RIPOTA PANORAMA
JESHI la Polisi limethibitisha kuwa Padri Evodius Msigwa alimpiga risasi mtoto mwenye umri wa miaka tisa anayefahamika kwa jina la Adamu.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog jana, Kamanda wa Polisi (RPC) wa Mkoa wa Mara, Longinus Tibashubwamu amesema hakuna ubishi kuwa Padri huyo alimpiga risasi mtoto Adamu lakini alitenda kitendo hicho kwa lengo la kumdhoofisha nguvu.
Kamanda Tibashubwamu amesema mtoto huyo alipigwa risasi na Padri Msigwa katika tukio la wizi baada ya kuruka ua na kuingia kwenye eneo la mapadri alikoiba sungura aliokamatwa nao.
“Hakuna ubishi kwamba Padri alimpiga risasi ya mguu lakini huyo kijana alikuwa anaiba sungura kwenye yard yao. Aliruka akaingia kwenye fence, akaiba, wakati wa kutoka ndiyo akapata majeraha hayo,” amesema Kamanda Tibashubwamu.
Kamanda huyo ambaye awali aliahidi kuzungumza na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu ukweli wa tukio hilo baada ya kuulizwa na kusema hajawahi kulisikia hivyo apewe muda afuatilie na angerejea kwa PANORAMA kulingumzia, hakutekeleza ahadi yake hadi alipoulizwa tena jana na kwa maneno yake mwenyewe, amesema;
“Nilicheki nikaona suala lenyewe halina kichwa wala miguu ndiyo maana sikukupigia tena kwa sababu tukio ni la mwaka 2020. Huyo kijana alikuwa amekwenda kuiba sungura kwa Padri.
“Padri akapiga risasi juu, yule kijana kweli, akampiga risasi ya mguu, wakamkamata wakampeleka hospitalini. Wale wazazi wa huyo mtoto wakaenda kumuomba Padri awasamehe kesi isiende mahakamani, Padri akasamehe. Juzi juzi tena sijui wamepata bush lawyer gani, ndiyo wanaanza kuliibua,” amesema Kamanda Tibashubwamu.
Akizungumzia hatua zitakazochukuliwa baada ya kubaini kuwepo kwa tukio hilo, Kamanda Tibashubwamu amesema ameagiza wasaidizi wake kuipeleka kesi hiyo mahakamani haraka iwezekavyo bila kujali kama mtoto huyo ni mgonjwa au mzima kwa kile alichosema ni mwizi.
“Sasa mimi nimetoa maelekezo, kwa sababu huyo kijana yupo, awe anaumwa asiumwe kwa sababu ni mwizi, vielelezo vipo, kesi iende mahakamani tuache kusumbuka kwa sababu kesi ya msingi ipo, kesi ya wizi, ushahidi upo na sungura wengine walikutwa nyumbani kwake.
“Kwa hiyo mambo ya jeraha kutopona mimi sioni kama ninanihii, lakini yule ni mwizi kama wezi wengine na jalada lipo, ushahidi upo kwa hiyo kesi muda wowote nimemwambia OCD ipelekwe mahakamani kwa sababu ni kesi ambayo ni ya mwaka 2020, kwa sababu itakuwa inasumbua,” amesema.
Kamanda Tibashubwamu ameleza kuwa anafikiri wazazi wa mtoto Adam wamepata wanasheria wa mitaani ambao wamewashauri kwenda kwa Padri Msigwa kumtaka awalipe.
“Nafikiri wazazi wanakwenda wanapata ma bush lawyer, wanakwenda wamwambie Padri labda awalipe ama nini. Hakuna ubishi kwamba Padri alimpiga risasi ya mguu lakini huyu kijana alikuwa anaiba sungura kwenye yard yao. Aliruka akaingia kwenye fence, akaiba, wakati wa kutoka ndiyo akapata majeraha hayo,” amesema.
Kuhusu mahali alipo Padri Msigwa kwa sasa amesema amehamishwa kituo cha kazi kutoka Wilaya ya Bunda mkoani Mara kwenda Wilaya ya Ukerewe iliyopo Mkoa wa Mwanza lakini hivi karibuni aliitwa akaitikia wito.
