RIPOTA PANORAMA
MOHAMED Ally Rwambo ambaye ni mfanyakazi wa Kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki cha Colourful Industry Limited, kilichopo Mbagala jijini Dar es Salaam amedai kuwa mwajiri wake aliyemtaja kwa jina la Fu He, maarufu zaidi kwa jina la Lina anamfanyia vitendo vya kikatili baada ya kuumia akiwa kazini.
Rwambo ametoa madai hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu kile alichoeleza kuwa ni ukatili uliopitiliza anaofanyiwa na Lina ikiwemo kumbambikia kesi ya polisi.
Amedai kuwa ukatili anaofanyiwa na Lina ni kumdhulumu haki zake alizopaswa kulipwa baada ya kupata ajali iliyosababisha kupoteza vidole viwili vya mkono wa kushoto na kimoja kupoteza uwezo wa kufanya kazi, kumlazimisha kusaini barua ya kuacha kazi kwa hiari kabla ya mkataba wake wa ajira kuisha na kumfungulia kesi polisi akimtuhumu kwa wizi.
“Hebu fikiria nina ulemavu wa vidole vitatu ambapo viwili vimekatika kabisa na kimoja kimepoteza uwezo wa kufanya kazi baada ya kupata ajali nikiwa kazini kwenye mashine. Niliponza kudai fidia na stahiki zangu wakaanza kunichukulia kama adui na sasa wameamua kunibambika kesi ya uongo,” anadai Rwambo.
Akitoa ufafanuzi wa shutuma zake hizo dhidi ya mwajiri wake, anasema alianza kufanya kazi katika kiwanda hicho mwaka 2014 kama ‘oparator’ wa mashine na ilipofika mwaka 2016 alipata ajali iliyosababisha kukatwa vidole viwili vya mkono wa kushoto huku kidole kimoja kikipoteza uwezo wake wa kufanya kazi.
Rwambo anadai zaidi kuwa visa vya bosi wake Lina vilianza baada ya kupata ajali ambapo alimuwekea vikwazo vingi katika kugharamia matibabu yake na baada ya kurejea kazini alisingiziwa kesi ya kuvamia eneo la kiwanda na kuwateka walinzi wawili, akawafunga kamba kabla ya kuiba Shilingi 200,000 na mashine ya kuoshea magari.
“Bila ya huruma sasa hivi wamenipa kesi ya kutengeneza ili waniondoe katika ajira bila kunipatia stahiki zangu, wanasema kwamba nimeshiriki kwenye tukio la kuwafunga kamba walinzi wawili na kuiba kiasi cha shilingi laki mbili na mashine mbovu ya kuoshea magari, mimi na ulemavu wangu huu wa vidole ninawezaje kuwakamata walinzi wawili na kuwafunga kamba.
“Hawa watu wanakuthamini pale unapokuwa mzima ukiwazalishia mali lakini ukishapata kilema hawakuthamini tena. Walinitibu kwa kusumbuana sana na nilipopona na kuanza kuulizia fidia na stahiki zangu nikageuka kuwa adui. Nashangaa hata baadhi ya watanzania wenzangu wenye vyeo pale kiwandani nao wanaungana na bosi wangu kunitisha, wanasema eti niwe mpole siwezi kushindana na hawa wachina kwa sababu wana pesa.
“Baada ya kutokea tukio la uhalifu kiwandani hapo, mimi na wale walinzi tulichukuliwa tukawekwa mahabusu kwa siku kumi ndiyo tukapewa dhamana na tangu hapo mpaka sasa tunaambiwa upelelezi haujakamilika kwa hiyo tupo tu hatujapelekwa mahakamani wala nini, tunazungushwa tu.
“Eneo lote la kiwanda lina kamera sasa sijui upelelezi gani unafanyika badala ya kwenda kutazama kamera ili kuwaona watu waliohusika na tukio hilo. Lakini jambo jingine la ajabu mimi ninayeambiwa niliwafunga kamba walinzi, tulikamatwa wote na walinzi tukawekwa mahabusu, hakuna mlinzi aliyetoa ushahidi kwamba mimi nilimfunga kamba. Haya ni mateso makubwa sana ninayoyapitia.
“Hivi sasa mshahara wangu umesitishwa licha ya kuwa mkataba wangu wa ajira haujaisha, nikiliuza naambiwa ni mtuhumiwa wa uhalifu hivyo sipaswi kuulizia mshahara. Najiuliza polisi hawataki kupeleka kesi mahakamani wanasema uchunguzi unaendelea wakati wanaweza kwenda kuangalia kwenye kamera wakaona kila kitu, sasa aliyenitia hatiani ni nani wakati sijafikishwa mahakamani?
“Kwa hali hii nitaishi vipi na ninaishi nyumba ya kupanga na nina familia, vidole vyangu vimepotelea kiwandani kwao, mshahara wangu wamesitisha na bado wanataka kunibambika kesi, naomba nisaidiwe kuonana na Waziri Mkuu au Rais ili wanisikilize kilio changu na wajue tabia halisi za huyu mwekezaji mchina zilivyo,” anasema Rwambo.
Anaongeza kuwa alipofuatilia kujua kama michango yake katika mfuko wa hifadhi ya jamii inawasilishwa kama inavyotakiwa alikuta amewekeza Shilingi 900,000 tu wakati amefanya kazi kiwandani hapo kwa miaka tisa.
“Ajabu nyingine kwa huyu Lina ambaye siyo jina lake halisi, watu wake wamekuwa wakinipigia simu wakinitaka nikasaini kuvunja mkataba eti ndipo wanilipe mafao yangu, sijaelewa huu utaratibu unatoka wapi, sijawakosea chochote hawataki kunilipa haki zangu eti mpaka nikubali kuvunja mkataba,” anasema.
Alipotafutwa Lina na kuulizwa kuhusu madai hayo alisema Rwambo ni muongo kwani jereha alilopata ni la miaka mingi iliyopita na alilipwa fidia. Alisema polisi walimkamata kwa sababu alihusika na wizi kwenye tukio lililowahusisha watu sita.
Lina alipoulizwa kuhusu kusitisha kumlipa mshahara Rwambo akingali mfanyakazi wake alisema yeye hana deni lolote naye na kuendelea kudai kuwa mara nyingi alikuwa akiiba lakini anamsaheme na alieleza mshangao wake kwa kudai kuwa ni kwa namna gani majambazi wanajiamini hivyo.
Alipoulizwa kuhusu uthibitisho wa madai yake kuwa Rwambo ni jambazi na iwapo kesi yake imekwishafikishwa mahakamani, Lina alisema maswali hayo aulizwe wakili wake kisha akatoa namba zake za simu.
Alipotafutwa Ijumaa wiki iliyopita, Wakili wa Lina ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema yupo polisi hivyo atafutwe Jumatatu, Disemba 19 ndiyo atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia suala hilo.
Alipotafutwa jana, wakili huyo alisema hakumbuki alichozungumzia na Tanzania PANORAMA Blog na alipokumbushwa alitaka atumiwe kwa maandishi kile kinachoulizwa ili akijibu kwa maandishi. Alipotumiwa alikaa kimya hadi tunakwenda mitamboni.
PERUZI TANZANIA PANORAMA BLOG KILA SIKU KUSOMA HABARI ZA SAKATA HILI NA MATUKIO MENGINE YA KIHABARI.