Thursday, July 17, 2025
spot_img

HOSPITALI MLOGANZILA VULULUVULULU, MUHIMBILI NAKO MAMBO MABAYA

RIPOTA PANORAMA

HALI ni mbaya katika Hospitali ya Mloganzila. Mwenendo wa utendaji kazi siyo wa kuridhisha na katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili nako hakuna usimamizi mzuri wa matengenezo ya vifaa tiba.

Mwenendo huu mbaya wa mambo kwenye taasisi hizi umebainishwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya mwaka 2021/2022 ambayo hivi karibuni iliwasilishwa bungeni na kuibua mjadala mkubwa miongoni mwa wabunge baada ya kubainika; pamoja na mambo mengine, ufujaji mkubwa wa fedha za umma.       

CAG katika tathmini aliyoitoa kwenye ripoti yake hiyo kuhusu utendaji kazi wa Hospitali ya Mloganzila, ameeleza kuwa gharama za uendeshaji ni kubwa kuliko mapato, ikiwa kati ya asilimia saba mpaka 19, kutoka mwaka 2018/2019 hadi 2021/2022.

Kwamba katika Hospitali ya Mloganzila, nakisi kwa mwaka iliongezeka kutoka Shilingi bilioni 1.92, mwaka 2018/2019 hadi kufikia Shilingi bilioni 5.81 mwaka 2021/22 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 394 katika kipindi hicho.

Mbali ya hayo, ripoti ya CAG imeeleza zaidi kuwa Hospitali ya Mloganzila inapoteza mapato mengi kutokana na kuongezeka kwa misamaha ya kupatiwa huduma za matibabu ambayo wakati mwingine haidhibitiwi vizuri na pia kuongezeka kwa madai yanayokataliwa kulipwa na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa huduma za matibabu inazotoa kwa wanachama wa mfuko huo.

CAG pia ameeleza kubaini Hospitali ya Mloganzila inatoa huduma duni za kibingwa kwa wagonjwa na pia ina usimamizi mbaya wa matengenezo ya vifaa tiba.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tathmini ya CAG kuhusu mpango wa kina wa matengenezo ya vifaa kutoka idara ya usimamizi wa vifaa tiba kwa mwaka 2021/2022, ilibaini kuwa kati ya vifaa tiba 192 vilivyopangwa kufanyiwa matengenezo, ni sita pekee vilivyofanyiwa matengenezo. Hiyo ni sawa na asilimia tatu ya vifaa vilivyopangwa kufanyiwa matengenezo.

Aidha, ripoti imeeleza zaidi kuwa Hospitali ya Mloganzila imekuwa ikifanya matengenezo ya vifaa tiba baada ya tatizo kutokea badala ya kuvifanyia matengenezo kwa muda uliopangwa kabla tatizo halijajitokeza ili kuzuia kukatisha utoaji wa huduma.

Kwa upande mwingine katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, ripoti CAG imeeleza kuwepo kwa tatizo la kuvifanyia matengenezo vifaa tiba na kutowiana kwa mpango wa matengenezo kulingana na ratiba ya matengenezo iliyowekwa kwa vifaa hivyo.

“Katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili, nilibaini kuwa mwaka 2021/22, kati ya vifaa vya matibabu 60 vilivyopangwa kwa ajili ya matengenezo, ni vifaa 27 (asilimia 45) tu vilifanyiwa kazi.

“Zaidi ya hayo, nilibaini kuwa mpango wa matengenezo (kwa baadhi ya mali) ambao taasisi imeanzisha hauwiani na ratiba ya matengenezo iliyoelezwa na mwongozo wa mashine.

“Iwapo vifaa tiba havitakaguliwa na kufanyiwa matengenezo kwa mujibu wa mpango, gharama ya juu ya ukarabati wa dharura wa vifaa inaweza kutokea na kuahirishwa mara kwa mara kwa huduma.

“Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2021/2022, mashine ya uchunguzi wa kina wa mwili (MRI) ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili iliharibika na iligharimu Shilingi milioni 20 kwenye matengenezo. Iwapo vifaa havitakaguliwa kwa mujibu wa mpango, ubora wa huduma utaathirika,” inasomeka ripoti ya CAG.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya