RIPOTA PANORAMA
MLOLONGO wa tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka vinazidi kumwandama Kamishna Mkuu wa Usimamizi wa Bima (TIRA), Abdallah Baghayo Saqware.
Tuhuma za sasa zimekuja kutoka kwa wadau wa sekta hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Tanzania PANORAMA Blog kuripoti skandali ya Kamishna Mkuu Saqware, sambamba na washirika wake kufungua Chuo Kikuu cha Bima na Mifuko ya Jamii barani Afrika, kwa kimombo kinaitwa Africa College of Insurance and Social Protection (ACISP.)
Okotoba 2, 2020 Saqware na wenzake watatu wasajili ACISP kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (Brela) na kupewa nambari ya usajili 140997609 wakiwa na mtaji wa hisa zenye thamani ya Shuilingi milioni 50 huku kila mwanahisa akiwa na hisa 250 zenye thamani ya Shilingi 1000.
Inadaiwa, Saqware kwa wadhfa wake wa Kamishna Mkuu wa Usimamizi wa Bima, moja ya majukumu yake ni kuiendeleza sekta ya bima nchini lakini kinyume chake, sasa amegeuka kuihujumu, akitumia ofisi ya umma kuwa mshindani mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kinachomilikiwa na Serikali.
IFM kinatoa pia kozi za masuala ya Bima hivyo ujuo wa ACISP umekifanya kuwa na mshindani katika utoaji wa huduma ya elimu hiyo lakini pia mshindani wake ACISP, licha ya kuendesha shughuli zake katika chumba kimoja huko Mikocheni mkoani Dar es Salaam, anadaiwa kujitangaza kuwa ndiye mwenye wataalamu wabobezi wa kufundisha kozi za bima kuliko vyuo vingine katika ukanda wa Afrika.
Saqware anadaiwa kutumia nembo ya TIRA ambayo ni taasisi ya Serikali kuandika barua kwenda kampuni na taasisi mbalimbali za Serikali kuzialika kushiriki na kuchangia mamilioni ya fedha za ushiriki wa warsha na makongamano ambayo yamekuwa yakiandaliwa na ama chuo chake cha ACISP au kwa ushirikiano baina ya chuo hicho na TIRA.
Taarifa za hivi karibuni zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimedai kuwa tangu Kamishna Mkuu Saqware ateuliwe kushika wadhfa huo vitendo vya ukiukwaji wa maadili katika utendaji wa soko la Bima vimekithiri na kwamba Saqware na washirika wake wameitumia TIRA kuchuma mamilioni ya fedha kwa kampuni na taasisi za Serikali; fedha ambazo zinapitia kwenye akaunti ya chuo cha ACISP ambayo haikaguliwi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
“Sekta ya Bima nchini ipo kwenye hali mbaya, hivi sasa mchango wa sekta ya Bima katika pato la Taifa unaendelea kushuka kutoka asilimia 0.4 mwaka jana kuelekea asilimia 0.3 mwaka huu. Hili hata Serikali inajua kuwa sekta ya bima inaporomoka lakini kwa nini inaporomoka? ni kwa sababu baadhi ya mabenki ambayo ni wafadhili wakubwa wa chuo hiki yanaendelea kufanya biashara ya Bima kinyume na Sheria ya Bima.
“Serikali ikitaka kuujua ukweli huu ifanye uchunguzi itabaini, sisi tumo kwenye sekta hii tunaona na tunajua hali ilivyo. Nikwambie, kila wakati Kamishna Mkuu akitoa waraka wa kurekebisha hali hiyo mabenki hutishia kugoma kukichangia chuo chake, anakuwa hana namna isipokuwa kufuta waraka wake wa mwanzo wenye maslahi kwa soko la bima na matokeo yake ni kudhoofisha soko la bima nchini,” anaeleza mmoja wa wadau wa Bima.
Taarifa zaidi zilizizopatikana kutoka vyanzo vya habari vya Tanzanuia PANORAMA Blog zimeeleza kuwa kukosekana kwa usimamizi mzuri wa biashara ya Bima kumesababisha kampuni nyingi za Bima kufilisika.
“Biashara yoyote inayofanywa chini ya vitisho au mashinikizo huwa haina afya. Kwa biashara ya Bima, kampuni nyingi zinazojihusisha na biashara hii sasa zimefilisika na sababu kubwa ni vitisho kama hili la kulazimisha kampuni za Bima na zile za udalali wa Bima kuchangia fedha shughuli zote zinazofanywa chini ya mwamvuli wa Chuo cha ACISP na wanaositasita hutishiwa kufutiwa leseni za biashara.
“Mpaka mabenki yenye leseni ya kufanya biashara ya Bima nayo yanalazimishwa kukichangia chuo hicho na yanayosita, kitisho ni kile kile cha kufutiwa lesseni ya biashara ya bima.
“Hata kampuni za Bima zilizoko nje ya nchi zinazojihusisha na biashara ya Bima ya Tanzania huwa yanaguswa na michango ya chuo hicho na yapo yaliyokutana na vitisho vya kutopatiwa hati ya kufanya biashara ya Tanzania (accreditation) kutoka kwa Kamishna Mkuu Saqware; haya yote yakichunguzwa yatabainika maana yako wazi kabisa,” ameeleza mtoa taarifa.
Wakati haya yakiibuliwa pamoja na mengine ambayo Tanzania PANORAMA Blog inaendelea kuyafanyia utafiti wa kihabari, Kamishna Mkuu wa TIRA, Saqware kila anapotafutwa kuzungumzia madai na tuhuma zinazoelekezwa kwake mwenyewe, TIRA na chuo chake cha ACISP amekuwa akikwepa kuzungumza kwa kutoa visingizio mbalimbali.