Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema anasubiri uchunguzi wa vyombo vya dola dhidi ya tuhuma za kuomba rushwa ya ngono na unyanyasaji wanawake mahali pa kazi zinazomkabili Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Gabriel Mwita Thobias ili hatua zichukuliwe.
Amesema Tume ya Ajira na vyombo vya dola vinafanyia kazi skendali hiyo na vitatoa ushauri kwa Serikali ambao utafanyiwa kazi.
Waziri Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumzia skendali hiyo, taratibu zinazopaswa kufuatwa kwa ajira za maafisa wa juu wa taasisi za umma na hatua zitakazochukuliwa baada ya taasisi za uchunguzi kukamilisha kazi yake.
“Siijui historia ya ajira ya huyo mkurugenzi, lakini ninachojua kwa afisa wa ngazi ya juu kiasi hicho mpaka kuajiriwa ni lazima kulikuwa na ‘vetting’ sasa sijui ilikuwaje.
“Kuna Tume ya uajiri na TAKUKURU na vyombo vingine vya dola acha vifanyie kazi na kama walivyosema TAKUKURU wanalisaka faili la tuhuma hizo, wakikamilisha uchunguzi watatushauri na sisi tutafanyia kazi ushauri wao.
“Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ana taratibu zake, akikamilisha uchunguzi kwa sababu ameitisha hilo faili atashauri na sisi kama Serikali tutafanyia kazi. Tunasimamia sheria,” alisema Waziri Prof. Mbarawa.
Gabriel Mwita Thobias |
Gabriel Mwita Thobias ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) anatuhumiwa kuomba rushwa ya ngono na kunyanyasa wanawake mahali pa kazi akiwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Kampuni ya Tanzania Leaf Tobacco Company Limited (TLTC), mkoani Morogoro.
Thobias alitiwa hatiani kwa mujibu wa taratibu za ajira kwa makosa hayo na kamati ya nidhamu iliyoundwa kuchunguza tuhuma zake ambayo kiongozi wake alikuwa mzungu, aitwaye Wayne Kluckow, ambaye anafanya kazi katika Ofisi ya Kanda ya TLTC iliyoko Afrika Kusini.
Jopo la kuchunguza na kusikiliza tuhuma za Thobias liliundwa na wajumbe vigogo waliotoka nje ya nchi hasa wale wanaoshughulikia mambo ya ‘compliance.’ kwa sababu ya uzito wa nafasi ya uongozi aliyokuwa nayo TLTC.
Thobias alifukuzwa kazi Oktoba 23, 2018 na nafasi yake ya Ukurugenzi wa Rasilimali Watu wa TLTC ilichukuliwa na Gladys Almas, mmoja wa wafanyakazi waliopata wakati mgumu kutoka kwake na pia aliyepata kushinikizwa na Thobias kukiuka taratibu za zabuni ili kuipatia upendeleo kampuni inayotajwa kwa jina la Nice, kupewa zabuni ya kulisha kiwanda cha Tumbaku.
Taarifa zinaonyesha kuwa baada ya Thobias kufukuzwa kazi, Menejimenti ya TLTC iliripoti tuhuma zake kwa TAKUKURU makao makuu ambayo ilituma timu ya maafisa uchunguzi iliyoongozwa na mtu aitwaye Hazina Mwisho iliyokwenda Morogoro kufanya uchunguzi huo.
Hata hivyo, katika hali ya sintofahamu, baadaye wachunguzi hao walikutana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Stephen Kabwe kabla ya kurejea makao makuu ambako baada ya hapo ukimya ulitawala kuhusu uchunguzi huo. Zipo taarifa kutoka kwa watu wa karibu zinazoonesha kuwa Dk. Kebwe ana uhusiano wa kindugu na Thobias.
Afisa wa TAKUKURU, Hazina Mwisho aliyeongoza timu iliyokwenda Mkoa wa Morogoro kufanya uchunguzi wa skendali ya Thobias alipouliuzwa kuhusu kilichobainika kwenye uchunguzi na walichoongea na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kebwe alisema hakumbuki hata kidogo kushiriki uchunguzi huo.
Lakini alipobanwa, alisema; “Nasema sina kumbukumbu hizo, hizo kazi zipo ofisini makao makuuu, kama hiyo kazi ilikuwepo mwelekezaji wa utekelezaji alikuwa Mkurugenzi Mkuu.
“Mimi sipo makao makuu kwa sasa nipo Wilaya ya Temeke. Hizo ‘issue’ za Kampuni ya Tumbaku zilikuwa na maelekezo ya Mkurugenzi Mkuu hicho ndicho ninachokikumbuka sasa wewe wasiliana na makao makuu.”
Mkurugenzi Mkuu wa sasa wa TAKUKURU, Salum Hamduni alipoongea na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni aliahidi kulifukua faili hilo na kulifanyia kazi.
Mbali na kutuhumiwa na kufukuzwa kazi kwa makosa ya kuomba rushwa ya ngono na unyanyasaji wanawake mahali pa kazi, Thobias anatuhumiwa pia kutumia ofisi na madaraka yake vibaya na taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa katika moja ya Benki alizopata kufanya kazi baada ya kufukuzwa TLTC, nako aliondoka baada ya kuandamwa na skendali zile zile zilizomfukuzisha kazi TLTC.
Afisa mmoja aliyepata kufanya kazi na Thobias katika benki hiyo, (jina limehifadhiwa) amesema skendali hiyo haijafutika bali ipo kwenye rekodi za benki hiyo.
“Kwa sasa sipo hapo benki, lakini hilo jambo lipo kwenye rekodi kwa sababu faili lipo, waliopo ofisini hapo benki wanaweza kulizungumzia kwa kurejea rekodi za kwenye faili,” amesema.
PANORAMA Blog inaendelea kufuatilia skendali hii.