewe ukaandika, lakini katika akili ya kawaida hivi hili suala ni la kuchukua mwaka mmoja kweli maana ndani ya huo mwaka watalii wanakuja, wanaziona changamoto zilizopo kwenye hoteli zetu halafu sisi tunasema bado tunalifanyia kazi wakati majirani zetu hawajalala wanaendelea kujiimarisha na kuvuna pesa 

 

“Dk Kijazi amekaa TANAPA miaka mingi mno, kweli hakujua kuwa hoteli hizo zina matatizo hadi alipokuwa kugundua aliyekuwa mmoja wa mawaziri?. Wewe mwandishi hili linakuingia akilini.?

 

“Serikali inakosa mapato,  bidhaa za ndani zinakosa soko, wanafanyakazi wanaachishwa kazi kiholela tu, hoteli zinaoza tu, mali yako inaendeshwa na wageni tena kutokea nje kwenye taifa jingine ambalo ingawa ni jirani mwema lakini ni mshindani wako mkubwa mnayegombea ugali. Wewe upo hauoni tu. Haya nimesoma umeandika anasema hakuwa na madaraka aliyonayo, ni sawa, sasa una madaraka hayo na anajua kila kitu kwanini huchukui hatua?

 

“Yaania unaomba muda wakati wenzako wanachukua uamuzi mgumu, Ngorongoro na Zanzibar wamechukua uamuzi mgumu. Dk. Kijazi hapa anataka kusema nini hasa maana sisi tunayajua sana haya mambo. Hebu aje aseme tusikie na sisi tuseme uandike kama hivi kama utakuwa bado unaandika ili mbivu na mbichi zijulikane. Tunamsubiri kwa hamu tumsikie, na siyo hili tu hii sekta ya utalii ina mambo mengi mno, maliza hili tutakupa mambo mpaka ukimbie,” alisema.

 

Dk Kijazi amekwishatamka kuwa kuna majadiliano ya ndani ya serikali yanayoendelea kuhusu mkasa wa hoteli hizo na yatakapokamilika atatoa kauli yake na kujibu maswali yote yaliyojitokeza.

 

Kwa upande wake mwanasheria wa Kampuni ya Hotel and Lodges, Ahmed El Maamry alisema anashangazwa na uamuzi uliochukuliwa NCAA wa kuichukua Hoteli ya Ngorongoro kwa sababu ni mali halali ya mteja wake aliyoinunua zaidi ya miaka 20 iliyopita.

 

Katika mahojiano ya hivi karibuni, El Maamry alirekebisha kauli yake kwa kueleza kuwa yeye ni mwanasheria wa Kampuni ya Hotel and Lodges.

 

Alisema Hoteli za Ngorongoro, Manyara, Lobo na Soronera zilinunuliwa na kampuni hiyo wakati wa ubinafsishaji mashirika ya umma hivyo ni mali halali ya kampuni hiyo na ni makosa kuinyang’anya.

 

Alisema Kampuni ya Hotel and Lodges imewekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 20 kwenye hoteli hizo na inalipa kodi kubwa serikalini ila kinachoendelea sasa ni vita ya kibiashara baina ya Kampuni ya Hotel and Lodges na mfanyabiashara mwenye asili ya kiasia anayemiliki ukwasi wa kutisha anayezitaka hoteli hizo kwa udi na uvumba.

 

“Dk. Kijazi anapaswa kusema na atasema mimi naamini kwa sababu mzigo huu ni wa kwake. Anajua ukweli, anavyokaa kimya lawama zinazidi kuelekezwa kwake. Inashangaza mtu unanunua kitu halafu unanyang’anywa. Ngoja tusibiri kauli yake,” alisema El Maamry ambaye mahojiano yake kamili na Tanzania PANORAMA Blog yatachapishwa hivi karibuni.

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya