Monday, July 21, 2025
spot_img

SIMAMIENI AJENDA ZA KITAIFA – MAJALIWA

*Awataka Ma-DC wafuate maono ya Rais Samia Suluhu Hassan

RIPOTA WA WAZIRI MKUU              

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa wilaya kusimamia ajenda za kitaifa ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa.

Amewataka pia kusimamia changamoto za upatikanaji wa ajira, kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kusimamia uoto wa asili na kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji.

Majaliwa amewataka vionozi hao kusimamia miradi ya maendeleo,ukusanyaji wa mapato ya Serikali na utatuzi wa kero za wananchi.

Maagizo hayo aliyatoa Jumamosi, Machi 18, mwaka huu alipokuwa akifungua mafunzo ya uongozi kwa wakuu wa wilaya 138 yaliyofanyika kwenye ukumbi wa St. Gasper, jijini Dodoma.

“Katika kukabiliana na tatizo la rushwa, nendeni mkakemee na kufuatilia mianya ya rushwa ili izibwe na kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu bila kulazimishwa kutoa rushwa,” alisema Majaliwa.

Akiwakumbusha wajibu wao, Majaliwa aliwataka wakuu hao wa wilaya wafuate maagizo na maelekezo ya mamlaka iliyowateua na aliwataka watambue kuwa wao ni wawakilishi wa Rais kwenye maeneo yao.

“Aina ya utumishi huu wa uteuzi ni tofauti na ule wa mchakato wa interview. Kwa hiyo mnapaswa kutambua mwenye mamlaka anataka nini, mnapaswa kuenenda na maono yake, matakwa yake na maelekezo yake.

“Ili mradi umeteuliwa na umeapa, wewe ni kiongozi wa Serikali wa eneo ulilopewa na ni msimamizi wa shughuli zote za Serikali na hata za sekta binafsi. Kwa hiyo unalo jukumu la kufuatilia na kujiridhisha yanayofanywa na sekta binafsi iwapo yanalenga kuleta maendeleo?” alisisitiza.

Akielezea umuhimu wa majukumu yao, Waziri Mkuu amesema: “Tunapozungumzia maendeleo ya nchi, hatuwezi kuyafikia bila uwepo wenu kwa sababu ninyi ndiyo wenye watu. Kuna wilaya ina halmshauri moja nyingine mbili au tatu. Ni lazima ufuatilie yanayoendelea katika wilaya yako na matarajio ya Mheshimiwa Rais ni kuona kuwa mtawahudumia wananchi, mtawatumikia na kusikiliza kero zao,” alisema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wakuu hao wa wilaya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki alisema mafunzo hayo ya siku sita yaliyoanza Machi 13, mwaka huu yalihusisha washiriki 139 ambapo kati yao 37 ni wapya na wengine 102 ni wale wanaoendelea na nyadhifa zao.

Akitoa rai kwa washiriki hao, Waziri Kairuki alisema: “Baada ya kupata mafunzo haya, tunataraji mkirudi kwenye vituo vyenu vya kazi, mtatekeleza yale yote mliyoyapata kwa kushirikiana na wengine ili kuharakisha utekelezaji wa shughuli za Serikali,” alisema Kairuki.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na Taasisi ya Uongozi na yalihusisha mada 17 zilizogusa masuala mbalimbali ambapo baadhi ya mawaziri walishiriki kutoa mada.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya