RIPOTA PANORAMA
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithinaasheri Jamaat ya Tanga, Hussein Walji anayetuhumiwa na wanachama wa jumuiya hiyo kwa ubadhirifu wa fedha za jumuiya, kudhulumu fedha za watu masikini, kupoka uongozi wa jumuiya na kuiongoza kwa mkono wa chuma ana rekodi ya wizi.
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog na nyaraka ilizoziona zinathibitisha pasipo shaka kuwa Mwenyekiti Walji alikamatwa, akashtakiwa kwa kosa la jinai katika Mahakama ya Mwanzo Tanga Mjini na kutiwa hatiani kwa wizi wa friza.
Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Tanzania PANORAMA Blog imeziona, Walji alikuwa mshtakiwa wa pili katika kesi ya jinai namba 272 ya mwaka 2019 na alitiwa hatiani na Mahakama ya Mwanzo Tanga Mjini mwaka huo huo baada ya kukutwa na kosa la wizi wa friza; akahukumu kifungo cha nje cha miezi sita.
Katika kesi hiyo, Walji alishtakiwa kwa kukutwa na friza ya wizi dukani kwake ambayo yeye na mshtakiwa mwenzake walidaiwa kuiiba katika duka la mfanyabiashara mwenzake na yeye alidai mahakamani hapo kuwa friza hiyo iliyokuwa namba BE 150 ni mali yake na akawasilisha risiti aliyodai ni ya manunuzi.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Tanga Mjini, S.B Odeyo alisema utetezi uliotolewa na Walji kuwa hata yeye dukani kwake kuna friza nyingi kama aliyokamatwa nayo na kutuhumiwa kuiiba dukani kwa mfanyabiashara mwenzake, siyo utetezi wa kweli kwa sababu alishindwa kuleta friza ya aina hiyo kuthibitisha kauli yake mahakamani.
Aidha, Hakimu Odeyo alisema vielelezo vya risiti alivyowasilisha Walji mahakamani havionyeshi kama kweli ni risiti za manunuzi ya friza aliyokamatwa nayo na stock movement aliyoiwasilisha nayo haionyeshi duka ambalo friza hiyo ilichukuliwa na lini.
Hakimu Odeyo alisema ushahidi wa Walji aliouwasilisha mahakamani ni wa kughushi kwa uwazi jambo ambalo linaweza kumfanya ashtakiwe kwa kosa la jinai la kughushi.
Akijitetea kabla ya kuhukumiwa, Walji aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ni mgonjwa, ana wazazi wagonjwa. Hakimu Odeyo aliyekuwa na washauri wawili, Mwajuma Mrisho na Mbwana Rashidi alimuhukumu Walji kifungo cha nje cha miezi sita baada ya kumtia hatiani kwa wizi.
Wakati huo huo, Mwenyekiti Walji mbali na tuhuma lukuki zinazomuandama huku naye akiendelea kuzifumbia macho, inadaiwa anaendelea na vitendo vyake vya kuiba fedha za msaada zinazotolewa na Shirikisho la Afrika la Jamaat kwa walemavu na wajane kupitia KSIJ Tanga Jamaat.
Moja ya mbinu anazotumia Walji kukwapua fedha hizo za wajane na walemavu ni kuwasainisha kiasi kikubwa cha fedha kisha anawapatia fedha kidogo.