RIPOTA PANORAMA
WAKATI skandali inayomuandama Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Kaimu Abdul Mkeyenge ya kutoa leseni ya kufanya biashara ya kupokea, kuhifadhi na kusafirisha kontena ‘kinyemele’ ikiwa haijapoa, imeelezwa kuwa sasa anafanya vikao vya siri na wadau wake mbalimbali kuhahakikisha skandali hiyo inazimwa.
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog kutoka kwa vyanzo vyake vya habari zimeeleza kuwa Mkeyenge, kwa nyakati tofauti amekuwa akikutana na wamiliki wa Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited kujadili namna ya kuliweka sawa jambo hilo na pia amekuwa akikutana na watu wazito (majina yao yamehifadhiwa kwa sasa) akiwalilia wamkingie kifua, skandali hii isiendelee kuripotiwa.
Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited ndiyo iliyopewa leseni ya kufanya biashara ya kupokea, kuhifadhi na kusafirisha kontena huku ikiwa haina vifaa vya kupokea na kupakia kontena na aidha;
Inadaiwa, TASAC ilitoa leseni hiyo bila kufanya ukaguzi kwenye eneo ambalo Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited iliomba kufanyia biashara; eneo ambalo kuna biashara nyingine ya uhifadhi wa kontena tupu za wenye meli.
Aidha, Mkeyenge anadaiwa kufikiwa kwanza na waombaji leseni hiyo kwa mazungumzo yaliyorasihisha kutolewa kwa leseni huku TASAC chini ya Mkeyenge ikijua kuwa Kampuni ya Mas Holding and Conteiner Depot Limited haina vigezo vya kupewa leseni.
TASAC ni mdhibiti wa biashara ya kupokea, kuhifadhi na kusafirisha kontena na moja ya majukumu yake ni kukagua eneo la biashara linaloombewa leseni kama lina vigezo vilivyowekwa na kuhakikisha muombaji anavyo vifaa vya kupokea na kupakia kontena kabla ya kutoa leseni.
Tangu Novemba mwaka, Tanzania PANORAMA Blog ilipofika ofisini kwa Mkeyenge ikiwa imefumbata maswali mawili mkono kuhusu ukiukwaji huo wa utaratibu wa utoaji leseni uliofanywa na ofisi yake ili kupata kauli yake ambapo Katibu Muhtasi wake alieleza bosi wake huyo hayupo hivyo aonwe Mkuu wa Kitengo cha Biashara, Habari na Mawasiliano, Josephine Bujimu ili ayajibu nay eye kuahidi kutoa majibu; maswali hayo hayajajibiwa hadi leo.
Tanzania PANORAMA Blog ilimfikishia Mkeyenge maswali hayo kupitia simu yake ya kiganjani na kuyasoma lakini hakujibu na kila anapopigiwa simu hapokei.
Taarifa nyingine zilizopatikana wakati uchunguzi wa skandali hii ukiendelea zilidai kuwa Mkeyenge amekuwa akijificha ofisini kwake na kuelekeza wasaidizi wake waseme hayupo kila mara waandishi wa Tanzania PANORAMA Blog wanapofika ofisini kwake kwa ajili ya kufanya naye mahojiano.
Tanzania PANORAMA Blog inaendelea kumtafuta Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ili kutoa kauli ya Serikali kuhusu skandali hii.