“Padri yupo amehamia yuko huko wapi, Ukerewe huko, lakini yupo na muda wowote akihitajika anatoa ushirikiano na anakuja. Juzi aliitwa akaja. Kwa sababu naona kuna watu wanaifukua fukua kama Padri alimjeruhi kijana mzuri lakini huyu kijana ni mwizi.
“Na nguvu aliyotumia ni ndogo kwa sababu alimlenga mguu kumdhoofisha aweze kukamatwa, angekuwa na nia mbaya si angemshuti tu akamuua lakini alilenga mguu ili asimame, akamatwe na sungura hao,” amesema.
Kamanda Tibashubwamu amesema polisi waliiweka kando kesi hiyo baada ya wazazi wa mtoto Adamu kwenda kumbembeleza Padri Msigwa awasamehe, kesi hiyo isipelekwe mahakamani.
“Wanambembeleza sasa na mapadri na wenyewe si unajua ni watu wa Mungu, wazazi walienda wakambembeleza tusamehe, basi wakaendelea kumtibu, sasa nasikia juzi juzi waliibuka tena, kwa hiyo Padri yupo tayari kesi iende mahakamani. Nimetoa maelekezo hiyo kesi iende mahakamani, sheria ichukue mkondo wake,” amesema.
Tanzania PANORAMA Blog imemuuliza Kamanda Tibashubwamu kama ni sahihi kwa Polisi kumwachia mwizi aliyekamatwa akiwa na kithibiti alichoiba naye amesema hilo lilifanyika baada ya Padri Msigwa kusema anaachana na kesi hiyo.
“Padri alisema achana nayo. Aliyeibiwa sungura yule Padri alisema achana nayo, kesi siitaki, mwache, baada ya kwenda kubembelezwa na wazazi. Lakini kesi ya msingi ipo, ushahidi upo vizuri, jalada lipo vizuri kwa hiyo nimemwambia OCD haraka iwekezanavyo hiyo kesi iende mahakamani.
“Kama ni kumsamehe atamsamehe mahakamani huko huko. Tumeamua kuipeleka mahakamani nafikiri huko itakuwa kwenye njia sahihi zaidi, Padri akiamua kumsamehe atamsamehe huko kwa hiyo ina maana ndani ya wiki tunayoanza kesho kutwa hii atapelekwa mahakamani.
“Mtu anaingia kwenye yard yako, hujui ana silaha gani, hujui amejihami vipi. Nguvu aliyoitumia ilikuwa ni ya kadri kwa sababu alimshuti mguu, ni nguvu ya kadri kumdhoofisha nguvu, alimpiga risasi moja tu mguuni.
“Wazazi nafikiri wanapata watu wanawadanganya danganya lakini jinai ipo, jalada lipo vizuri, sungura wapo walioibwa, kila kitu kimesimama kwa hiyo nafikiri kesi itaenda vizuri tu, nafikiri ikienda mahakamni hizi kelele kelele zote zitaisha,” amesema Kamanda Tibashubwamu.
Awali, ndugu wa mtoto Adam walidai kuwa aliitwa na Padre Msigwa akiwa anatoka kununua mkaa kabla ya kushutumiwa kwa kuiba sungura wake kisha akampeleka kwenye banda la sungura ambako alimuamuru kulala chini kifudifudi kisha akampiga risasi mbili kwenye paja la mguu.
Ilidaiwa kuwa banda la sungura hao lipo kwenye njia ya kwenda kanisani ambayo inatumiwa na watu wote na kwamba baada ya tukio hilo kufikishwa polisi, mtoto huyo alipelekwa hospitali akiwa chini ya ulinzi wa polisi ambao walimlinda usiku na mchana kwa siku mbili kabla ya kutoweka bila taarifa yoyote.
Mtoto Adamu ambaye inadaiwa wakati anapigwa risasi alikuwa mwanafunzi wa darasa la pili, aliacha masomo kwa sababu ya kusumbuliwa na majeraha ya risasi alizopigwa na Padri Msigwa na sasa anatibiwa kwa mganga wa kienyeji.