Tuesday, December 24, 2024
spot_img

OUT SEHEMU YA MAENDELEO ZANZIBAR

DK. MOHAMED OMARY MAGUO

NI utamaduni wa kawaida, sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ambazo husherehekewa kila ifikapo Januari 12 kuambatana na matukio mbalimbali ya kijamii, kiutamaduni na kimaendeleo.

Hapa nataja matukio hayo kwa uchache; uzinduzi na ufunguzi wa shule mpya, hospitali, vituo vya afya, zahanati, miradi ya maji na barabara. Vilevile, sherehe hizo hupambwa na sanaa na michezo, ukiwemo mchezo wa soka ambao hushirikisha timu za ndani ya nje ya nchi zinazoshindana kuwania Kombe la Mapinduzi.

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ni Taasisi ya Umma ya Elimu ya Juu inayojivunia kuwa sehemu ya maendeleo ya Zanzibar. Madhumuni ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha visiwa hivyo vinajipatia maendeleo katika sekta zote ikiwemo elimu.

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilianzishwa mwaka 1992 kwa Sheria ya Bunge nambari 17. Lengo lake ni kutoa elimu ya juu kwa njia huria, masafa na mtandao na hivi sasa kina umri wa miaka 30 na huduma zake zipo Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.

Zanzibar inaposherehekea miaka 59 ya Mapinduzi, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinajivunia kuwa sehemu ya maendeleo makubwa kiliyoyafikia kikiwa kinatoa mchango wa kukuza na kuimarisha rasilimali watu, utafiti, ushauri wa kitaalamu, ugunduzi na ubunifu.

Katika umri wake wa miaka 30 ya kutoa huduma ya elimu ya juu kwa umma kama yalivyo madhumuni ya kuanzishwa kwake; Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, kimekuwa sehemu ya mafanikio yaliyofikiwa Zanzibar ambayo sasa imetimiza umri wa miaka 59 tangu ilipojinasua kutoka kwenye makucha ya ukoloni;

Na kinajivunia kuwa na matawi Unguja na Pemba yanayotoa huduma kwa Wazanzibari katika ngazi zote za elimu ya juu.

Ieleweke kuwa dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuona Wanzanzibari wanapata elimu ya juu kwa gharama nafuu wakiwa popote pale mijini na mashamba.

Zanzibar inapoazimisha miaka 59 ya mapinduzi, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinajivunia walimu na wanafunzi wake wanaofanya utafiti katika sekta mbalimbali zikiwemo utalii na uchumi wa buluu. Kupitia tafiti hizo kunapatikana ufumbuzi wa changamoto zinazokabili sekta hizo na pia kuibua fursa za ajira kwa vijana na jamii nzima ya Wanzanzibari.

Zipo Tasinifu na Tazmini nyingi kutoka kwa wahitimu zilizowasilisha masuala mbalimbali ya Zanzibar. Tasnifu na Tazmini hizo zinapatikana mtandaoni kupitia ā€“ OUT – Repository.

Pia wapo wahitimu waliotafiti katika sekta binafsi, mazingira, ujasiriamali, usafirishaji, Lugha ya Kiswahili, elimu, afya, miundombinu nakadhalika. Tafiti hizo zinatumiwa na watunga sera kuandaa sera nzuri zinazoiletea Zanzibar maendeleo ya kasi.

Rekodi ya ushiriki wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwenye maendeleo yaliyofikiwa na Zanzibar ni ndefu ikiwemo kutambuliwa kama taasisi ya elimu ya juu inayotoa wahitimu wa fani mbalimbali ambao ni sehemu ya watumishi wa Umma wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Watumishi hao wapo katika sekta mbalimbali na baadhi ni viongozi waandamizi, maafisa na watumishi wa kawaida katika sekta ya umma na binafsi wakitoa huduma kwa wananchi.

Chuo Kikuu Huria Tanzania kinahusika kuwafudisha watumishi wa sekta za elimu, afya, maji, utalii, biashara, hoteli na ukarimu ambao sasa wanashiriki kuijenga Zanzibar.

Alumni wa Chuo Kikuu Huria Tanzania ni miongoni mwa watumishi wanaofanya kazi nzuri kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar.

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinatoa mchango wa kuitangaza Zanzibar kimataifa. Katika matangazo ya chuo, huelezwa bayana kuwa chuo kina matawi Unguja na Pemba na faida zake ni kuimarisha sekta ya utalii, huduma za hoteli na ukarimu kutokana na wingi wa watalii na wageni wanaotembelea Zanzibar.

Jengo la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Tawi la Pemba.

Mwaka 2021 Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilifanya mahafali yake Zanzibar. Mahafali hayo yaliitangaza Zanzibar duniani na huo ni mchango wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wa kuiletea Zanzibar Maendeleo.

Lakini pia, Chuo Kikuu Huria Tanzania kikiwa moja ya Taasisi za Elimu ya Juu nchini, kama ulivyo utamaduni wa taasisi za elimu ya juu kimekuwa kikiandaa mashairi, tenzi, insha na makala za kuhamasisha jamii katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni. Kazi hii inafanyika kupitia mitandao ya kijamii, redio, magazeti na televisheni.

Zanzibar inapoazimisha miaka 59 ya mapinduzi, Chuo Kikuu Huria Tanzania kinaendelea na mikakati yake ya kuzalisha wataalamu wenye viwango vya juu vya ubora ili kuendelea kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.

Ni fahari kwa Chuo Kikuu Huria Tanzania kuendelea kubuni program muafaka kwa Zanzibar na hasa uchumi wa buluu ili kusaidia na kuendeleza kazi nzuri inayofanywa na Rais Hussein Mwinyi na Serikali yake.

Mwandishi wa Makala haya, Dk. Mohamed Omary Maguo ni Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya