Monday, July 21, 2025
spot_img

WATATU WASIMAMISHWA KNCU WAKITUHUMIWA KUTAFUNA MIL 300

MWANDISHI MAALUMU – MOSHI

VIONGOZI watatu wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kufuja fedha za wakulima wa kahawa.

Wanatuhumiwa kufuja Shilingi milioni 300 za wakulima wa Chama cha Msingi cha Mwika Kinyamvuo na wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.

Mwenyekiti wa Bodi ya KNCU, Philemoni Ndossi amethibitisha kusimamishwa kwa viongozi hao kwa kueleza kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na malalamiko ya wakulima wa Chama cha Msingi Mwika.

Waliosimamishwa ni Meneja Mkuu, Godfrey Massawe, Meneja wa Fedha ambaye pia ni Meneja Majengo, Wilberd Lyimo na Meneja Huduma za Wakulima, Wilbert Nyella.

Taarifa zilizopatikana zinadai kuwa, KNCU iliingia makubaliano na wakulima hao ya kununua kahawa yao, kila kilo moja kwa Dola za Marekani 4.8, sawa na Shilingi 11,250 lakini baadaye ilitaka kuwalipa Shilingi 4,500 kwa kila kilo moja.

“Hizo taarifa ni kweli, wamesimamishwa kupisha uchunguzi, hatujui uchunguzi utachukua muda gani hayo ni mambo ya Serikali hatuwezi kuyaingilia na kahawa inayolalamikiwa ni ya msimu wa 2021/2022,” alisema Ndossi.

Inadaiwa kuwa KNCU ilikuwa na makubaliano na mnunuzi wa kahawa kutoka nje ya nchi ambaye mpaka sasa hajatajwa. Kwamba KNCU ingemuuzia mnunuzi huyo kilo 40,283 za kahawa ya kilimo hai kwa Dola za Marekani 4.8 kwa kilo moja na mnunuzi huyo tayari amekwishalipa Shilingi milioni 300 kama malipo ya awali lakini cha KNCU kimeshindwa kutekeleza makubaliano.

Inadaiwa zaidi kuwa mnunuzi huyo baada ya kuona KNCU kinakiuka makubaliano alifikisha malalamiko yake kwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ambaye alimwagiza Mrajis wa vyama vya ushirika Dk. Benson Ndiege kushughulikia malalamiko hayo.

Taarifa zinadai kuwa Waziri Bashe aliwaita ofisini kwake viongozi wa KNCU na kuwahoji kwanini wameshindwa kutekeleza makubaliano yao na mnunuzi huyo lakini viongozi hao wa KNCU hawakuwa na majibu.

Kwa muda mrefu viongozi wa KNCU wamekuwa wakiandamwa na tuhuma za ufisadi kwani haya yanatokea huku tuhuma nyingine zilizosababisha waliokuwa viongozi wa chama hicho kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi, yakiwa bado hayasahaulika.

Katika sakata hilo la awali, waliokuwa viongozi wa KNCU walishtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi baada ya kuuza mali za wanaushirika kwa bei ya kutupa.

Mauzo hayo yaliyozua utata yalikuwa ya shamba kubwa la kahawa la Gararagua, mali ya KNCU lililopo Wilaya ya Siha ambalo mauzo yake hayakuzingatia thamani halisi ya bei ya soko pamoja na kutokujulikana zilipokuwa ekari nyingine 2,000 za shamba hilo. 

KNCU ililiuza shamba hilo mwaka 2017 kwa Dola za Marekani milioni 4.2 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 9,240,000,000. Mauzo hayo yalikuwa ni mkakati wa KNCU kujinasua na madeni makubwa kinayodaiwa likiwamo deni la Shilingi bilioni 5.2 ambalo chama hicho kilikuwa kinadaiwa na Benki ya CRDB.

KNCU kiuliza shamba hilo kwa Kampuni ya Tanbreed/Africado baada ya chama hicho kuvunja mkataba na mwekezaji aliyekuwa akiliendesha, Kampuni ya Ocean Link Shipping Services Limited na kukubali kumlipa fidia ya Shilingi bilioni 2.9 malipo yaliyodaiwa kugubikwa na utata pia.

