RIPOTA PANORAMA
RIPOTI ya ukaguzi wa ufisadi ulioibuliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Halmashauri ya Jiji la Arusha imekabidhiwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Hilo limebainishwa kwenye ripoti ya ukaguzi ya CAG ya mwaka 2021/2022 ambayo pamoja na mambo mengine mengi, inaeleza kuwa Waziri Mkuu Majaliwa alimuomba CAG kufanya ukaguzi katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhusu mambo mbalimbali ya uendeshaji wa halmashauri hiyo.
Ripoti ya CAG imeyataja maeneo iliyoyafanyia ukaguzi kuwa ni usimamizi na utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo, ufuataji wa sheria na kanuni za manunuzi, mapato, miamala ya fedha taslimu na maandalizi ya bajeti.
Ameyataja maeneo mengine aliyoyafanyia ukaguzi kuwa ni ukusanyaji wa kodi, mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kuhakiki madeni ya wakandarasi, uhamisho wa wafanyakazi na uendeshaji wa Kampuni ya Arusha Meat.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Hargeney Reginald Chitukuro ambaye ametafutwa na Tanzania PANORAMA Blog kwa ajili ya kufanya mahojiano naye kuhusu mambo kadhaa anayoelekezewa sambamba na kujua mwenendo wa mambo kwa sasa katika halmashauri hiyo, hata hivyo hakuwa tayari kutoa ushirikiano.
Kwa mujibu wa CAG, mbali na kuiwasilisha ripoti yake TAKUKURU, pia ameiwasilisha kwenye taasisi nyingine zinazohusika kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi.
Waziri Mkuu Majaliwa aliwasimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk. John Pima, aliyekuwa Mweka Hazina, Mariamu Shabani, Mchumi wa Jiji, Innocenti Maduhu pamoja na watumishi wengine watatu kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikiwaandamana.
Alipokuwa akichukua hatua hiyo, alisema iwapo uchunguzi dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za Halmashauri ya Jiji la Arusha utawaweka salama, watarejea kwenye utumishi wao lakini ikiwa vinginevyo basi wataendelea na kukabiliana na tuhuma zao.