Monday, July 21, 2025
spot_img

JINA LA ROSTAM AZIZ LATAJWA SHAMBULIZI LA TINDIKALI LA VIJANA WA CHADEMA IGUNGA

RIPOTA PANORAMA

JINA la Mfanyabiashara maarufu, Rostam Aziz limetajwa katika shambulizi la kumpiga na kummwangia tindikali machoni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Tesha lililofanywa na kikosi maalumu cha utekaji, utesaji na kushambulia watu cha Chama cha Demorasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Igunga.

Akizungumza hivi karibuni na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu matukio ya kihalifu anayoyajua yaliyotekelezwa na kikosi cha utekaji, utesaji na kushambulia watu cha Chadema kipindi akiwa kiongozi wa chama hicho, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha na pia Mhasibu Taifa wa chama hicho, Samsoni Mwigamba, alisema moja ya matukio ya kihalifu yaliyotekelezwa na kikosi hicho ni la kumpiga vibaya na kumwangia tindikali machoni, Mussa Tesha.

Mwigamba alisema kikosi hicho kilichokuwa na vijana waliokuwa wamevalia sare za CCM, kilimvamia Tesha wakati akishusha bendera ya Chadema na kujitambulisha kuwa wao ni vijana wa Rostam Aziz kisha wakampiga kabla ya kummwagia tindikali machoni wakimtuhumu kwa kosa la kushusha bendera hiyo.

Samsoni Mwigamba

ā€œHuyu Musa Tesha alikuwa yuko juu anashusha bendera ya Chadema na hawa vijana walikuwa wamevaa sare za CCM, walipofika wakamwambia unafanya nini. Wakajitambulisha kwamba sisi ni vijana wa Rostam Aziz, mbunge wetu, aliyekuwa mbunge wetu.

ā€œRostam alikuwa anatufaa sana sisi vijana wa hapa Igunga, alikuwa anatusaidia hela, anatupatia mitaji lakini CCM kwa ajili ya unafiki wenu mmefanya siasa zenu za hovyo, mmemshambulia, mmemwita gamba na nini mwishowe ameamua kujiuzulu ubunge na sisi vijana sasa hivi hatuna mtu wa kutusaidia.

ā€œSasa kama mlikuwa mnajiamini, kama mlikuwa hamjui kuwa hapa CCM ilikuwa inashinda kwa nguvu zake kwanini mnashusha bendera za wapinzani? Acheni tupambane basi bila Rostam tuone kama mtashinda, shuka,ā€ alisema Mwigamba wakati akizungumzia shambulio hilo lilivyotekelezwa.

Rostam Aziz ambaye alikuwa Mbunge wa Igunga tangu mwaka 1994 alijiuzulu wadhfa huo pamoja na ujumbe wa Kamati ya Halmashauri Kuu ya Chama (NEC) Julai, 2011.

Katika hotuba yake ya kujiuzulu alisema moja ya sababu za kuchukua uamuzi huo mgumu ni tuhuma za ufisadi na madai kuwa alisababisha CCM kufanya vibaya kwenye baadhi ya majimbo katika uchaguzi mkuu wa 2010.

Alisema tangu alipokuwa Mbunge wa Igunga alikuwa mwaminifu na mwenye kujali maendeleo ya wananchi badala yake binafsi.

Mwigamba alianza kwa kueleza kuwa matukio ya kuvamia, kuteka na kupiga watu kama yalivyofichuliwa hivi karibuni na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa yaliyokuwa yakitekelezwa na kikosi hicho cha Chadema yapo anayoyafahamu kwa uhakika.

ā€œSasa matukio ya kuvamia watu, teka, piga yako kadhaa ambayo mimi nayakumbuka vizuri na ambayo nimeyashuhudia. Kwa hiyo hilo la aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke nilikuwa nasikia, nilikuwa najua, la huyo kijana wa Temeke kwamba ni Chadema ndiyo walifanya hivyo lakini nilikuwa sina uhakika maana hilo sikuwepo.

