Tuesday, December 24, 2024
spot_img

CAG – MITA 1,638 ZA TANESCO HAZIPO KWENYE MFUMO, 874,019 HAZIJATHIBITISHWA

RIPOTA PANORAMA

MITA 1,638 kati ya 1,803 za Shirika la Umeme (Tanesco) zilizopo kwenye vituo vya umeme katika mikoa 29 hapa nchini hazionyeshwi kwenye mfumo wa usomaji mita moja kwa moja kwa muda wa mwaka mzima.

Sambamba na hilo, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 Tanesco ilinunua na kutumia mita 875,019 zenye thamani ya Shilingi bilioni 115 ambazo hazikuthibitishwa na wakala wa vipimo.

Haya yamefichuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

CAG anaeleza katika ripoti yake kuwa licha ya mita 1,638 ambazo ni asilimia 90.9 ya mita 1,803 kutosomwa kwenye mfumo moja kwa moja, mita nyingine 52 zinasoma nishati ya umeme iliyopokelewa tu huku mita nyingine 90 zikisoma nishati ya umeme iliyosafirishwa tu.

Kwa mujibu wa CAG, mwenendo huu wa Tanesco inakiuka kanuni nambari 45 (1) ya kanuni za sheria ya umeme (huduma za ugavi) za mwaka 2019.

CAG anaeleza kwenye ripoti yake kuwa katika ukaguzi wake alibaini kuwepo ugumu wa kufuatilia usomaji wa mita kwa mitambo ya kulisha umeme na usambazaji umeme ikiwa ni pamoja na kwa watumiaji wakubwa wa nishati hiyo kutokana na upungufu wa maelezo kuhusu mitambo ya kulisha umeme au vituo vidogo vya umeme katika mfumo wa usomaji mita moja kwa moja.

Ripoti yake CAG inaukariri uongozi wa Tanesco ukieleza sababu za kuwepo udhaifu huo ni matatizo ya mtandao wa mita zilizoharibika kwenye vituo vya umeme; hata hivyo yeye anaeleza kuwa ufungaji wa mita za Tanesco haukuakisi thamani ya fedha.

“Kwa maoni yangu, ufungaji wa mita katika mitambo ya umeme haukuakisi thamani ya fedha na kuna uwezekano kuwa baadhi ya mita au mitambo ya umeme imefanyiwa udanganyifu au kughushiwa, hivyo kusababisha wizi wa nishati unaofanywa na wateja (hasa watumiaji wakubwa wa nishati) kwa kushirikiana na wafanyakazi wasio waaminifu,” inasomeka ripoti ya CAG.

Wakati huo huo, CAG anaeleza kuwa manunuzi ya mita 874,019 zenye thamani ya Shilingi bilioni 115 yaliyofanywa na Tanesco pasipo kuthibitishwa na wakala wa vipimo yanaweza kulisababishia shirika hilo na wateja wake hasara.

CAG anakielezea kitendo hicho cha Tanesco kuwa ni ukiukwaji wa kanuni ya 22 (1) ya kanuni za uzani wa vipimo za mwaka 2019 zinazokataza matumizi ya mita kwa mkandarasi au mnunuzi kwa madhumuni ya kupima umeme au gesi.

“Hii ni kinyume na kanuni ya 22 (1) ya kanuni za uzani na vipimo za mwaka 2019 zinazoelekeza kuwa hakuna mita itakayoruhusiwa kutumiwa na mkandarasi au mnunuzi kwa madhumuni ya kupima umeme au gesi inayotolewa au kutumika kwake, isipokuwa imethibitishwa kwa mujibu wa sheria za umeme Na.10 ya 2008 (Sura.131),” inasomeka ripoti ya CAG.

Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta bila mafanikio Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Maharage Chande kuzungumzia pamoja na mambo mengine ukiukwaji wa kanuni unaofanywa na shirika lake pamoja na mita za Tanesco kutosomwa moja kwa moja kwenye mfumo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya