RIPOTA PANORAMA
TUHUMA za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka zinazidi ‘kutokota’ katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) huku Chuo Kikuu cha Bima na Mifuko ya Jamii barani Afrika, ambacho kwa lugha ya kimombo kinaitwa Africa College of Insurance and Social Protection (ACISP) kikiendelea kuficha siri ya yaliyomo TIRA.
Ikiwa ni zaidi ya wiki moja sasa tangu Kamishna Mkuu wa TIRA, Abdallah Baghayo Saqware aulizwe kuhusu tuhuma anazoelekezewa za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka katika TIRA na yeye kukwepa kujibu mara kadhaa, mmoja wa washirika wa Saqware katika ACISP, Anselmi Anselmi Mushy ambaye pia ni Katibu wa ACISP naye amechukua mchepuo huo huo.
Kamishna Mkuu Saqware na washirika wake wanadaiwa kuanzisha ACISP ambacho kimesababisha kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa maadili katika utendaji wa soko la bima hapa nchini linalodaiwa kuporomoka kwa kasi na kwamba chuo kikuu hicho ambacho kinaendeshwa katika chumba kimoja huko Mikochenim Dar es Salaam kimekuwa kikinufaika kifedha kwa mgongo wa TIRA.
Pamoja na tuhuma nyingine, inadaiwa Kamishna Mkuu Saqware, kwa kutumia wadhfa wake katika TIRA amekuwa akialika taasisi mbalimbali za Serikali kushiriki shughuli za ACISP kwa kuchangia fedha chuo hicho na ili kuficha uhalisia wa makusanyo hayo ya fedha na kujenga ushawishi kwa taasisi za Serikali kushiriki shughuli za chuo na kukichangia, yeye na washirika wake wamekuwa wakiwaalika viongozi wazito serikalini wakiwemo mawaziri na wakati nmwingine hata Waziri Mkuu kuwa wageni rasmi.
Kama ambavyo Saqware amekuwa akikwepa kujibu madai na tuhuma hizo kila anapoulizwa, Anselmi naye mwenye hisa 250 katika ACISP alipoulizwa alijibu kila swali kwa kuuliza swali lakini mwisho alipoambiwa kuwa anachokisema nacho ni jibu hivyo kitaandikwa kama kilivyo, haraka alijibu kuwa yeye siyo msemaji wa chuo hicho.
Tanzania PANORAMA Blog ambayo imefanya uchunguzi wa kina wa Skandali hii, leo inaripoti mahojiano baina yake na Anselmi; neno kwa neno ili wasomaji wetu na umma kwa ujumla; wapate mwanga wa kutosha wa Skandali hii.
PANORAMA: Salamu Bwana Anselemy. Rejea mazungumzo yetu ya muda mfupi uliopita. Africa College of Insurance and Social Protection (ACISP) ni taasisi binafsi na wewe ni mmoja wa wabia; zipo taarifa kuwa pamoja na taasisi yenu kutumia ofisi za umma kujinufaisha, pia taasisi yenu hiyo inatumika kutisha wadau wengine wa bima. Tunaomba kupata kauli yako.
ANSELMI: Fafanua.
PANORAMA: ACISP ambayo wewe ni mmoja wa wabia wake imekuwa ikipokea fedha kutoka makampuni ya bima, madalali wa bima na mabenki kwa ajili ya shughuli za taasisi yenu hiyo binafsi. Tunaomba kujua msingi wa taasisi yako hiyo kupokea fedha hizo. 2) Inaelezwa kuwa ACISP imekuwa ikitumia mwamvuli wa TIRA kupata fedha hizo, tunaomba kupata kauli yako kuhusu jambo hilo.
3) TIRA inalalamikiwa kuyatisha makampuni ya bima na madalali wa bima ambao wamekuwa wakisita kuchangia shughuli za Chuo cha ACISP kuwa wasipokichangia leseni zao zinaweza kufutwa. Tunaomba kauli yako kuhusu hili.
ANSELMI 1. Shughuli gani za taasisi? 2. Mwamvuli wa TIRA ndio inakuaje? 3. Naomba kuona huo mfano wa vitisho niweze kuelewa.
PANORAMA: Tunaomba kujua je kweli kwamba ACISP imekuwa ikipokea fedha kwa ajili ya shughuli hizo kutoka kampuni za bima, madalali wa bima na mabenki?
2) Tunaomba kujua TIRA imepata kuandika barua kuomba michango kwa kampuni za bima, madalali wa bima na mabenki kwa ajili ya shughuli za chuo chako?
ANSELMI: Shughuli zipi? Maswali ya TIRA si unatakiwa uwaulize TIRA chief?
PANORAMA: Msingi wa swali letu ni iwapo ACISP imekuwa ikipokea fedha kutoka vyombo hivyo tulivyovitaja kwa ajili ya shughuli za chuo.
2) Kuhusu TIRA wewe kama mwanahisa, je unafahamu kuwa TIRA imekuwa ikiyaandikia barua makampuni ya bima na mabenki kutoa fedha kwa ajili ya chuo chako?
ANSELMI: Na mimi nimekuuliza shughuli zipi za chuo? Si unajua chuo kina shughuli nyingi? chuo kina kazi katika maeneo tofauti:
i. Training 2. specialized training 3. certified training 4. partners designed training 5. sponsored training 6. scholarship training 7. Masterclasses 8. action based research 9. academic research 10. deep dives 11. diagnostic studies 12. feasibility studies 13. policy papers 14. journal articles 15. academic articles etc etc etc….. Sasa wewe unasemea shughuli zipi hasa?
PANORAMA: Tumefafanua kuwa je, ACISP imepata kupokea fedha kutoka kwenye vyombo tulivyovitaja kwa ajili ya shughuli yoyote ya chuo chako?
Na TIRA imepata kuandika barua kwa vyombo hivyo ikivitaka kuchangia shughuli yoyote ya chuo chako. Ni hayo tu.
ANSELMI: Hujavitaja bado. Ni taasisi gani hizo?
PANORAMA: Naomba soma vizuri maswali. Nimetaja kampuni za bima, madalali wa bima na mabenki. Shughuli zote za chuo chako.
ANSELMI: Hayo sio majina ndugu…hayo ni makundi. Majina ni kama ACISP na TIRA.
PANORAMA” Salamu Bwana Anselemy. Naomba kukumbusha kuhusu majibu ya maswali haya hapo juu.
ANSELMI: Salamu sana. Hujafafanua bado ndugu.
PANORAMA: Tunaomba kujua je kweli kwamba ACISP imekuwa ikipokea fedha kwa ajili ya shughuli zozote za chuo au imepata kupokea fedha kwa ajili ya shughuli za chuo kutoka kampuni za bima, madalali wa bima na mabenki?
2 ) Tunaomba kujua TIRA imepata kuandika barua kuomba michango kwa kampuni za bima, madalali wa bima na au mabenki kwa ajili ya shughuli za chuo chako?
…..Ndugu tumeuliza shughuli ya aina yoyote ile ya chuoni kwako hapo kama imepata kugharamiwa kwa fedha kutoka kwa vyombo tulivyovitaja. Na kama haijawahi kupokea ni kutujibu tu.
ANSELMI: Shughuli za aina yeyote ndio zipi sasa? Inabidi uwe specific…. Kila shughuli ina idara yake…nikijua ni shughuli gani naweza kukuelekeza idara husika wakupe majibu sahihi.
PANORAMA: Nitatumia majibu yako hayo nadhani yanatosha. Asante kwa ushirikiano wako
ANSELMI: Mimi sio msemaji. Ukitaka majibu uliza msemaji wa taasisi.
ENDELEA KUSOMA TANZANIA PANORAMA BLOG KUJUA UNDANI ZAIDI WA SAKATA HILI