Mkataba baina ya KNCU na Kampuni ya Ocean Link Shipping Services Limited ulikuwa na uhai wa miaka 30 ambayo ilikuwa inaisha mwaka 2030 hivyo mwekezaji huyo alilipwa fidia ya miaka 16 iliyobakia kulingana na mkataba wake wa uwekezaji katika shamba hilo.

Ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi wa Ushirika, Mkoa wa Kilimanjaro ilionyesha kasoro kwenye mchakato mzima wa kuuzwa kwa shamba hilo lililokuwa na ukubwa wa ekari 5,414 kwa mwaka 1980.

Kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi iliyoishia Juni 30, 2018 aliyekuwa Mkaguzi wa Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro, Joseph Macha alisema kwa mujibu wa hati miliki ya shamba hilo yenya namba 4359, iliyotolewa Oktoba 1980, shamba hilo lilikuwa na ukubwa wa ekari 5,414.

Kwamba pamoja na hati hiyo kuonyesha shamba hilo lilikuwa na ekari 5,414, uthaminishaji wake uliofanywa Februari, 2015 ulionyesha lina ukubwa wa ekari 3,414. Ekari 2,000 zikiwa zimepungua.

Kasoro hiyo kwenye uthamini kama ilivyoonyeshwa kwenye ripoti ilifanya KNCU kukosa mapato ya Shilingi bilioni 5,545,931,759 ikiwa ni wastani wa Shilingi 2,772,966 kwa kila ekari moja huku ikiwa hakuna hatua zilizochukuliwa kutokana na udanganyifu huo. 

Kasoro nyingine iliyobainika kwenye ripoti hiyo ni shamba hilo kuuzwa chini ya thamani halisi ya bei yake, Shilingi bilioni 9.240,000,000 wakati thamani ya bei ya soko kwa mujibu wa ripoti ya uthamini wa shamba hilo ya mwaka 2015 ikiwa ni Shilingi bilioni 9.942,000,000.

Ripoti ya mkaguzi ilionyesha kuwa kwa sababu ya kuuzwa chini ya bei halisi ya soko, KNCU ilipata hasara ya Shilingi milioni 642 na ilipendekeza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu kasoro hiyo.

Mbali ya hayo, ripoti ilionyesha zaidi kuwa Bodi ya KNCU iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Aloyce Kittau na Makamu Mwenyekii Hatibu Mwanga, iliilipa Kampuni ya Uwakili ya Kisaka, Shilingi milioni 236 kama malipo ya ushauri kwenye mchakato wa uuzwaji wa shamba hilo.

Kwamba licha ya kampuni hiyo kulipwa mamilioni hayo ya fedha, hakuna nyaraka zozote zinazoonyesha kampuni hiyo ililipwa fedha hizo licha ya kuwa na Kampuni ya Uwakili ya Maruma ambayo hulipwa na KNCU kama mshauri wa masuala ya kisheria.

“Tulijaribu kuomba nyaraka zinazoonyesha makubaliano baina ya KNCU na Kampuni ya Uwakili ya Kisaka ikiwamo mikataba lakini KNCU kilishindwa kuthibitisha hilo pamoja na hati za malipo ya fedha hizo,” inasomeka sehemu ya ripoti ya mkaguzi.

Hayo yakiwa yamethibitishwa ndani ya ripoti ya mkaguzi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliunda timu ya kuchunguza mwenendo mzima wa uuzwaji wa shamba hilo.

Baada ya uchunguzi huo, Mwenyekiti wa Bodi KNCU na makamu wake pamoja na aliyekuwa Meneja, Honest Temba wakafunguliwa mashitaka ya uhujumu uchumi kwenye Makahama ya Hakimu Mkazi ya Moshi Mjini. Walishtakiwa kwa kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia KNCU hasara ya Shilingi bilioni 2.9.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya