Saturday, July 19, 2025
spot_img

KSIJ TANGA KUFUTIWA USAJILI ENDAPO…

RIPOTA PANORAMA

WIZARA ya Mambo ya Ndani, itafuta usajili wa jumuiya ya kidini ya Khoja Shia Isnaasheri Jamaat (KSIJ) iliyopo Mkoa wa Tanga iwapo uchunguzi unaofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwa viongozi wake, zitathibitika pasipo shaka.

Hayo yameelezwa jana na Afisa Habari wa Mkoa wa Tanga, Jamal Zuberi alipozungumza na Tanzania PANORAMA Blog kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba kuhusu hatua zinazochukuliwa na ofisi yake kushughulikia tuhuma na malalamiko ya wanajumuiya hiyo dhidi ya mwenyekiti wao.

Mwenyekiti wa KSIJ Tanga, Hussein Walji anadaiwa kuchukua wadhfa huo pasipo kuchaguliwa na wanajumuiya na kwamba anaiongoza pasipo kuwa na msaidizi yoyote huku akidhulumu fedha za misaada, kutumia fedha za jumuiya kinyume cha taratibu na kukiuka sheria za nchi zinazoelekeza jinsi ya uendeshaji jumuiya za aina hiyo.

Akitoa kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Zuberi alisema Wizara ya Mambo ya Ndani imeishaanza kutekeleza majukumu yake kwa kufuatilia tuhuma zilizopo na endepo itabainika ni kweli na hatia kupatikana itaifuta KSIJ Tanga na wahusika wa vitendo vinavyolalamikiwa watawajibishwa.

“Msajili wa taasisi hiyo (Wizara ya Mambo ya Ndani) ameishaanza kutekeleza majukumu yake kwa kufuatilia tuhuma zilizopo juu ya taasisi hiyo na endepo itabainika ni kweli na hatia kupatikana, ameeleza kuwa itaifutia usajili taasisi hiyo na kuwawajibisha wote waliohusika na vitendo hivyo.

“Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga siyo msemaji wa taasisi hiyo,.. anayepaswa kujibu tuhuma hizo ni taasisi husika. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itafuatilia taarifa zote kuhusu tuhuma hizo na ukweli utakaobainika utawekwa wazi kwa umma pamoja na hatua zitakazochukuliwa,” alisema Zuberi.

Kwa mara ya kwanza, Tanzania PANORAMA iliripoti kuwepo kwa mgogoro ndani ya KSIJ Tanga mapema Februari, mwaka huu, ambapo ilidaiwa kuwepo kwa uongozi wa kiimla, Mwenyekiti Walji kudhulumu fedha za misaada, ufisadi wa mali za jumuiya hiyo pamoja na kutowasilisha serikalini taarifa ya kila robo mwaka ya jumuiya kama inayoelekezwa na sheria za nchi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wanajumuiya hiyo na nyaraka ambazo Tanzania PANORAMA imeziona, wanajumuiya zaidi ya 40 wa KSIJ Tanga walitia saini waraka wa kutokuwa na imani na Mwenyekiti Walji (pichani juu) wakimtuhumu kuiendesha kiimla, kudhulumu fedha za misaada za watu masikini wakiwemo vijana na walemavu ambao wanasaidiwa kujikimu kimaisha na jumuiya hiyo.

Inadaiwa, Walji huwa anawapatia kiasi kidogo cha fedha za misaada wanazopaswa kupewa huku akiwalazimisha kusaini nyaraka zinazoonyesha wamepokea kiasi kikubwa cha fedha pamoja na kukiuka taratibu za uchukuaji fedha za jumuiya zilizohifadhiwa benki.

Tuhuma nyingine anazoelekezewa Walji ni kutumia uwezo wake wa kifedha akisaidiwa na washirika wake, kuwashughulikia wanaomkosoa ikiwemo kuwafungulia kesi za uongo polisi na kuwatisha kwa kutumia majina ya viongozi.

Katikati ya tuhuma hizo, baadhi wa wanajumuiya waliibua hoja ya uadilifu kwa Walji kuwa hafai kuwa kiongozi wa jumuiya hiyo, kwa kurejea mashtaka yaliyopata kumkabili mahakamani kabla ya kukutwa na hatia ya wizi wa friza kwenye kesi ya jinai namba 272 ya mwaka 2019 iliyosikilizwa Mahakama ya Mwanzo Tanga Mjini na kuhukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita.

Walji alishtakiwa mahakamani kwa kukutwa na friza alilodaiwa kuliiba katika duka la mfanyabiashara mwenzake na katika hukumu yake, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Tanga Mjini, S. B. Odeyo alisema utetezi wake mahakamani hapo haukuwa wa kweli bali wa kughushi na kwamba kitendo chake cha kughushi  nyaraka alizowasilisha mahakamani kinaweza kumfanya ashtakiwe kwa kosa la kughushi.

Walji mwenyewe katika mahojiano aliyopata kufanya na Tanzania PANORAMA alishindwa kukanusha wale kukubali tuhuma dhidi yake na badala yake alisema hayo atayazungumzia atakapokuwa ameketi kitako ofisini kwake na Tanzania PANORAMA.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga (RPC) Kamishna Msaidizi (ACP) Henry Mwaibambe, (pichani hapo juu) awali alipozungumzia mgogoro huo alikana kuujua na kueleza kuwa hata yeye taarifa za kuwepo kwake alizisikia kwenye mitandao.

“Hata mimi nimesoma tu kwenye mtandao kuhusu hizo taarifa lakini mimi binafsi sijapata taarifa hizo. Hapa ndiyo ninataka nifuatilie, labda niulize kama walileta malalamiko lakini mimi binafsi sijalipata hilo. Unajua RPC ni ofisi labda kuna taarifa zilifika mimi nikiwa sijafika. Ngoja nifike hapo maana saa hizi ndiyo natoka kwenye msiba kwa hiyo kwa sasa siwezi kusema chochote kwa sababu sijajua lakini tumepokea hizo taarifa, tunazifuatilia, tunachunguza kujua ukweli, kiini cha mgogoro ni kitu gani. Nipe muda kidogo niongee na OCD,” alisema RPC Mwaibambe.

Wakati RPC Mwaibambe akisema hayo, Tanzania PANORAMA ilikuwa na taarifa za uhakika kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga lilifanya uchunguzi kuhusu mgogoro huo baada ya Mwenyekiti Walji kuwashtaki polisi baadhi ya wanajumuiya waliokuwa wakitaka aachie ngazi na lilibaini mambo kadhaa yakiwemo mambo mazito kabla ya kuliweka kapuni faili hilo kwa kile kilichodaiwa ni maagizo kutoka juu.

Siku chache baadaye RPC Mwaibambe aliliambia Tanzania PANORAMA kuwa faili la kesi hiyo halijafika ofisini kwake hivyo amemuagiza Kamanda wa Makosa wa Jinai wa Mkoa wa Tanga (RCO) kulisaka na kulifanyia kazi kikamilifu.

Wakati Kamanda Mwaibambe akisema hayo, taarifa ilizopata Tanzania PANORAMA kutoka ndani ya ofisi yake zilieleza kuwa aliliitisha faili hilo akapelekewa mkononi na baada ya kulisoma aliita baadhi ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Tanga kuzungumza nao kuhusu suala la mgogoro wa KSIJ Tanga lakini Tanzania PANORAMA Blog ambayo ilikuwa ikiripoti suala hilo, hakuiita.

Tangu wakati huo, Tanzania PANORAMA imefanya jitihada kubwa za kumpata Kamanda Mwaibambe kuzungumzia suala hilo pasipo mafanikio na badala yake imekuwa ikikutana na misukosuko ya hapa na pale.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga hadi sasa halisema uchunguzi wa tuhuma hizo ulibaini nini.

Aidha, inadaiwa Septemba 12, 2022 Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Emmanuel Kihampa aliuandikia barua uongozi wa KSIJ Tanga akiutaka kufika ofisini kwake kuzungumzia malalamiko ya wazee, wajane na watu wenye ulemavu wanaosaidiwa na taasisi hiyo lakini agizo lake hilo lilitupwa kapuni na Walji.

Kihampa alipozungumza na Tanzania PANORAMA kuhusiana na hilo alisema mambo ya jumuiya za kidini hawezi kuyazungumzia kwenye vyombo vya habari kwa sababu ya kulinda hadhi na heshima za jumuiya za aina hiyo.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Tanga, Omary Mgumba (pichani juu) wakati akizungumzia sakata hilo, pamoja na mambo mengine alisema atauita uongozi wa jumuiya hiyo ofisini kwake kuzungumzia tuhuma dhidi ya Mwenyekiti Walji za kufuja fedha za umma zilizochangwa kusaidia makundi ya wazee, wajane na wasiojiweza.

“La kwanza kwa sababu kuna tuhuma hapo za kufujwa kwa fedha za umma zilizochangwa kusaidia makundi hayo, sisi kama Serikali nafikiri hiyo ni NGO’s, shirika lisilokuwa la kiserikali na kwa kuwa ndiyo unanipa taarifa, nilikuwa sina taarifa kuhusu hilo suala, naomba nilifanyie kazi.

“Sisi kama Serikali na kwa sababu kuna jinai na wana utaratibu wa kuleta taarifa zao na hizo bado ni tuhuma hazijathibitishwa, basi ngoja tupate taarifa ya kwao hiyo taasisi kwa mujibu wa sheria kwa sababu wanatakiwa walete taarifa kila robo mwaka na Katibu Tawala wa Mkoa ndiyo mratibu wa mambo hayo basi nitaomba taarifa hiyo waniletee,” alisema Mgumba.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya