RIPOTA MAALUMU
POMBE ya mnazi imetajwa kuwa na Madini ya Zinki na Magnesiamu, pia protini, wanga, Asidi ya Amino na Vitamini B3 na C, hulainisha ngozi na hufanya nywele kuwa na afya .
Kinyume kabisa na ambavyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya watu kuwa pombe hiyo ina madhara makubwa ya kiafya kwa watumiaji, Harrison Omonhinmin ambaye ni mtaalamu wa lishe, amekaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akieleza kuwa utafiti alioufanya mwaka 2014 kuhusu tathimini ya maudhui ya Antioxidant ya pombe hiyo ikilinganishwa na vinywaji vingine vyenye kilevi, uliiweka katika nafasi ya mwisho ya kuwa na upungufu wa vitamini C na Antioxidants nyingine.
Utafiti wa Omonhinmin unaonyesha kuwa Pombe ya Mnazi inatengenezwa kwa kutumia utomvu wa mnazi na mitende na ni kinywaji kinachotumiwa na watu wa mataifa mbalimbali duniani, ikiwa ni pamoja mataifa ya Marekani ya Kusini, Asia ya Kusini na Afrika, ikiwemo Tanzania na inajulikana kwa majina tofauti tofauti.
Katika Bara la Afrika, Pombe ya Mnazi inanyweka zaidi kwenye mataifa ya Tanzania, Kenya, Nigeria, Ghana na Cameroon na kwa miongo mingi pombe hiyo ambayo sukari yake husababisha uchashushaji wa haraka unaokoleza kiwango cha kilevi kwa muda mfupi baada ya kutengenezwa, imekuwa na simulizi nyingi; lakini katika siku za karibuni, simulizi zisizokuwa rasmi zimekuwa zikiitaja kuwa kwenye kundi la pombe ambazo si salama kwa matumizi ya binadamu.
Omonhinmin anakaririwa kueleza kuwa utafiti alioufanya kuhusu Pombe ya Mnazi ulionyesha ina kiwango cha chini cha Glycemic ikiwa na maana kuwa pombe ya mnazi haipandishi kwa kasi kiwango vya sukari ya damu.
Kwa mujibu wa Omonhinmin, Glycemic ni neno linalotumiwa kufafanua muda unaochukuwa kwa viwango vya sukari ya damu kupanda, ikilinganishwa na vinywaji vingine vya sukari Pombe ya Mnazi ni bora kwa wagonjwa wa kisukari.
BBC inamkariri mtaalamu mwingine Collins Akanno kuwa kwa watu wanaopambana na ugonjwa wa moyo na mishipa, kwa wanawake wanashauriwa kutumia glasi moja ya Pombe ya Mnazi kwa siku na kwa wanaume glasi mbili kwa siku.
Akanno anaeleza kuwa Pombe ya Mnazi ina Madini ya Potasiamu ambayo husaidia neva na misuli kufanya kazi vizuri na kwamba mishipa hii yenye joto na misuli huwezesha mapigo ya moyo kwenda vizuri na hupunguza uwezekano wa mtu kupata shinikizo la damu.
Lakini Omonhinmin yeye anaeleza zaidi kuwa Pombe ya Mnazi ina wanga unaosaidia kuupa mwili nguvu na pia husidia kulainisha ngozi na kuzifanya nywele kuwa na afya huku Akanno yeye akakizia kuwepo kwa vitamini, zinki na magnesiamu katika Pombe ya Mnazi kunaifanya kuwa chakula ambacho watalaamu wa ngozi na nywele wanapaswa kuzingatia.