ā€œKwa hiyo Katibu Mkuu mwenyewe naona alivyolithibitisha. Sasa mimi nitakupatia yale ambayo ninayafahamu kwa sababu nimeyashuhudia.

Mussa Tesha baada ya kurejea kutoka India kutibiwa, Pembeni yake ni kada wa CCM ambaye sasa ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba aliyeshiriki kikamilifu kampeni za CCM za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Igunga.

ā€œLa kwanza lilifanyika Igunga. Kule Igunga tumeenda, tumeanza kampeni sisi kama Chadema, halafu ikawa sasa CCM wanakuja kuzindua rasmi kampeni …. tulikuwa na hao vijana wetu wa intelejensia kwa hiyo kijana mmoja akaja akatuambia CCM wameagiza vijana wao washushe bendera zote za Chadema wakati wa uzinduzi wa kampeni zao,ā€ alisema Mwigamba na kuendelea.

ā€œYuko kijana mmoja anaitwa (anamtaja jina) alikuwa havai haya magwanda haya, tunaita nini ni makombati au ni mavitu gani! Yeye tulikuwa tunamtumia kama mtu wa Intelejensia. Kuingia kwenye kambi za CCM na kunusa …., yeye alikuwa analala kwenye guest ambayo walikuwa watu wengi sana wa CCM.

ā€œAlikuwa halali kwenye guest ambazo walikuwa wanatumia watu wa Chadema, kwa hiyo, na wakati CCM wanaendelea na mipango yao yote kulikuwa na vijana pia tumewachomeka huko, wenyeji wa Igunga ambao CCM walidhani ni wenzao.

ā€œKwa hiyo wakawa wanaleta information, information moja wapo ambayo ililetwa ilikuwa ni kwamba wakati Mkapa, mwenyekiti mstaafu wa CCM, Benjamin Mkapa anakuja kuzindua kampeni za CCM. CCM wameagiza vijana wao washushe bendera zote za Chadema.

ā€œWanataka mwenyekiti akute Igunga nzima ni kijani, nakumbuka pale Igunga, Oparesheni Kamanda ambayo ilikuwa wanaita central post, ilikuwa ni central post commander (CPC) maana yake tulikuwa na mfumo kama wa kijeshi hivi.

ā€œCentral post commander walikuwa wawili ambao waligawana kanda. Kulikuwa kuna Benson ambaye upande wake ulikuwa ukiwa unatokea Dar es Salaam kuelekea Mwanza, ukifika pale Igunga. Upande wa kulia nadhani ndiyo ulikuwa wa Waitara halafu upande wa kushoto ulikuwa wa Benson,ā€ alisema.

Akizungumzia jinsi kikosi hicho cha utekaji, kutesa na kushambulia watu kilivyokuwa kikitekeleza majukumu yake, Mwigamba alisema kilifahamika kama out post.

ā€œHii out post kilikuwa ni kikosi ambacho kiliishi, vilikuwa ni vikosi viwili vilivyoishi nje ya jimbo, … ambavyo hivyo vilikuwa chini ya Deputy Central Commander upande wa ulinzi, Lwakatare (Wilfred.)

ā€œKwa hiyo kimoja kilikuwa kinaishi Shelui ambayo ipo ndani ya Singida, nje ya Igunga na kimoja kilikuwa kinafanya kazi zake kutokea Nzenga ambayo ni nje ya Igunga upande wa Tabora. Sasa hizi out post zilikuwa ni nini, kilikuwa ni kikosi cha watu kikihusisha wanajeshi waliostaafu na waliofukuzwa jeshini.

ā€œHii out post ilikuwa na gari aina ya Land Cruiser ambayo inaaminika kwamba ipo vizuri, moja ya Land Cruiser iliyokuwa inatumika ni Land Cruiser ya mwenyekiti ya kijivu. Kwenye lile gari kuna silaha, lazima kuwe na mmoja mwenye bastola, halafu kuna mapanga, nondo na silaha nyingine za jadi.

Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu, Hayati Benjamin Mkapa baada ya kuwasili Igunga kwa ajili ya kuzindua kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge mwaka 2011

ā€œHalafu wana dereva ambaye pia ni mwanajeshi ambaye anajimudu, yaani ni kamanda pia. Wao kazi yao sasa, tukiambiwa mahali fulani kuna tukio wanakuja wanashambulia wakimaliza wanaondoka ili kusudi ile gari hata kama kuna mtu aliikariri, akashika na namba akawaambia polisi, wataisaka jimbo zima hawataiona,ā€ alisema Mwigamba.

Akielezea zaidi, Mwigamba alisema kikosi hicho baada ya kumaliza kazi ya kushambulia kama kilivyoelekezwa kilikuwa kikiondoka usiku huo huo kurudi kwenye maficho yake nje ya Jimbo la Igunga.

Alisema baada ya vijana wa intelejensia wa Chadema kuwapatia taarifa viongozi wao kuhusu mpango wa CCM kuwaagiza vijana wake kushusha bendera za Chadema, walitafuta vijana 24 wa pale pale Igunga ambao waliwalipa Shilingi elfu tano kila mmoja ambazo yeye Mwigamba alisema, kwenye ripoti yake ya fedha kama Mhasibu aliandika ni matumizi kwa ajili ya ulinzi maalumu.

ā€œKwenye ripoti yangu ya fedha ya uchaguzi niliandika kwamba ni ulinzi maalumu ambapo ilikuwa Shilingi 120,000 kwa vijana 24 na aliyepokea pesa alikuwa ni somebody Hemed Sabula, ambaye alikuwa msaidizi wa Lwakatare.

ā€œKwa hiyo wale vijana walipelekwa sasa kwenda ku – patrol kuona wana CCM watakaoshusha bendera ndipo wakamkuta sasa Tesha. Musa Tesha, yule aliyekuwa anazunguka sana na Mwigulu Nchemba.

ā€œHuyu Musa Tesha alikuwa yuko juu anashusha bendera ya Chadema na hawa vijana walikuwa wamevaa sare za CCM, walipofika wakamwambia unafanya nini. Wakajitambulisha kwamba sisi ni vijana wa Rostam Aziz, mbunge wetu, aliyekuwa mbunge wetu.

ā€œRostam alikuwa anatufaa sana sisi vijana wa hapa Igunga, alikuwa anatusaidia hela, anatupatia mitaji, lakini CCM kwa ajili ya unafiki wenu mmefanya siasa zenu za hovyo, mmemshambulia, mmemwita gamba na nini mwishowe ameamua kujiuzulu ubunge na sisi vijana sasa hivi hatuna mtu wa kutusaidia.

ā€œSasa kama mlikuwa mnajiamini, kama mlikuwa hamjui kuwa hapa CCM ilikuwa inashinda kwa nguvu zake kwanini mnashusha bendera za wapinzani? Acheni tupambane basi bila Rostam tuone kama mtashinda, shuka.

ā€œBasi, wakamshusha yule kijana, wakampiga. Sasa kosa alilolifanya yule kijana akawa amegundua vijana wawili wa hapo hapo Igunga lakini akawa hawajui majina akasema ninyi si vijana wa hapa hapa Igunga basi tutaonana.

ā€œWanasema huyo kijana alikuwa mbabe mbabe pale Igunga. Kwa hiyo walivyoona hivyo wameishampiga lakini amejua sura za hao wawili ndiyo wakaona sasa itakuwa shida.

ā€œSasa kuna vifaa ambavyo tulikuwa tukienda kwenye oparesheni kama hizo vilikuwa vinanunuliwa na mnunuaji alikuwa ni (anamtaja jina) kwa hiyo tulipokuwa tunakwenda Igunga kulikuwa na vifaa vimenunuliwa kama tindikali, baadhi ya sumu na kuna boksi ambalo CCM waliliokota pale kwenye guest…..

