RIPOTA PANORAMA
IDADI wa watu waliothibitika kuambukizwa virusi vya UVIKO 19 / Corona hapa nchini imeongezeka kwa asilimia 62.5 katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2, 2022.
Taarifa iliyotolewa leo na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu kuhusu mwenendo wa ugonjwa huo hapa nchini imeeleza kuwa kuanzia Oktoba 29 hadi Disemba 2, 2022 jumla ya maambukizi mapya 442 yalithibitishwa.
Prof. Nagu amesema idadi hiyo ya maambukuzi ni kubwa ikilinganishwa na takwimu za mwezi uliopita ambapo maambukizi yaliyothibitishwa yalikuwa 272 na kwamba Serikali inaendelea kutoa huduma ya chanjo ya ugonjwa huo ili kuwawezesha wananchi kupata kinga kamili inayozuia kupata ugonjwa mkali na hata kifo pale mtu anapopata maambukizi ya virusi vinavyosababisha UVIKO 19.
“Hadi kufikia Disemba 2, 2022 jumla ya watu 29,123,387 kati ya walengwa 30,740,928 ambao ni sawa na asilimia 94.7 wamepata dozi kamili ya chanjo ya UVIKO 19.

“Wizara inawahimiza watu wote wenye dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama vile homa, mafua, kikohozi, mwili kuchoka, maumivu ya viungo, kuumwa kichwa, vidonda vya koo na kupumua kwa shida kwenda vituo vya kutolea huduma za afya mapema,” inasomeka taarifa ua Prof. Nabi.
Taarifa hiyo inatoa tahadhari kwa umma kuchukua hatua za kujikinga na UVIKO 19 na magonjwa mengine ya kuambukiza kwa kupata dozi kamili ya chanjo ya UVIKO 19, kuvaa barakoa pindi mtu anapokuwa na dalili za mafua au kikohozi, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara na kuendelea kuchukua hatua za kujenga mwili imara kwa kufanya mazoezi na kula vyakula bora.