RIPOTA PANORAMA
IMEBAINIKA kuwa, genge la watu wenye nia ovu ‘wahuni’ na mwenendo wa sasa wa huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) linapanga na kutekeleza vitendo vya kuihujumu kibiashara.
Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Slaam, Mrisho Seleman Mrisho alipoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha tukio za wizi wa vipuri vya magari linalodaiwa kutokea bandarini hapo.
Akijibu, Mrisho amesema video hiyo ni ya muda mrefu, zaidi ya miaka miwili iliyopita na imekuwa ikitumiwa na maadui wa kibiashara wa Bandari ya Dar es Salaam ili kuichafua kwa lengo la kuharibu mwenendo wake wa kibiashara ambao sasa unastawi wa kasi baada ya uboreshaji mkubwa wa utoaji huduma.
Mrisho amesema uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam ulifanya uchunguzi wa uhalisia wa tukio linaloonyeshwa kwenye video hiyo na kubaini kuwa ni la kupandikiza kwa sababu halikutokea kwenye bandari na hata mavazi ya wahalifu wanaoonekana kuiba hayana mfanano na mavazi ya wafanyakazi wa Bandari ya Dae es Salaam.
“Watanzania waipuuze hiyo video, kwanza ni ya miaka miwili iliyopita na tukio hilo halikuwa katika Bandari ya Dar es Salaam wala bandari yoyote iliyopo Tanzania kwani eneo linaloonekana kwenye hiyo video halipo kwenye bandari yetu.
“Wakati ule walipoanza kuisambaza kwa mara ya kwanza tulichukua namba za makasha yanayoonekana kwenye video tukazihakiki kwenye mifumo ya forodha hususan tancis tukabaini kuwa makasha hayo hayakuwepo katika Bandari za Tanzania na wala hayakuwahi kupokelewa hapa nchini.
“Uchunguzi uliofanyika ulikuwa wa kina na ulibaini zaidi kuwa tofayuti na kwenye video hiyo, eneo la kuhifadhi shehena ya magari katika Bandari ya Dar es Salaam haichanganywi na shehena nyingine kama ya makasha (kontena) kama inavyoonekana kwenye hiyo video n ahata Bollard za rangi ya njano zinazoonekana kwenye video hiyo hazipo katika bandari zetu na hasa katika Bandari ya Dar es Salaam,” amesema Mrisho.
Aidha, Mrisho amesema hata viakisi mwanga (reflectors) vilivyovaliwa na wahusika wa tukio la wizi linaloonekana kwenye video vimechoka na havirandani na vinavyovaliwa na wafanyakazi wa Bandari ya Dae es Salaam.
“Reflectors za watumishi wa Bandari na zile zinazotumiwa na wafanyakazi wa kutwa wa SUMA JKT zina nembo maalumu tofauti na hizo zinazoonekana kwenye hiyo video na naomba niuhakikishie umma kuwa tukio la namna hiyo la wizi haliwezi kutokea bandarini kwa sasa kutokana na mifumo thabiti ya ulinzi iliyosimikwa,” amesema Mrisho.
Wakala wa utoaji mizigo bandarini na madreva wanaofuata magari bandarini hapo waliofikiwa na Tanzania PANORAMA Blog na kuulizwa kuhusu usalama wa magari yao wanayoyatoa bandarini hapo wameeleza kuwa matukio ya aina hiyo hayapo na kwamba inapaswa kijipanga kukabiliana na vita vya kiushindani wa biashara ambavyo siyo vigeni kwani vimeanza kupiganwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.