Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Hassan Saidy |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
KUNA utata mkubwa kuhusu utaratibu wa utekelezaji miradi ya usambazaji umeme vijijini katika Wilaya ya Buhigwe, mkoani Kigoma.
Chanzo cha utata huo ni kukinzani kwa taarifa kuhusu anayepaswa kubeba gharama za ununuzi wa vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi wa miundombinu ya usambazaji umeme, kati ya mkandarasi na Serikali.
Mkinzano huo wa taarifa unawahusisha Meneja Miradi wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Samsoni Mayama, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Hassan Saidy na Meneja wa Tanesco wa Wilaya ya Buhigwe, Elioza Kachira.
Taarifa zilizoifikia mapema Tanzania PANORAMA Blog, zilieleza kuwa mkandarasi anayetekeleza miradi ya REA katika Wilaya ya Buhigwe, (jina tunalihifadhi kwa sasa kwa sababu hajapatikana kuzungumza) anatumia vifaa vya Tanesco kujenga miundombinu ya kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Sambamba na hilo, Tanzania PANORAMA Blog ilidokezwa kuwa mkandarasi huyo aliondoka eneo la mradi Juni, 2021 kabla hajamaliza kazi na taarifa zilienda mbali zaidi kwa kudai kuwa tayari amekwishalipwa sehemu kubwa ya malipo ya kazi huku kazi alizoacha hazijakamilika, zikifanywa sasa na mafundi wa mtaani kwa ujira wa ‘kibaba cha unga.’
Taarifa hizo zinashabihiana na zile zilizotolewa na baadhi ya watu walioko sasa eneo la mradi ambao katika mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog walisema waliombwa kufika Kigoma kwa ajili ya kumalizia kazi iliyoachwa na mkandarasi kwa sababu wana ufahamu wa kazi za ujenzi wa miundombinu ya umeme.
Mmoja wa watoa taarifa, alisema kuwa yeye aliitwa na rafiki zake kwenda Kigoma kufanya kazi hiyo kwa maelezo kuwa mkandarasi aliyekuwa akiitekeleza ameondoka kabla ya kuikamilisha.
Nguzo zenye nembo ya Tanesco zilizo katika vijijini mbalimbali ambako ujenzi wa miundombinu ya umeme inajengwa na mkandarasi aliyepewa zabuni na REA |
“Mimi nina ujuzi wa kujenga miundombinu ya umeme lakini sina kazi na nipo na wenzangu, wao walipata hiyo nafasi ya kazi ya Buhigwe mapema, lakini walipofika wakakuta kazi ni kubwa sana maana kuna vijiji saba ambavyo viikuwa bado miundombinu haijajengwa ndiyo wakaanita mimi kuongeza nguvu.
“Hapa tunasimamiwa na Meneja wa Tanesco wa Wilaya, huwa anakuja anatuletea soda na maji. Nilipofika niliambiwa mkandarasi baada ya kulipwa aliondoka kabla hajakamilisha kazi na hii kazi lazima iishe hivyo wanatafutwa watu wanaoweza kuifanya na malipo tunakubaliana hivyo hivyo. Ni kibaba cha unga tu,” alisema.
Meneja wa Tanesco Wilaya ya Buhigwe, Elioza Kachira alipoulizwa kuhusiana na hayo alisema mkandarasi huyo ameishakamilisha kazi lakini bado yupo eneo la mradi kwa ajili ya kufanya marekebisho madogo madogo.
Alisema taarifa kwamba aliondoka eneo la mradi mwezi Juni, 2021 siyo sahihi bali usahihi aliondoka Disemba mwaka jana na kuacha mafundi wake wachache ambao wanarekebisha upungufu unaojitokeza kwenye eneo lake la mradi.
Alipoulizwa kuhusu mkandarasi huyo kulipwa kabla hajamaliza kazi alisema jambo hilo siyo la kweli na kuhusu vifaa vya Tanesco kutumiwa na mkandarasi pia alikanusha.
“Siyo kweli kwamba alimaliza mwezi Juni, yeye kamaliza Disemba na hawa mafundi wake waliopo sasa wanarekebisha sehemu zenye upungufu na kuunganishia wateja umeme.
“Kwa hiyo hajamaliza kazi na mimi sijasaini popote kwa hiyo hajalipwa mpaka amalize kabisa kazi yake kwa mujibu wa ramani ya ujenzi katika mkataba wake.
“Na hilo la kutumia vifaa vya Tanesco siyo kweli, yeye katumia vifaa vyake mwenyewe katika vijijini vyote alivyokuwa na ukandarasi wa kujenga miondombinu yetu ya umeme,” alisema Meneja Kachira.
Maelekezo haya ya Meneja Kachira yanatofautiana na uchunguzi wa Tanzania PANORAMA uliobaini kuwa kinachofanyika sasa katika eneo la mradi ni ujenzi wa miundombinu ya umeme.
Uchunguzi umeonyesha kuwa jana kazi iliyokuwa ikifanyika ni kufunga vifaa ambavyo kwa lugha ya kimombo vinaitwa, pin insulator, disc insulator na channel iron kwenye transformer kubwa iliyopo Kijiji cha Kibwinga, Wilaya ya Buhigwe.
Aidha, vijijini ambavyo mafundi waliopo sasa eneo la mradi wamethibitisha kujenga miundombinu na siyo kufanya marekebisho ni pamoja na Msangara, Kibande, Nyarubonza, Mkatanga na Kibande.
Uchunguzi umebaini zaidi kuwa vifaa vya Tanesco vilivyotumika kwenye mradi unaotekelezwa na mkandarasi huyo ambavyo pia vinafahamika zaidi kwa kimombo ni Palomeric, disc insulator, base plate, nguzo za mita tisa zinazofahamika kwa jina la LT Poles na katika baadhi ya vijiji mradi ulikotekelezwa zipo nguzo ndogo zinazoingia kwenye njia za mtaani zenye nembo ya Tanesco.
Kwa upande wake Meneja Miradi wa Tanesco Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Mayama alisema miradi ya REA inayotekelezwa na wakandarasi katika Wilaya ya Buhigwe ni ya Serikali hivyo vifaa vinavyotumiwa na wakandarasi hao kujenga miundombinu hiyo ni vya Serikali vikiwa chini ya usimamizi wa Tanesco.
“Kama nilivyokwishakwambia, hii miradi haina kificho chochote, hii miradi ni ya Serikali, ipo wazi. Ni miradi ya Serikali kwa hiyo vifaa vinavyotumiwa na mkandarasi ni vya Serikali chini ya Tanesco. Kazi ya mkandarasi ni kujenga miundombinu tu, vifaa vinanunuliwa na Serikali.
“Ndiyo maana mkandarasi akimaliza kazi haondoki na vifaa hivyo bali huwa anaviacha kwa sababu ni mali ya Serikali,” alisema Mhandisi Mayama huku akielekeza maswali mengine aliyoulizwa aulizwe Meneja wa Tanesco Wilaya ya Buhigwe.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy ambaye amefanya mahojiano ya Tanzania PANORAMA Blog kuhusu taratibu za utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya umeme inayosimamiwa na REA, majibu yake yametofautiana kwa kiwango kikubwa na yale yaliyotolewa na Mhandisi Mayama na Meneja Kachira.
Akijibu maswali aliyoulizwa na Tanzania PANORAMA; kupitia kwa Meneja Uhusiano wa REA, Veronica Simba, Mhandisi Saidy ambaye kwanza aliulizwa; wakandarasi wanaopewa kazi na REA kusambaza umeme vijijini wanaruhusiwa kutumia vifaa vya Tanesco, kama vile nguzo na nyaya kwenye miradi wanayoitekeleza?
Akijibu, Mhandisi Saidy anaandika, ‘wakandarasi wanatakiwa wanunue vifaa vya ujenzi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini.
‘Kama Tanesco wana utaratibu wa kuazimishana vifaa na wakandarasi, Tanesco wanaweza kutolea maelezo suala hilo lakini REA huwalipa wakandarasi gharama ya vifaa na ujenzi wa miundombinu.’
Tanzania PANORAMA ilimuuliza tena Mhandisi Saidy kuwa; wakandarasi waliopewa kandarasi na REA kusambaza umeme vijijini, kwa sababu zozote zile wanaruhusiwa kuondoka eneo la mradi kabla ya kukamilisha kazi yao na au kuiacha kazi husika mikononi mwa mkandarasi mwingine au mafundi binafsi wa mtaani?
Mhandisi Saidy anaandika kujibu; ‘wakandarasi wanapewa wigo wa mradi unaohusisha maeneo, urefu wa njia za umeme, mashine umba na idadi ya wateja watakaounganishwa na huduma ya umeme.
‘Mkandarasi anaweza kutoa sub-contract kwa kampuni iliyopitishwa na Tanesco na kuridhiwa na REA.
‘Mkandarasi haruhusiwi kuondoka eneo la mradi lakini kwa kuwa katika mkataba kuna maeneo vijiji/vitongoji vingi anaweza kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na mpango kazi wake.
‘Suala la muhimu ni kuwa mkandarasi lazima amalize kazi ndani ya kipindi kilichoainishwa katika mkataba.’
Na mwisho Tanzania PANORAMA ilimuuliza hivi Mhandisi Saidy; utaratibu wa kulipa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA upoje?
Naye anaandika tena kujibu; ‘mkandarasi anapomaliza kazi, huandaa nyaraka za madai na kuzipitisha Tanesco kwa ajili ya uhakiki, baada ya kuhakikiwa huletwa REA kwa taratibu za malipo.’
Tanzania PANORAMA itazidi kukuletea ripoti zaidi kuhusu sakata hili.