RIPOTA PANORAMA – TANGA
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeeleza kusikitishwa na kitendo cha Kampuni ya Batul Aluminium, kung’oa vioo katika jengo lake linalofanyiwa ukarabati na Kampuni ya Rick Plan ya jijini Tanga.
Masikitiko hayo yametolewa leo na Meneja Miliki wa Nyumba za NSSF, Geofrey Thomas katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu kitendo kilichofanywa na kampuni hiyo inayojishughulisha na uuzaji vioo vya milango na madirisha ambaye amesema kilichofanyika ni uhalifu kama uhalifu wowote wa kuvamia nyumba na kuiba.
“Kuna mkandarasi tumempa kazi ya kukarabati jengo letu huko Tanga, sasa kuna supplies amekwenda kung’oa vioo, sisi tutamchukulia hatua kwa kufanya kitendo hicho.
“Alichokifanya ni uhalifu kama alikuwa na jambo lolote alitakiwa awasiliane na mkandarasi na siyo kwenda kufanya uharibifu kwenye jengo la mfuko kwa hiyo tunaendelea na taratibu nyingine za kisheria,” amesema Thomas.
Alipotafutwa mmiliki wa Kampuni Batul Aluminium kuzungumzia kitendo aalichokifanya, hakupatikana lakini mtoto wake aliyejitambulisha kwa jina la Burhan Fakrudin alipoulizwa, alikiri baba yake kwenda kwenye jengo hilo na kung’oa vioo kwa kile alichodai kuwa mkandarasi alishindwa kuwalipa malipo yao ya mwisho.
“Sisi hapa tunauza vioo cash, hatukopeshi, Brayan (mkandarasi) alikuja hapa kutulilia zaidi ya mara nne tumsaidie kumfungia vioo katika jengo hilo, tukaenda kufunga,” amesema Burhan.
Alisema thamani ya vioo viliyofungwa katika jengo hilo lenye ghorofa tatu ni Shilingi milioni 38 na tayari wamelipwa Shilingi milioni 27.
Akizungumza kutoka nje ya nchi kuhusu kitendo kilichofanywa na Kampuni ya Batul Aluminium, Mkandarasi anayekarabati jengo hilo, Brian Kikoti amesema kitendo kilichofanywa na kampuni hiyo ni uhalifu na kuwataka NSSF kuchukua hatua za kisheria haraka.
Amesema iwapo wadai wote wangekuwa wakifanya vitendo kama kilichofanywa na Kampuni ya Batul Alumunium katika kazi za ukandarasi kusingekuwa na majengo yanayojengwa na kukamilika.
“Huyo supplies wa vioo tulishamlipa zaidi ya asilimia 80 ya malipo yake, fedha zilizobaki ilikuwa alipwe mara baada ya wateja wake kukagua jengo kisha wamalizie malipo yote kwangu na kwa aliyefunga vioo hivyo,” amesema.
Tukio hilo lililofanyika jana katika jengo la NSSF lililopo barabara ya Eckenforde jirani na Tanesco Ufundi, limewaacha wapangaji wa jengo hilo wakitumia mapazia kuzuia mbu pamoja na wezi.