RIPOTA PANORAMA.
HATIMAYE Wizara ya Afya, imetoa kauli ikifafanua taarifa iliyomo kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ongezeko la vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga kwa wastani wa kati ya vifo 102 hadi 989 kwa kila vizazi hai 1,000 katika halmashauri 20 hapa nchini.
Sambamba na hilo, pia imefafanua kuhusu uwiano wa vizazi hai na vifo kwa watoto wachanga kutotambuliwa katika halmashauri 20 hapa nchini kutokana na kutopatikana kwa takwimu za uzazi.
Ufafanuzi huo umetolewa leo na Msemaji wa Wizara ya Afya, Englibert Kayombo alipokuwa akijibu kwa niaba ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuhusu kuwepo kwa ongezeko la juu la vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga katika halmashauri 20 nchini.
Akijibu kuhusu ongezeko hilo kinyume na shabaha iliyowekwa na Serikali, Kayombo ameeleza kuwa takwimu za hali ya afya na watu nchini hutolewa kila baada ya miaka mitano.
Amesema takwimu hizo zinaonyesha kuwa mwaka 2005 kulitokea vifo vitokanavyo na uzazi 578 kwa kila vizazi hai 100,000, mwaka 2010 vilitokea vifo 454 kwa kila vizazi hai 100,000 na mwaka 2015 kulitokea vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000
Kayombo amesema takwimu mpya za Shirika la Afya Duniani (WHO), ambazo hulinganisha nchi zote duniani za mwaka 2023 zinaashiria hali ya vifo vitokanavyo na uzazi hapa nchini kuwa ni 238 kwa kila vizazi hai 100,000.
Akijibu kuhusu Wizara ya Afya inavyokabiliana na ongezeko la vifo vya akinamama wajawazito, Kayombo ameeleza kuwa Tanzania imeendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma kwa kutengeneza miundombinu ya utoaji huduma kwa kujenga zahanati 100, vituo vya afya 500 na hospitali za wilaya 102 zimekarabatiwa ili kuziwezesha kutoa huduma bora za afya ya uzazi, mama na mtoto.
“Uwekezaji huu umeongezea vituo vya afya uwezo wa kufanya upasuaji mkubwa wa kumtoa mtoto tumboni karibu na wananchi. Hii yote imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya ngazi ya msingi, hususan huduma za uzazi na watoto wachanga. Aidha Serikali inaendelea kuajiri watumishi wenye ujuzi na kununua vifaatiba katika vituo ngazi zote vya kutolea huduma,” ameeleza Kayombo.
Kuhusu hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Afya kukabiliana na ongezeko la vifo vya watoto wachanga amesema hali ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano imeendelea kushuka kwa asilimia 35 kutoka vifo 67 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2015 hadi vifo 43 kwa kila viazi hai 1,000 mwaka 2022.
“Hata hivyo, vifo vya watoto wachanga vimeonekana kupungua kwa kasi ndogo ambako kunatokana na kiwango kidogo cha upatikanaji huduma za watoto. Hili limeisukuma nchi yetu kuamua kuwekeza kwenye huduma za watoto wachanga kwa kuanzisha wodi maalumu kwa ajili ya huduma za matibabu ya watoto wachanga (NCU) kutoka hospitali 14 mwaka 2018 hadi hospitali 175 mwaka 2023 na kuanzisha vyumba vya mama kangaroo (KMC) katika kila kituo cha afya.
“Kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba kwa ajili ya huduma za watoto wachanga wagonjwa na njiti ambako katika bajeti ya 2022/2023, Serikali imenunua vifaatiba kwa kutumia fedha za ahueni ya UVIKO 19 vyenye thamani ya Shilingi bilioni 6.3 kuptia Bohari Kuu ya Dawa ambavyo vitasambazwa kwenye hospitali mbalimbali nchini.
“Aidha, Wizara ya Afya imeendelea kuwajengea uwezo watoa huduma katika ngazi mbalimbali za namna ya kuwahudumia watoto wachanga, ikiwemo mafunzo elekezi kazini kwa kutumia watalaamu mbalimbali ikiwemo madaktari bingwa na wabobezi kwa kushirikiana vyama vya kitaaluma vilivyopo nchini,” ameeleza Kayombo.
Akijibu swali lililouliza vifo vingi vya watoto wachanga vinasababishwa na nini? Amesema asilimia 80 ya vifo vya watoto wachanga husababishwa na shida kuu tatu alizozitaja kuwa ni kuzaliwa njiti, kushindwa kupumua kunakotokana na changamoto za uzazi na maambukizi ya bakteria.
Kayombo pia amejibu kuhusu kutopatikana takwimu za uzazi na utaratibu unaotumiwa na hospitali za hapa nchini kutunza kumbukumbu za vizazi hai na vifo kwa kueleza kuwa miaka 2000 kushuka chini hakukuwa na mfumo imara wa ukusanyaji wa takwimu ila kwa sasa kuna mfumo wa taarifa za uendeshaji huduma za afya (MTUHA).
“Mfumo huu wa ukusanyaji takwimu za afya unaanzia katika ngazi ya jamii, zahanati, vituo vya afya na hospitali umewezesha upatikanaji wa takwimu kutoka nchi nzima. Kupitia mfumo huu tumeweza kufuatilia takwimu za uzazi wa mpango, huduma wakati wa ujauzito, uchungu na kujifungua na baada ya kujifungua. Aidha, baadhi ya vituo vya huduma kama hospitali za Taifa, kanda, mkoa na baadhi za wilaya zimeanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa utoaji huduma na ufuatiliaji takwimu umezidi kuimarisha utendaji wa mfumo wa MTUHA,” ameeleza Kayombo.
Katika maswali ambayo Tanzania PANORAMA Blog ilimuuliza Waziri Ummy Mwalimu ni mtizamo wake kuhusu utaratibu unaotumika sasa kutunza kumbukumbu za vizazi hai na vifo kwenye hospitali zetu kama unafaa au haufai na Kayombo; alijibu kwa niaba ya Waziri Ummy kuwa takwimu za vifo vitokanavyo uzazi na watoto ndiyo takwimu pekee zenye uhakika.
Amesema takwimu hizi zimewezesha sekta ya afya kufanya tathmini ya kujua changamoto za mifumo ya afya zinazosababisha vifo vitokanavyo na uzazi wa watoto na kwamba takwimu hizo ni bora kwani zinaonyesha visababishi na zimewezesha kufanya mapitio.
Kayombo amezungumzia pia changamoto ambazo Wizara ya Afya imezibaini katika utaratibu unaotumika sasa kutunza kumbukumbu za vizazi hai na vifo kwa kueleza kuwa ukusanyaji wa takwimu unaotegemea rejista za karatasi baadaye kwenye mfumo wa kielektroniki huchelewa kutoa taarifa na wakati mwingine husababisha kupotea au kuharibika kwa takwimu wakati ikifanyiwa kazi ngazi mbalimbali.
Kwa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuwa na viwango vya juu vya vifo vya watoto wachanga, Kayombo amesmema hizo ni takwimu za kutolea huduma ndani ya vituo.
“Ni vema kusubiri taarifa ambazo takwimu hizi zinatolewa kutoka National Bureua of Statistics ambazo huangalia mpaka kwenye jamii. Aidhaa kama survey zinaonyesha hali ya vifo vya watoto ni 20-24 kwa kila vizazi hai 1,000 basi takwimu hizi zipo kwenye upande wa juu sana kuaminika,” amesema.