RIPOTA MAALUMU
IMEELEZWA kuwa wachungaji wa madhehebu ya dini wana nguvu ya ushawishi dhidi ya wafuasi wao kwa sababu huwa wanajifunza mbinu za kutumia kuwakusanya katika makanisa yao.
Kwamba wachungaji wana mvuto ambao mara nyingi huupata kutokana na uzoefu walionao unaotokana na kujifunza jinsi ya kuwashawishi watu kuwa wafuasi wao.
Wanasaikolojia Dk. Alexandre Stein wa Uingereza na Richard Turner ambaye ni mshauri katika Jumuiya ya Kisaikolojia ya Marekani (APA), katika mahojiano waliyoyafanya na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuhusu vifo vya watu zaidi ya 100 waliofunga kula na kunywa hadi walipokufa kwa kile kinachodaiwa walishawishiwa na mchungaji wao, Paul Mackenzie kuwa wakifa wanakwenda kuonana na Mungu, walieleza kuwa wachungaji wa madhehebu ya dini wana akili nyingi na hutumia matatizo ya watu kuwashawishi kujiunga nao.
Katika mahojiano hayo, mwanasaikolojia Dk, Stein aliyebobea katika itikadi kali na mahusiano mengine hatari katika jamii, alisema wachungaji siyo wajinga bali wana akili nyingi na ni watu wenye nguvu na hilo linathibitishwa na jinsi wanavyoweza kuyaongoza madhehebu wanayoyaanzisha kwani siyo rahisi kuongoza dhehebu la dini.
Alisema wachungaji huwa wanajifunza hila ambazo huzitumia kukusanya wafuasi huku wakiamini kuwa wanaweza kufanya mambo yao peke yao.
Dk. Stein aliendelea kueleza kuwa wachungaji wa madhehebu mengi ya dini ni wanaume tofauti na wanawake ambao idadi yao ni ndogo na katika moja ya mikasa ya kusitikisha iliyopata kufanywa na mchungaji mwanamke, Raia wa Brazil aliyemtaja kwa jina la Valentina de Andrade ulihusu tuhuma za mauaji.
Akisimulia mkasa huo, Dk. Stein alisema, Andrade ambaye mbali na uchungaji alikuwa mwanasiasa aliongoza kikundi cha Superior Universal Lineage ambacho miaka ya mwanzoni mwa 1990 kilidaiwa kusababisha mfululizo wa mauaji ya watoto, tuhuma ambazo zilibebwa na wanausalama wa Brazil kuzichunguza lakini baadaye waliishia kukiacha huru kikundi hicho.
Akizungumza kuhusu watu wanaojiunga na madhehebu ya dini kushindwa kujitoa kwa urahisi, Dk. Stein alisema ni rahisi sana kwa mtu kujiunga na madhehebu hayo kwa sababu viongozi wake wana uwezo mkubwa wa kulipua mabomu lakini ni vigumu kuachana nayo kwa sababu ya kutekwa akili.
Akirejea uzoefu alioupata mwaka 2013 alipovutiwa na kile alichotaja kuwa ni dhehebu la kikristu la Hisper alipokuwa akitafuta kazi ya kuwahudumia waathirika wa biashara haramu ya binadamu, alisema haijalishi mtu ni tajiri kiasi gani, amefanikiwa kiasi gani au ana akili kiasi gani. Kila mtu hukutana na hali ya kuyumba katika safari ya maisha yake.
Alizitaja hali za kuyumba kwa mtu ambazo humuweka katika wakati mgumu kuwa ni pamoja na kupoteza kazi, kufiwa au mabadiliko mengine ya kutatanisha katika maisha.
Alisema; “Kisha mtu akiwa katika hali hizo ngumu wanatumia hali hiyo alinayo ya kutojielewa kujenga mazingira yasiyofaa na kumpa dawa za kulevya. Dhehebu lenye imani potofu siku zote hujaribu kukutenga na marafiki na wapendwa wako ili iwe rahisi kukutumia vibaya,” alisema.
Akizungumzia jinsi mtu anavyoweza kujua kama shirika ni dhehebu, alisema siyo rahisi kwa watu kutambua kwamba shirika ni ibada lakini inaweza kuwa rahisi kwa kuperuzi kwenye mtandao wake ambao unaweza kutoa vidokezo.
Alisema ni vizuri kuangalia mtandaoni watu wanazungumza nini kuhusu kundi fulani na pia kuwa mwangalifu iwapo kikundi ulichojiunga nacho kitaanza kusema mambo mabaya kuhusu marafiki na jamaa zako na kujaribu kukufanya ujitolee zaidi katika shughuli za kikundi hicho ikiwa ni pamoja na kujitolea kwenye shughuli ambazo mtu anapaswa kulipwa.
Alisema Serikali za nchi zinapaswa kudhibiti madhehebu yenye utata ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha watu kuhusu makundi yenye utata badala ya kukaa kimya zikihofia kudhibiti madhehebu au makundi hayo hasa yanayojionyesha kama makanisa.
DHEHEBU NI NINI
Kwa mujibu wa Jumuiya ya Kisaikolojia ya Marekani (APA) inalielezea dhehebu kuwa kundi la kidini lenye sifa ya imani isiyokuwa ya kawaida au ya kutatanisha, iliyotengwa na ulimwengu wa nje na yenye muundo wa kimabavu.
Mwanasaikolojia Turner wa APA yeye alieleza kuwa ingawa ibada nyingi zinazofanywa na madhehebu ni za dini, zinaweza pia kujihusisha na masuala mengine kama siasa.
Kwa mujibu wa Turner, sehemu yako ya kazi inaweza kuwa kama dhehebu iwapo unashurutishwa kufanya mambo kama vile kufanya kazi mara kwa mara kwa muda mrefu na aliongeza kuwa baadhi ya vikundi vya masoko vya ngazi mbalimbali vinaendekeza mbinu za kuajiri zinazofanana na madhehebu.