RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
MFANYABIASHARA Hiten Parik, ameibuka na kuzungumzia tuhuma anazoelekezewa.
Parik alifanya mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog mwishoni mwa wiki iliyopita mkoani Dar es Salaam na kukiri kuwa ni kweli anadaiwa mamilionu ya fedha na wakuliwa kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania ambako amekuwa akifika kukusanya mazao au kuwatumia mawakala.
Aidha, alikiri kudaiwa fedha nyingi na baadhi ya wafanyabiasha waliomkopesha na wale waliompatia fedha kwa ajili ya kununulia mazao.
Alizitaja sababu za kudaiwa mamilioni ya fedha na wakulima wengi kuwa ni kuanguka kwa bei ya mazao katika soko la India ambako huyapeleka na pia kuchelewa kufika kwa shehena ya mazao hayo.
Parik alisema, alianza kuingia kwenye mgogoro wa kibiashara mwaka jana baada ya meli iliyokuwa imebaba shehena ya mazao aliyokuwa akiyasafirisha kwenda India kushindwa kufika kwa wakati.
Alisema kuchelewa kwa meli hiyo kulisababisha mazao aliyokuwa akiyasafirisha kufika India huku bei ikiwa imeshuka hivyo kuuzwa kwa hasara.
Parik alisema mbali na kuingia hasara hiyo, wasafirisha huwa hawalipi fidia kwa hasara wanayomsababishai mfanyabishara hata kama makosa yanakuwa upande wao ikiwa ni pamoja na kuchelewesha mizigo.
Aidha, Parik alisema hivi sana anatafuta mkopo katika Benki ya NMB anaoukusudia kumsaidia kulipa baadhi ya madeni na kukuza tena mtaji wake.
Awali Tanzania PANORAMA iliripoti kuwa Parik, ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Indo Africa Investment Limited anadaiwa kuzunguka mikoa mbalimbali akijitambulisha kuwa ni mfanyabiashara mkubwa anayenunua mazao hasa kunde, mbaazi na choroko.
Kwamba mfanyabiashara huyo amekuwa akikusanya mazao katika mikoa ya Manyara, Arusha na Mwanza.
Kwa mujibu wa watu walio karibu yake, Parik anao mawakala wake ambao humkusanyia mazao ya wakulima kwa ahadi kuwa yanakwenda kuuzwa nje ya nchi kwa bei ya juu hivyo wapokee fedha kidogo na baada ya kuuzwa watapewa fedha zilizosalia.
Inadaiwa zaidi kuwa baadhi ya wakulima waliompatia kiasi kikubwa cha mazao na yeye kutokomea nayo, walikwenda kumsaka katika ofisi zake zilizopo eneo la Karakana, Barabara ya Nyerere mkoani Dar es Salaam ambako walikuta amekwishafunga ofisi yake.
TANZANIA PANORAMA INAENDELEA KUFUATILIA MKASA HUU.