RIPOTA TANROADS
UTIAJI saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Igawa, Uyole, Songwe hadi Tunduma sehemu ya tatu, kuanzia Nsagala hadi Ifisi itakayojengwa kwa njia nne katika Jiji la Mbeya ni moja ya mikakati mikubwa ya Serikali.
Hayo yaliyoelezwa hivi karibuni mkoani Mbeya na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila wakati wa hafla ya utiaji Saini mkataba za ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 29.
Mhandisi Mativila ambaye alitumia fursa ya kuzungumza kwenye hafla hiyo kuufahamisha umma kuhusu upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo, utaratibu wa zabuni ya ujenzi, gharama, utekelezaji wa kazi ya ujenzi na kumtaja mkandarasi, alisema utiaji saini huo unadhihirisha dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini hususan katika Mkoa wa Mbeya kwa kuboresha mtandao wa barabara.
Alisema upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Igawa hadi Tunduma yenye urefu wa kilomita 218 pamoja na barabara ya mchepuko ya Uyole hadi Songwe yenye urefu wa kilomita 48.9 ulianza mwaka 2019 na ulikamilika Agosti 2021.
“Kazi hii alitekelezwa na Kampuni ya Usanifu wa Kihandisi ya STUDI International ya Tunisia kwa kushirikiana na Kampuni ya Global Professional Engineering ya Tanzania kwa gharama ya Dola za Marekani 1,557,500, chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.
“Sehemu ya barabara ya Nsagala, Uyole hadi Ihisi, Uwanja wa Ndege wa Songwe ina urefu wa kilomita 29 na itajengwa kwa njia nne, ambapo ni sawa na kilomita 58 kwa barabara ya njia mbili,” alisema Mhandisi Mativila.
Mtendaji Mkuu huyo wa TANROADS aliendelea kuufahamisha umma kuwa ujenzi utazingatia vigezo mbalimbali ikiwemo tabaka la chini la msingi litakalojengwa kwa kifusi cha changarawe kilichochanganywa na saruji yenye unene wa milimeta 350.

“Tabaka la juu la msingi litajengwa kwa kutumia zege la lami lenye unene wa milimeta 210 na upana wa barabara utakuwa mita 7.0 kwa kila barabara ya njia mbili ya upande mmoja, upana wa mita 9.0 kwa sehemu ya katikati ya kutengenisha barabara na kutakuwa na njia ya watembea kwa miguu yenye upana wa mita 2,5 kila upande,” alisema Mhandisi Mativila.
Aidha, Mhandisi Mativila alieleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utahusisha Daraja la Nzovywe, makaravati madogo, kuweka alama za barabarani na taa za barabarani.
Akizungumzia taratibu za manunuzi alisema zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo ilitangazwa Juni 7, 2022 na kufunguliwa Oktoba 20, 2022 ambapo jumla ya zabuni nane zilipokelewa na kufanyiwa tathmini.
Alimtaja mkandarasi aliyeshinda tuzo ya kujenga barabara hiyo kuwa ni Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) ya China na gharama za mradi ni Shilingi 138,735,674,662.20, bila kujumlisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni Shilingi 24,970,828,439.20 na alitaja muda wa utekelezaji wa mradi kuwa ni miezi 24.
Barabara hiyo ni sehemu ya barabara kuu ya Tanzania hadi Zambia (TANZAM) inayoanzia Dar es Salaam hadi Tunduma mkoani Songwe ambayo inaunganisha nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mativila, barabara hiyo ilifanyiwa ukarabati kwa mara mwisho mwaka 1993, hata hivyo miaka michache iliyopita sehemu ya barabara ya Iyayi hadi Igawa yenye urefu wa kilomita 11.5, ilifanyiwa ukarabati na sasa ina hali nzuri.
Mhandisi Mativila alisema sehemu ya barabara iliyobaki kuanzia Igawa hadi Songwe (Mbeya/Songwe Border) yenye urefu wa kilomita 142 imeharibika sana kutokana na ongezeko la magari yenye uzito mkubwa na barabara kutumika muda mrefu bila kukarabatiwa.
HABARI HII ILIANDIKWA KWANZA KATIKA JARIDA LA TANROADS LA FEBRUARI 2022. KUTOKANA NA UMUHIMU WAKE, TANZANIA PANORAMA BLOG INAICHAPISHA IKIWA IMEHARIRIWA KWA KIWANGO KIDOGO ILI KUWAFIKIA WASOMAJI WAKE WA NDANI NA NJE YA NCHI.