RIPOTA WA WAZIRI MKUU
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wa vyama vya siasa watumie majukwaa waliyonayo kuhimiza kilimo cha michikichi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.
Agizo hilo alilitoa Jumapili, Februari 26, wakati akizungumza na wadau wa zao la chikichi mkoani Kigoma kwenye ukumbi wa NSSF. Wadau hao wanajumuisha wakulima, wazalishaji miche, wakamuaji mawese, viongozi wa vijiji, viongozi wa taasisi za fedha, viongozi wa wilaya, halmashauri na mikoa.
Majaliwa aliitisha kikao hicho kujadili changamoto zinalolikabili zao hilo na kujadiliana njia za kuliendeleza ili nchi iwe na kiasi cha kutosha cha mafuta ya mawese na kupunguza kuagiza kiasi kikubwa cha mafuta kutoka nje nchi.
“Viongozi wote wa mikoa, wilaya na wa vyama vya siasa mnayo majukwaa ya kukutana na wananchi kila wakati. Twendeni tukahamasishe wananchi walime michikichi kwa sababu ni zao litakalowapatia fedha kwa muda mrefu,” alisema.
Aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya wenye ardhi inayokubali zao hilo wafanye hivyo mara moja kwani mbali na kuwapa fedha za uhakika, litaleta fursa ya ajira kupitia viwanda vinavyofunguliwa.
“Chikichi ni fursa, chikichi ni maendeleo. Ni fursa ya kuleta viwanda hapa Kigoma na kwenye mikoa mingine itakayolima zao hili. Chikichi ni uchumi, ni uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa kitaifa,” alisisitiza Majaliwa.
Akizungumzia kuhusu mahitaji ya mafuta ya kula nchini, Majaliwa alisema hivi sasa mahitaji ya mafuta nchini ni zaidi ya tani 650,000 huku uzalishaji ukikadiriwa kuwa tani 290,000 tu hivyo tani 360,000, sawa na asilimia 55.4 huagizwa kutoka nje ya nchi na kuigharimu Serikali takribani Shilingi bilioni 470 kila mwaka.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, Majaliwa alisema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kwa kufanya mageuzi makubwa katika mazao ya mafuta ikiwemo michikichi.
“Mageuzi haya yanakwenda sambamba na kupanda miche mipya iliyoboreshwa ambayo ina uzalishaji mkubwa wa mafuta. wana-Kigoma tuamue sasa hivi tupande michikichi kwa bidii,” alisisitiza.
Aidha, Majaliwa alisema Serikali ilichukua hatua za makusudi kuliingiza zao la michikichi katika orodha ya mazao ya kimkakati. Mazao mengine ya kimkakati aliyoyataja ni pamba, tumbaku, kahawa, korosho, chai, mkonge, zabibu na alizeti.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu Majaliwa kuzungumza na wadau hao, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alisema uzalishaji unaendelea wa mbegu na miche bora ya michikichi aina ya TENERA inayotoa mafuta mara tatu zaidi ya aina ya DURA ambayo inalimwa na wakulima kwa takribani asilimia 90.
“Hadi kufikia Januari, 2023 TARI kwa kushirikiana na kampuni binafsi imezalisha jumla ya mbegu milioni 14.14. Kati ya hizi mbegu milioni 11.59 zimezalishwa na TARI na mbegu milioni 2.54 zimezalishwa na kampuni binafsi zikiwemo FELISA, NDF na Yangu Macho Group Ltd,” alisema Mavunde.
Alisema kati ya mbegu milioni 14.14 zilizozalishwa, mbegu milioni 9.60 zimekwishasambazwa na kuoteshwa na taasisi mbalimbali zikiwemo JKT na magereza, halmashauri zote nane za Mkoa wa Kigoma, halmashauri 25 za nje ya Mkoa wa Kigoma, vituo vya TARI na Wakala wa Mbegu za Kilimo Tanzania (ASA).
Amesema hadi kufikia Januari, 2023 jumla ya miche 3,122,566 imepatikana ambapo miche 1,968,087 imegawiwa kwa wakulima ndani na nje ya Mkoa wa Kigoma.