MCHEZA soka bora wa karne wa FIFA na gwiji wa kabumbu wa Brazil, Edson Arantes Do Nascimento – Pele, aliyefariki dunia Disemba 29, 2022 akiwa na umri wa miaka 82 ameacha mambo matano ambayo hayafahamiki na wengi duniani.
Pele ambaye haina shaka kuwa ndiye mchezaji soka bora zaidi kuwahi kutokea duniani, taarifa ya kifo chake ilianza kusambaa baada ya binti yake, Kely Nascimento aliyekuwa karibu naye hospitalini alikokuwa amelazwa kuandika mitandaoni kuwa “kila kitu tulichanacho ni shukrani kwako. Tunakupenda sana, pumzika kwa amani.”
Kely ambaye alikuwa akiwafahamisha mashabiki wa soko duniani kuhusu mwenendo wa afya ya baba yake kila kipindi chote alichokuwa amelazwa hospitalini, aliandika ujumbe huo siku ya Alhamis katika picha iliyokuwa ikionyesha mikono ya familia ya Pele kwenye mwili wake.
Pele amefariki akiacha mambo mengi ya kukumbukwa ikiwemo rekodi yake ya kufunga mabao 1,281 katika mechi 1,363 kwenye kipindi cha miaka 21 ya maisha yake, yakiwemo magoli 77 katika mechi 92 za nchi yake na pia mchezaji pekee aliyeshinda Kombe la Dunia mara tatu, yapo mambo matano kwenye historia yake ambayo hayafahamiki na wengi yaliyomuhusu.
Jambo la kwanza ni kucheza nafasi ya Golikipa katika michezo minne tofauti mbali na namba 10 yake aliyozoeleka kuicheza akiwa uwanjani.
Rekodi zilizopo kuhusu maisha ya Pele kisoka zinaonyesha kuwa aliwahi kukaa golini kama golikipa kwa timu yake ya Santos kwa sababu ya matukio mbalimbali ya uwanjani yaliyosababisha golikipa kutolewa nje na katika moja ya mechi akiwa langoni, aliisaidia timu yake kushinda.
Pele alicheza nafasi ya golikipa mwaka 1959, 1963,1969 na 1973 lakini mechi inayotajwa zaidi Pele akiwa golini ni ya mwaka 1963 ambapo timu yake ya Santos ilikuwa ikimenyana na timu ya Gremio de Porto Alegre kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Brazil.
Golikipa wa Santos ambaye alikuwa maarufu sana kutokana na ubora wake langoni, Gimar alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 86 ya mchezo na hakukuwa na mbadala mwingine alioruhusiwa kuingia uwanjani hivyo ikambidi Pele kwenda golini ambapo aliokoa mikwaju mikali miwili iliyokuwa akielekea kwenye lango la timu yake na hadi mchezo huo unamalizika Santos walitoka kifua mbele kwa goli 4 dhidi ya 3 za Gremio de Porto Alegre na Santos ikafanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Brazil.
Jambo la pili lisilofahamika sana kuhusu Pele ni tukio lililotokea Julai 17, 1969 huko Bogota nchini Columbia ambako Pele alisababisha mwamuzi wa mchezo baina ya timu yake na timu ya Olimpiki ya Columbia kutolewa nje ya uwanja baada ya mwamuzi huyo kumtoa Pele uwanjani.
Kwa mujibu wa rekodi za maisha ya Pele kisoka, mechi hiyo iliyochezwa majira ya usiku ilitawaliwa na vituko vya haba na pale wa mwamuzi wa mchezo, Guillermo Velasquez alijikuta katika mvutano na Pele na hivyo kumtoa nje ya uwanja.
Wachezaji wa Santos hawakukubaliana na uamuzi huo hivyo walimvamia mwamuzi Velasquez wakamtoa nje wa uwanja na nafasi yake ya uamuzi ikachukuliwa na mtazamaji kisha wakamrudisha Pele uwanjani kuendelea kusakata kabumbu.
Jambo la tatu ambalo halifahamiki sana kuhusu Pele ni kumpiga kichwa puani mchezaji wa timu ya Argentina, Juniors Jose Agustin Masiano na kumvunja pua katika mechi ambayo Brazil ilikuwa ikichuana na Argentina na beki huyo kupewa jukumu la kumkaba mguu kwa mguu Pele.
Gazeti la Argentina Ole ambalo lilipata kufanya mahojiano na Masiano, lilimkariri akieleza kuwa kocha wake, Maria Minella alimpanga katika mechi baina ya Argentina na Brazil na kumpa jukumu maalumu la kumkaba Pele mguu kwa mguu na yeye alilitekeleza jukumu hilo kwa nguvu zake zote lakini Pele baada ya kuona anaandamwa uwanja mzima na Masiano alimpiga kichwa cha pua na kuivunja.
Mwamuzi wa mchezo huo hakuona vizuri tukio hilo hivyo hakumwadhibu Pele kwa kumpa kadi nyekundu lakini baadaye Pele alipofanya mahojiano na Jarida la Argentina El Grafico alikiri kumpiga kichwa beki hiyo na kueleza kuwa tukio hilo analijutia sana katika maisha yake ya soka.
Jambo la nne ambalo halifahamiki sana katika maisha ya Pele ni kujihusisha na uigizaji wa filamu na uimbaji na moja ya filamu alizopata kuigiza, ameigiza pamoja na Sylvester Stallone – Rambo na Michael Caine.
Kwa mujibu wa mtandao wa data za filamu wa IMDB ambao hurekodi mienendo ya ulimwengu wa sinema, unamuonyesha Pele kama muigizaji katika filamu 11 ambapo kumi ni sinema za moja kwa moja na pia amecheza filamu moja ya kwenye televisheni. Lakini pia Pele anatajwa katika tasnia ya uimbaji.
Na tano, Pele aliitwa mhaini na nguli mwingine wa soka wa Brazil kwa sababu tu alimkumbatia aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) Rocardo Teixeira baada ya kumshtaki kwa makosa ya rushwa.
CHANZO CHA MKUSANYIKO WA HABARI HIZI NI VYOMBO MBALIMBALI VYA HABARI DUNIANI