RIPOTA PANORAMA
WAZEE, wajane na watu wasiojiweza wanaopata msaada wa fedha za kujikimu kimaisha kutoka Jumuiya ya KSIJ Tanga Jamaat, sasa wametoa kilio cha kucheleweshewa fedha za msaada huku baadhi yao wakidai kunyimwa fedha hizo.
Taarifa za hivi karibuni zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimedaiwa kuwa baadhi ya wahitaji hao sasa hawana chakula huku wengine wakilazimika kuanza kuomba kutoka kwa wasamaria wema baada ya kuwepo sintofahamu ya misaada waliyokuwa wakiipata kutoka KSIJ Tanga Jamaat.
Baadhi ya vilio vya wahitaji hao ambavyo Tanzania PANORAMA Blog imevisikia vikitolewa kwa wasamaria wema wanaoombwa msaada, vinadai Mwenyekiti wa KSIJ Tanga Jamaat, Hussein Walji amekuwa akitoa fedha kwa wahitaji kwa kadri anavyojisikia badala ya kufuata utaratibu uliowekwa na jumuiya wa kusaidia wazee, wajane na watu wasiojiweza.
Aidha, inadaiwa Walji ambaye anaiongoza jumuiya hiyo kiimla huku akiwa hana msaidizi hata mmoja amekuwa akichota fedha katika akaunti ya KSIJ Tanga Jamaat, ambazo hutolewa na Shirikisho la Jamaat Afrika na kuzitumia kwa maslahi yake binafsi.
Walji pia anadaiwa kuwadhulumu baadhi ya wahitaji kwa kuwasainisha vocha zinazoonyesha wamepokea kiasi kikubwa cha fedha huku akiwapatia pungufu na zile alizowasainisha.
Haya yameibuka ikiwa tayari kuna madai ya muda mrefu ya Walji kudaiwa kupoka uongozi wa jumuiya hiyo kwa nguvu na kukaidi wito wa Serikali iliyoutoa kwa viongozi wa KSIJ Tanga Jamaat baada ya kupata malalamiko ya kuwepo kwa mgogoro ambao umekuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Inadaiwa Septemba 19, 2022 Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Emmanuel Kihampa aliuandikia barua uongozi wa jumuiya hiyo kufika ofisi kwake kwa ajili ya kuzungumzia malalamiko ya wazee, wajane na wasiojiweza wanaosaidiwa na KSIJ Tanga Jamaat lakini agizo lake hilo halikutekelezwa kwa madai kuwa wito huo ulichelewa kufika.
Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Kihampa alipoulizwa na Tanzania PANORAMA kuhusu hilo alisema mambo ya jumuiya za kidini hawezi kuyazungumzia kwenye vyombo vya habari kwa sababu ya kulinda hadhi ya heshima ya jumuiya za aina hiyo.
Kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Henry Mwaibambe katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA alisema anafuatilia lilipo faili la mgogoro huo kwani uliporipotiwa polisi yeye alikuwa hajahamishimiwa katika mkoa huo.
Hata hivyo jitihada za kumpata Kamanda Mwaibambe ili kujua iwapo faili hilo limefika mezani kwake hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuita bila majibu na jana ilipokelewa na mmoja wa wasaidizi wake aliyeeleza kuwa yuko safarini Mkoa wa Mbeya.
Inadaiwa polisi mkoani Tanga walifanya uchunguzi wa mgogoro wa jumuiya hiyo na kubaini kiini cha mgogoro pamoja na mwenendo usioridhisha wa matumizi ya fedha ikiwa ni pamoja watu wasio viongozi kwenda kuchota fedha kwenye akaunti ya KSIJ Tanga Jamaat lakini kabla ya kuanza kuchukua hatua, faili hilo liliwekwa kando.
Walji mwenyewe alipoulizwa kuhusu madai hayo hakukanusha wala kukubali na badala yake aliomba kukutana na Tanzania PANORAMA Blog kwa mazungumzo ya mezani na hata aliposisitiziwa kuwa huo siyo utaratibu sahihi bali ajibu madai anayoelekezewa alisisitiza msimamo wake huo.
Baadaye Walji, ambaye aliwahi kutiwa hatiani na kuhukumu kwa kosa la wizi wa friza na Mahakama ya Mwanzo Tanga Mjini, alianza kuitumia Tanzania PANORAMA video ambazo hazihusiani na kile alichoulizwa na alipokumbushwa kujibu tuhuma dhidi yake hakujibu lakini baadaye alianza kusambaza mitandaoni barua yenye mwelekeo wa kuitisha Tanzania PANAROMA.
Jitihada za kumtafuata Waziri wa Mambo ya Ndani, Injinia Hamadi Masauni ambaye wizara yake ndiyo yenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao pamoja usajili wa jumuiya ili kuzungumzia kadhia hii bado zinaendelea.