ā€œKulikuwa na vitu vingi vingi humo. Sasa vile vitu, ile tindikali ndiyo waliyompulizia yule bwana mdogo machoni ili kusudi asiweze kuona baadaye akaenda kuwatambua wale vijana kwenye gwaride la utambuzi.

Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu, Hayati Benjamin Mkapa akizindua kampeni za CCM za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Igunga mwaka 2011.

ā€œKwa hiyo wakampulizia lakini wakawa wamempiga sana na nadhani walijua amekufa, wakamtupa huko porini wakamuacha,ā€ alisema Mwigamba.

Alisema Tesha baada ya kutupwa akiwa amepigwa sana na kumwangiwa tindakali machoni alikuwa hajapoteza uhai na baadaye aliokotwa kabla CCM hakijamtambua kuwa ni kijana wake na kufanya mipango ya kumpeleka nchini India kutibiwa.

Mwigamba alisema vijana wawili wa kikosi cha utekaji na utesaji cha Chadema waliohusika kwenye shambulio la kumwangia tindikali machoni Tesha nao walipata madhara.

ā€œVijana wetu wawili katika jitihada za kumpulizia tindikali na wenyewe tindikali ikawa imewagusa kwenye mikono, wakaungua. Kwa hiyo wakajua kuwa watakapoanza msako wa kuwatafuta waliomfanyia Musa Tesha huo unyama watawakamata na wao kwa sababu tayari wana majeraha ya kuungua na tindikali.

ā€œKwa hiyo wakawekwa kwenye gari usiku huo huo, Lwakatare akawapeleka Nzenga akaenda akatafuta dispensari ya private, wakapatibiwa matibabu ya awali lakini bado hawakuachwa hapo Nzenga, wakasafirishwa kwenda Mwanza.

ā€œKule Mwanza kuna jamaa mmoja walimfukuza chama, alikuwa Meya, ….. ndiye aliyewapokea hao vijana, alikuwa mtu mwenye fedha zake… akawatafutia matibabu pale, wakatibiwa.

ā€œBaadaye katika namna ya kutafuta mahali pa kujificha akaleta taarifa kwamba hawa vijana wanasema kwa namna ambayo hili jambo lilivyo wasije wakakamatwa bora wapelekwe Morogoro kwa sababu mmojawapo alikuwa ana dada yake anaishi Morogoro vijijini, mashambani.

ā€œIkaja hiyo taarifa nikiwa kwenye kikao cha sekretarieti ya chama makao makuu, ikapitishwa hela Katibu Mkuu (Dk. Wilbroad Slaa), akaidhinisha na mimi ndiyo nilikuwa mtoa hela, zikatoka hizo hela nikamtumia ili aweze kuwasafirisha hao vijana, Katibu Mkuu akiwa bado ni Dk. Slaa. Kwa hiyo pesa zikatumwa baada ya hapo ndiyo sijui kama wale vijana walikwenda kweli,ā€ alisema Mwigamba.

Kada mwingine wa Chadema aliyezungumzia hilo (jina lake linahifadhiwa kwa sasa) alisema uchaguzi wa Igunga uliacha makovu mengi kwa wanaCCM na wanaChadema na kwamba Rostam alikuwa akiwasaidia watu wa Igunga kwa nia njema lakini baadhi ya aliokuwa akiwasaidiwa walikuwa wanaitumia misaada yake vibaya pasipo yeye mwenyewe kujua.

ā€œDk. Slaa na wengine waliokuwa Chadema hawatungi kuhusu kuwepo kwa kundi la kuteka, kutesa na kushambulia watu ndani ya Chadema. Wanajua wanachokiongea na Igunga, tukiizungumzia Igunga, ule uchaguzi ulikuwa na mambo mengi sana mabaya lakini Rostam alikuwa akisaidia kwa wema sema hao aliokuwa anawasaidia baadhi yao ndiyo walikuwa na yao mengine,ā€ alisema.

TANZANIA PANORAMA ITAENDELEA KURIPOTI MAMBO YALIYOFICHIKA AMBAYO HAYAJAPA KURIPOTIWA.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya