Friday, May 16, 2025
spot_img

JINSI FEDHA ZA BENKI YA DUNIA ‘ZILIVYOPIGWA’

 

Charles Werongo

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

MIRADI mingi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na umeme iliyotekelezwa kwa awamu mbili na wakarandasi wa ndani kwa fedha zilizotolewa kwa mkopo na Benki ya Dunia, tayari ‘imekwishaoza.’

Miradi hiyo ya mabilioni ya fedha ilitekelezwa mwaka 2006 na 2010 ikihusisha ujenzi wa barabara katika Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na ujenzi wa miundombinu ya umeme ikiwa ni kusikimika nguzo, kutandaza nyaya za umeme na kufunga taa za barabarani.

Hayo yameelezwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mabibo Construction Co. Ltd, Charles Werongo katika mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog yaliyofanyika ofisini kwake Mabibo, Dar es Salaam.

Werongo alikuwa akijibu na kutoa ufafanuzi wa jinsi kampuni yake ilivyotekeleza miradi mbalimbali iliyopewa na Serikali kwa gharama za fedha za Benki ya Dunia baada ya kudaiwa kuwa ni moja ya wakandarasi waliotafuna bila huruma fedha hizo.

Katika utekelezaji wa miradi hiyo, inadaiwa baadhi ya wakarandasi walijenga barabara na miundombinu ya umeme chini ya kiwango na katika baadhi ya maeneo walitumia vifaa visivyofaa vinavyopatikana kwa bei ya chini ambavyo pia ni hatarishi kiusalama.

Kwamba hayo yalifanywa makusudi na wakarandasi hao ili waweze kuweka kibindoni mabilioni ya fedha za mkopo za miradi hiyo; fedha ambazo sasa zinalipwa na Serikali.  

Kampuni ya Werongo ya Mabibo Construction Co, Ltd, pamoja na mambo mengine inadaiwa kusimika miti ya mirunda kama nguzo za umeme katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Ilala. Maeneo hayo ni Buguruni kwa Binti Madenge hadi Buguruni Malapa.

Maeneo mengine ambayo kampuni hiyo inadaiwa kusimika nguzo za miti ya mirunda kwa ajili ya kushikilia nyaya za umeme yapo Wilaya ya Temeke eneo la Tandika katika vitongoji vya Keko Toroli, Tambuka Reli, Mashine ya Maji, Mtoni Unguja na kwingineko.

Awali Tanzania PANORAMA Blog ilifanya mahojiano na mmoja wa mafundi waliohusika kusimika nguzo za miti ya mirunda ambaye alikiri hilo kwa kueleza kuwa yeye aliitwa kwenda kufanya kazi ya kusimika nguzo na kukuta ni za miti ya mirunda lakini baada ya kusimika, Mhandisi Mshauri aliyekuwa akisimamia ujenzi huo kwa Wilaya ya Temeke alibaini kasoro hiyo na kuiamuru Mabibo Constuction Co, Ltd kuiondoa mara moja kwa sababu ingesababisha maafa makubwa.

Mirunda

 

“Yeye kwenye huo mradi alitakiwa kuweka ‘sub contractor’ lakini badala yake alituita baadhi ya mafundi tunaojua kazi za umeme kwenda kufanya kazi hiyo na mimi nikiwemo. Hiyo mirunda mimi niliikuta na tuliambiwa tusimike hiyo.

“Sasa huwezi kumuhoji bosi wako akishatoa amri, tulisimika tukafunga nyaya za umeme na tukaweka taa Buguruni hiyo kuanzia kwa Binti Madenge hadi Buruguni Malapa.

“Hiyo ni kwa Wilaya ya Ilala na kwa Wilaya ya Temeke tulifunga Tandika kuanzia Keko Toroli, Tambuka Reli, Mashine ya Maji, Mtoni Unguja na kwingineko. 

“Sasa yule Mhandisi Mshauri wa Wilaya ya Temeke hakutaka ubabaishaji alipofika tu akafoka na akaamuru mirunda yote iondolewe ziwekwe nguzo za ukweli, ikabidi mimi ndiyo nitumwe sasa kwenda kutafuta nguzo halisi maana Werongo hajui chochote kuhusu umeme na kampuni yake ni ya ujenzi wa barabara siyo umeme.

“Nikaenda kununua nguzo za ukweli Mbezi Makonde kuna jamaa namfahamu anauza pale, tukaja tukafunga na hizo ndiyo zipo mpaka leo.

“Lakini kwa upande wa Buruguni kote tulikofanya, sijui jamaa alicheza vipi na hao watu wa manispaa na Mhandisi Mshauri hawakuhoji chochote na hazichukua muda kwa sababu mirunda inaliwa sana na mchwa, miezi minne zikawa zimeanguka zote na mpaka leo hakuna umeme kote huko.

“Jamaa akakunja mabilioni yake akatia mfukoni, sisi alitulipa hela yetu ya ufundi hayo mengine muulizeni yeye,” alisema fundi huyo ambaye jina lake tumelifadhi.

Akijibu hayo yote, Werongo kwanza alikanusha kata kata kampuni yake kupewa zabuni ya kujenga miundombinu ya umeme mahali popote tangu alipoianzisha.

“Hata siku moja siyo kweli, sisi, kampuni yangu hatujawahi kupata tenda yoyote ile ya kujenga miundombinu ya umeme. Tangu kampuni hii ianzishwe inahusiana na ujenzi wa barabara, mitalo na nyumba lakini mambo ya umeme, hilo halipo,” alikanusha Werongo.

Alipoelezwa kuwa Tanzania PANORAMA Blog imefika katika eneo la miradi mbalimbali aliyoitekeleza katika Wilaya za Ilala na Temeke na kukuta yote imeoza na kumbukumbu zilizopo kwenye manispaa hizo zinaonyesha kuwa kampuni yake ndiyo iliyokuwa na kandarasi ya kujenga miundombinu hiyo kwenye baadhi ya vitongoji vya Buguruni ambako sasa hakuna nguzo hata moja; alibadili kauli, alisema.

“Jamani, mimi ni mwafrika, ni mweusi. Iko hivi, 2006 na 2010 ndiyo tulitekeleza huo mradi, tulipata zabuni ya kujenga barabara na kuweka taa. Ni kweli kama mmefika hayo maeneo kwa sasa taa hazipo, hatujui zipo wapi, sisi tulimaliza jukumu letu tukakabidhi.

“Barabara pia zilishaharibika ni muda mrefu sana tangu tuzijenge, taa za barabarani tulizofunga zilishatolewa lakini hilo siyo jukumu letu ni jukumu la wale tuliowakabidhi baada ya sisi kumaliza kazi,” alisema Werongo.

Nguzo halisi za umeme

 

Alipoulizwa barabara alizozijenga zilipaswa kudumu kwa muda gani kwa makadirio ya chini alisema hilo halikuwemo kwenye mkataba wake bali kilichokuwa ndani ya mkataba huo ni ‘guarantee’ ya muda usiozidi mwaka mmoja.

“Hayo mambo mimi hayakuwa kwenye mkataba wangu, mkataba wangu ulikuwa na ‘guarantee’ ya barabara hizo na ni miezi sita nadhani au mwaka mmoja, basi,” alisema.

Akijibu kuhusu kusimika nguzo za miti ya mirunda kama nguzo za umeme alisema siyo kweli bali alifunga nguzo ambazo hazina viwango zilizokataliwa na Mshauri Elekezi wa Wilaya ya Temeke aliyemtaka kuzibadilisha, jambo ambalo alilitekeleza lakini kwa upande wa maeneo ya Ilala hakukuwa na tatizo.

Kwa maneno yake mwenyewe; alisema, “Nguzo za kawaida ndiyo tulisimika na tulifunga taa, siyo mirunda. Hizo zilikuwa nguzo za umeme. Sasa tuliweka hizo nguzo zikakataliwa na mshauri kuwa hazikuwa na ubora na zile ni kabla mradi hatujakabidhi, zikakataliwa kwamba hazina ubora.

“Tukabadilisha, aliyekuwa anasimamamia huo mradi ni huyo huyo mmoja kwa Wilaya ya Temeke na Ilala, ndiye aliyekataa kwa upande wa Temeke akataka zibadilishwe.

“Lakini huku upande mwingine wa Buguruni hakukuwa na shida, hakukataa na tunachojua sisi tulipata shida kwenye mradi wa kule Tandika kwamba nguzo hazina ubora na tukabadilisha.

“Mimi niwaambie sasa, msipende mambo ya kusikia sikia, huo mradi wa umeme kwanini umefeli, naweza kuwaambia mimi lakini suala la kwamba hazina ubora lilikuwa Tandika tukabadilisha nguzo lakini siyo Buguruni.

“Na Mshauri Elekezi alikubali kwa upande wa Buguruni kwa sababu ule mradi ulikuwa na Mshauri Elekezi wa umeme ambaye alikuwa anacheki kuanzia waya mpaka nguzo.

“Huo mradi umefeli pote, hata ukiambiwa kulikuwa na ‘street light,’ hii Manzese utakubali? mahakama ya ndizi mpaka midizini kulikuwa na taa za barabarani lakini sasa hazipo, Mbona sasa hata huku Manzese kuliwa na taa lakini sasa hazipo? we fuatilia. Ule ulikuwa mradi wa Benki ya Dunia ambao ulikuwa mpaka huku Manzese lakini sasa hamna kitu hata huku Manzese, hamna.

“Mimi kwenye mkataba wangu kuna ‘parkage ya street lights,’ mkataba wangu wa ujenzi wa barabara ulikuwa na ‘parkage ya steet lights’ kwa hiyo mimi kazi yangu ni kumtafuta ‘sub contractor.’ Lakini simkumbi kwa sababu tunazungumza mambo ya miaka ya 2006.

“Na mnapaswa mjue kuwa kuna sehemu tatu ambazo mnatakiwa muende, hapo kwanza kuna mwenye mradi wake ambao ni manispaa anaweza kuelezea pande zote kwa sababu na wao walikuwa na mshauri wa mradi wa umeme na wa kusimamia hizo barabara, halafu mimi mkandarasi na kulikuwa na Mshauri Elekezi wa Benki ya Dunia.

“Mimi nafanya kazi yangu, nikimaliza inakaguliwa lakini mtu asikudanganye kuwa eti ule mradi wa umeme umefeli kwa sababu nguzo zilikuwa mbovu.

“Ule mradi umefeli kwa sababu kwanza hawakuwa na hela ya kununua umeme kwa ajili ya mtaani hao Manispaa ya Ilala. Umeme wa kutumia, ule umeme haukuwa wa ‘solar’ ulikuwa wa Tanesco. Waliweka weka mwanzoni wakashindwa, mtaani wakawa wanachangishana wakashindwa.

“Sasa kushindwa kwao, wakati ule ndiyo kulikuwa na shida ya waya za umeme. Kwa hiyo waya zikawa zinaibiwa, waya kuibiwa nguzo nazo zikawa zinaibiwa na msishangae kama kuna vishoka na watu wanaruhusiwa kununua nguzo zao hiyo siyo ajabu.”

Nyaya za umeme (Picha kwa hisani ya mtandao)

 

Kuhusu mkandarasi mdogo aliyempa ukandarasi wa kujenga miundombinu ya umeme; alisema “sisi tuliwapa mafundi siyo kampuni . Mimi ninachosema ni hivi nilipewa kufanya kazi nikaifanya, ikakaguliwa ikaonekana ina ubora isipokuwa na ubora nikarekebisha, nikafanya kipindi changu kile cha maangalizo nikamaliza, ‘that my end,” alisema.

Tanzania PANORAMA ilipomuuliza Weronga mahali aliponunua nguzo zilizokataliwa na Mshauri Elekezi wa Wilaya ya Temeke, ghafla alibadilika na kuanza kung’aka, alisema, “Nguzo zilizokataliwa niliponunua ‘is not your issue’ kwa sababu nguzo zilizoharibika ulinunua wapi haikuhusu.

“Umeleta nguzo imethibitishwa kuwa hii ndiyo ina ubora, kwa sababu kuna mtu ambaye ni ‘consultant,’ yule ni ‘specialist’ wa umeme wa mradi mzima wa ‘world bank.’ Umeleta kitu ambacho sicho amekukatalia lakini umeleta kitu kingine amesema hiki ndicho sahihi sasa shida ni nini?

“Ni kweli baadhi ya nguzo nilinunua Makonde, yule jamaa ni ‘supplier’ mkubwa, ni mtu wa dini sana, ana maduka yake pale Mwenge. Ataendaje kununua fundi wakati mwenye jukumu ni mimi?

“Watu wa ‘world bank’ walikuwepo kuangalia, ndiyo wanaotoa hela, hii kazi ilikuwa ya ‘world bank’ watu wa manispaa walikuwepo,  watu wa jiji walikuwapo, sasa sidhani kama hapo unaweza kufanya kitu cha ajabu. Mimi ndiyo najua kwanini huo mradi ulifeli.

“Mimi ninapoweka fundi akija mkaguzi na msimamizi wa mradi akisema ‘ok, issue’ ni nini? Mimi nilifanya kazi nzuri na kazi yangu ikakamilika, mimi nimemaliza.

“Nguzo nilinunua wapi inakuhusu nini, wewe shati lako umenunua wapi?” aliuliza kwa ukali Weronga na Tanzania PANORAMA ilimjibu Kariakoo.

Akiwa bado amekunja ndita aliuliza bei lililonuliwa na kujibiwa sh. 17,000 mashati sita katika maduka ya wachina, kisha alitaka kuonyeshwa risiti na kujibiwa ipo imetunzwa mahali salama nyumbani. Hapo alishusha pumzi kwa nguvu huku akieleza mshangao kwa mtu mzima kutunza risiti ya sh.17,000 aliyonunulia mashati kwa wachina kisha aliendelea kueleza kuwa;

“Kama kuna watu, hao mafundi wamewaambia kuwa hizo nguzo hazipo ni kweli zilikaa miezi mitatu au minne hivi nadhani zikaanza kuharibika, zikaanguka lakini siyo eneo hilo tu, miradi yote ya Benki ya Dunia imefeli,” alisema kisha akakataa kuulizwa swali jingine lolote kwa kile alichodai amekwishasigana na Tanzania PANORAMA Blog.

Jitahada za kupata kauli ya uongozi wa Wilaya ya Ilala na ile ya Mshauri Elekezi wa mradi kuhusu sakata hili zinaendelea.


 

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya