Tuesday, December 24, 2024
spot_img

HIFADHI YA NGORONGORO YAKABILIWA NA VITA YA BINADAMU NA WANYAMA

RIPOTA PANORAMA

MIGOGORO ya binadamu na wanyamapori katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, inayohusisha vifo vya binadamu na changamoto za usimamizi wa maji kwenye hifadhi na maeneo ya uhifadhi ni mambo yaliyofikia rekodi ambayo si nzuri katika kipindi cha mwaka 2021/2022.

Rekodi hizi ambazo si nzuri zimebainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Kwa mujibu wa CAG, migogoro ya binadamu na wanyamapori iliyohusisha vifo vya binadamu kwa mwaka 2020/2021 ilisababisha wanyamapori kuua watu 26 na kujeruhi 77 na kwa mwaka 2019/ 2020 ilisababisha vifo vya watu 20 na majeruhi 66.

“Mwaka 2021/22, nchi ilikumbwa na ukame wa muda mrefu na kusababisha uhaba wa maji kwa wanyamapori katika Hifadhi za Taifa na maeneo ya hifadhi. Katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, wanyamapori wapatao 135 walikufa kutokana na ukame na pia wengine kukimbilia katika makazi ya watu kutafuta maji na malisho.

“Vifo hivyo ni pamoja na nyati 40, nyumbu 30, pundamilia 60 na viboko watano. Aidha, migogoro ya binadamu na wanyamapori iliyohusisha vifo vya binadamu ilifikia rekodi ambayo siyo nzuri kwani miaka ya 2020 na 2021, wanyamapori waliua watu 26 na kujeruhi 77, wakati 2019/2020, watu 20 waliuawa na 66 kujeruhiwa hali iliyosababisha kulipiza kisasi huku wanyamapori nao kuuwawa; sababu ikiwa ni kugombania maji na malisho,” anaeleza CAG katika ripoti yake.

Aidha, CAG ameeleza kuwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori imeongezeka kutoka visa 31 vilivyoripotiwa mwaka 2020/2021 hadi visa 42 vilivyoripotiwa mwaka 2021/2022 na kwamba hifadhi na maeneo ya uhifadhi yalikabiliwa na changamoto za usimamizi wa maji kwa vile maji yanayotiririka ndani ya hifadhi yanatokea nje ya mipaka yake ambapo mamlaka haina mamlaka kuyasimamia.

“Kwa mfano, kiasi cha maji katika mito ya Katuma na Kapapa iliyopo Hifadhi ya Taifa ya Katavi, kina cha maji kilipungua kutokana na uvamizi wa wafugaji na wakulima kwenye vyanzo vya maji.

“Kwa maoni yangu mfumo wa ikolojia unaweza kuharibika kwa kiasi kikubwa, wanyamapori wanaweza kuangamia na pia migogoro kati ya wanyamapori na binadamu inaweza kuongezeka

hadi kufikia kiwango kisichoweza kudhibitiwa iwapo hatua stahiki hazitachukuliwa ili kuimarisha usimamizi wa maji katika Hifadhi za Taifa za Tanzania ikiwa ni pamoja na kujenga mabwawa ya kuvuna maji ya mvua,” ameeleza CAG.

Ameshauri mamlaka husika kwa kushirikiana na Serikali kusitisha shughuli zote za kibinadamu zinazozunguka hifadhi na kujenga mabwawa ya maji yatakayotumika unapotokea ukame wa muda mrefu na kuathiri upatikanaji wa maji.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya