The Trinity of Steven Kanumba’s Death
HAMEES SUBA
0672 86 65 74
ILIPOISHIA
SIKU ya tatu tangu kurushwa kwa kipindi kile ndipo nilipokuja kumpata Kanumba baada ya kumpigia simu na kupokea. Licha ya kuwa mimi ndiye nilikuwa mpigaji wa simu ile lakini alipopokea tu, yeye ndiye akawa mzungumzaji wa kwanza.
Akanimbia; “Ogaa samahani sana kwa kutopokea simu zako lakini najua uliona intrerview yangu na Zamaradi ndiyo maana ukawa unanipigia, kifupi ni kwamba wakati nakusimulia yale mambo siku zile nilikuwa tayari nimesharekodi kipindi na Zamaradi kwa hiyo hakukuwa na namna ya kuzuia kipindi kisirushwe wakati walishapoteza muda wao na kipindi kilishaingizwa kwenye ratiba ya kurushwa siku hiyo.”
Alitoa maelezo mengi ya kujitetea kuhusu jambo hilo lakini kwangu hayakuwa na maana yoyote kwani yalikuwa masuala yake na familia yake. Mimi nikamuuliza; “vipi mrejesho wa watazamaji baada ya kutazama mahojiano hayo?”
Akajibu; “Ukweli mashabiki na watu wengi wamenipigia simu na kunipongeza sana, wameniambia ni kitendo cha kijasiri nilichokifanya na wamefurahishwa kwa mimi kuwa muwazi na mkweli, kwa hiyo mrejesho ni mzuri kabisa.”
Nikamuuliza; “Kwa upande wa baba yako mrejesho ukoje?” Akasema; “Sijapata simu toka upande huo, najua watakuwa wamenuna lakini potelea mbali, mimi jambo langu limetimia.”
TUUNGANE NAYO
Baada ya Kanumba kunieleza kwamba mrejesho kwa upande wa mashabiki zake ni mzuri na hakuna aliyemkosoa, mimi niseme nini tena? na hata nikisema itasaidia nini wakati kila kitu kimeshawekwa hadharani? nikaona ni vema tukaufunga mjadala huo na kuangalia masuala mengine ya mbele.
Nikamwambia; “Basi hakuna shida ogaa maadam umeshatema nyongo iliyokuwa ikikusumbua moyoni tuyaache hayo tuangalie mambo mengine, kuna mpya gani huko?”
Akaniambia; “Ogaa unajua nina safari nyingine ya Marekani na hapa tunavyoongea nina wiki mbili tu za kuwepo nchini.” Nikamuuliza; “ikoje hiyo na mbona imekuwa haraka sana?” Akaniambia; “ofcourse siyo haraka kwani ilikuwepo kwenye ratiba tangu kitambo sema tu mambo yamekuwa mengi ndiyo maana hatukuweza kuzungumza kila kitu.
“Kabla sijaenda Marekani ile mara ya kwanza nilikwenda Nigeria na kule nilikutana na mdau mmoja wa filamu aliyevutiwa na kazi zangu, tukapeana mawasiliano kwa ahadi kuwa atanitafutia connections za kuigiza na wasanii wa nje ya Tanzania wakiwemo wasanii wa Hollywood, Ghana, Zambia nk. Sasa niliporudi Marekani alinipigia na kuniambia amenitafutia mchongo wa kwenda kuigiza Hollywood, kwa hiyo ndiyo dhumuni la safari yangu hii.”
Nikamwambia; “hongera sana, anaitwa nani huyo jamaa na kwako anasimama kama nani?” maswali yangu hayo kwake yalilenga kupata habari ya kuandika. Akajibu; “huyu Mnigeria anaitwa Prince Richard Nwaobi, kwa sasa anasimama kama meneja wangu.”
Nikamwambia, “safi sana, nitaitumia hii taarifa kama habari kwenye toleo letu lijalo.” Akaniambia; “sawa ogaa ila usiandike kuwaambia watu nitaondoka lini maana si unawajua waswahili walivyo? hii nimekwambia wewe tu kwa wengine nataka iwe surprise, wewe andika tu Kanumba kwenda Marekani tena, safari hii nakwenda kufanya kweli siyo kama yale yaliyopita.”
Alisema siyo kama yale yaliyopita akimaanisha kukiri ‘magumashi’ aliyoyafanya kuhusu ile tuzo aliyodai kupewa Marekani. Nikamwambia; “nimekusoma ogaa nami nakuombea kila la kheri ufanikiwe katika safari yako.” Akajibu: “amina.”
Baaada ya hapo tulifunga mazungumzo lakini tukiwa na ahadi ya kukutana ndani ya siku mbili au tatu kwa ajili ya mazungumzo zaidi.
Baada ya siku mbili kupita nilikutana na Kanumba maeneo ya Kijitonyama kwenye Baa ya Hongera iliyopo jirani na Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam, yeye alitokea ofisi za Global Publishers na mimi nilitokea nyumbani kwangu wakati huo nikiishi maeneo hayo nyuma ya Baa ya Hongera.
Baada ya kusalimiana alitulia kwa sekunde kadhaa bila kuzungumza chochote, alionekana kama mtu asiye na utulivu wa akili au mtu mwenye mambo mengi kichwani akihitaji kuyafanya yote kwa wakati mmoja.
Nikafanya kama kumshtua; “inakuwaje ogaa?” Akaniambia; “nimetoka kuongea na Eric ((Shigongo) kuhusu safari yangu ya Marekani. Nikamwambia; “sawa, kuna tatizo?” Nilimuuliza swali hilo kutokana na ule ukosefu wa utulivu nilioubaini akilini mwake.
Akajibu: ‘hapana ogaa, hakuna tatizo ila natakiwa kwenda nyumbani Shinyanga kuaga kabla sijasafiri na kwa mujibu wa ratiba yangu natakiwa kukamilisha suala hilo wiki hii hii kwa sababu baada ya hapo nitakuwa busy na maandalizi ya safari ya Marekani.”
Alipoyasema hayo akilini mwangu nikajua kumekucha. Papo hapo nikagundua kwanini alikosa utulivu wa akili japokuwa sikujua alizungumza nini na Eric Shigongo lakini nilihisi kuwa kuna vitu Eric atakuwa amemshauri kuhusu mambo ya kwao hasa ikizingatiwa kuwa wote ni wasukuma japo mmoja ni wa Mwanza na mwingine wa Shinyanga.
Nikajiuliza kama anatakiwa kwenda nyumbani kuaga, atakwenda kumuaga nani wakati ni kipindi kifupi tu ametoka kuvurugana na baba yake? Nikaona akinitazama kama mtu aliyekuwa akijisemea moyoni; “lau kama ningemsikikiza huyu mwamba haya yote yasingeniumiza kichwa.”
Hakuna mtu wa kumuaga katika ukoo wake bila kuunganishwa na baba yake. Hakika alikuwa akiwaza namna ya kwenda kumvaa baba yake na kumuaga kwa ajili ya safari hiyo. Nikamuuliza; “kwa hiyo umepangaje?” Akasema; “ogaa najua unajua ugumu wa hii safari lakini lazima niende kwa namna yeyoye ile.”
Ukweli nilijua ugumu aliokuwa akikabiliana nao kuhusu hiyo safari lakini kwa sababu sikuwa nafahamu taratibu za mila za kisukuma sikuwa na chochote cha kumwambia. Nilitaka kumshauri kwenda kumuomba msamaha na kumtaka radhi baba yake lakini bado niliona kuna uzito mkubwa mbele yake.
Mwisho wa yote nikamwambia; “wewe ni mwanaume huwezi kushindwa jambo, mimi niko pamoja na wewe kwa kila hatua nakuombea kila jambo liende sawa. Akasema; “nashukuru ogaa, wacha mimi niende Kurasini kumuona mama nitajua nini cha kufanya.”
Kipindi hicho mama yake Kanumba alikuwa akiishi Kurasini. Tulifunga kikao tukaachana mimi nikarudi nyumbani na kumwacha akielekea Kurasini kumuona mama yake.
Baada ya siku kama tano hivi kupita Kanumba alinipigia simu na kunitaarifu kuwa amerejea kutoka Shinyanga. Nikamuuliza; “vipi mambo yamekwenda sawa?” Akanijibu; “kila kitu kipo sawa ogaa. Nikamuuliza; “ulionana na mzee?”
Alichukua muda sana kujibu swali hili kwani alianza kutoa maelezo mengi ambayo kimsingi sikuyaelewa kabisa. Lakini mwisho akasema hakukuwa na ulazima sana wa kuonana na baba yake ila alichotakiwa kwenda kukifanya Shinyanga amekitekeleza.
Jibu lake lilinishangaza kwa kiasi fulani lakini kwa kuwa jambo hilo lilikuwa halinihusu sana, nikaliachia hapo nikiwa na maswali yangu kichwani.
Nilimuuliza kuhusu ratiba yake ya safari baada ya kutoka Shinyanga akaniambia; “natarajia kusafiri (kwenda Marekani) siku ya Jumatatu au Jumanne, ila mpaka Jumapili nitakuwa na jibu la uhakika nitakufahamisha.
Hii ilikuwa mchana wa siku ya Alhamisi tarehe 5 Aprili, 2012 tulipozungumza mambo haya. Kwa maana hiyo alikuwa amebakiza siku takribani nne tu ili safari yake ya Marekani itimie kwa mujibu wa maelezo yake.
Kesho yake, yaani Ijumaa ya tarehe 6 Aprili, 2012 majira ya saa kumi jioni nikiwa newsroom kwenye maandalizi ya Gazeti la Kiu ya Jibu (Matukio) lililokuwa likitoka kila Jumatatu, niliwasiliana na Kanumba ili kama kuna updates za safari yake aweze kunipa ili nianze kuandaa stori ya kutumika kwenye gazeti letu la Jumatatu.
Alipopokea simu aliniambia kuwa yupo njiani anaelekea Ukumbi wa Dar Live Mbagala alikokuwa amealikwa hivyo akitoka huko ndipo tutaongea.
Nilimwelewa nikakata simu na kufunga mazungumzo yetu. Maandalizi ya gazeti nililokuwa naliandaa yalikuwa na siku mbili za ziada mbele, yaani kulikuwa na siku nzima ya Jumamosi na Jumapili zilizokuwa zimebaki kukamilisha maandalizi hayo.
Kwa kawaida gazeti lilikuwa likichapwa usiku wa Jumapili na kuingizwa sokoni alfajili ya Jumatatu. Kwa hiyo nilikuwa na muda wa kutosha kukutana na Kanumba ili kupata updates za safari hiyo.
Nilitoka ofisini majira ya saa moja na kurudi Sinza nikisubiri simu ya Kanumba atakapotoka Dar Live. Niliweka kambi mitaa ya Sinza kwa Remmy kwenye baa iliyoitwa Tanzanite, baadaye nikahamia Sinza Kijiweni kwenye Baa ya Deluxe ambapo nilikutana na washkaji zangu wa mitaa hiyo tukapiga stori mbili tatu halafu nikahamia Vatican kuwaona Chuchu Sound ‘Fire Brigade.’
Nikiwa Vatican nikapigiwa simu na Liva Hassan Sultan aliyekuwa kiongozi wa Bendi ya Diamond Musica na baadaye Schengen Academy akaniita Kinondoni. Harakati zilikuwa nyingi sana na nililazimika kukimbizana nazo zote kwa ajili ya kukusanya taarifa.
Nilipofika Kinondoni majira kama ya saa tatu na nusu hivi, iliingia meseji kwenye simu yangu kutoka kwa muigizaji Emanuel Miyamba, maarufu Kama Pastor Myamba akitaka kuthibitisha kutoka kwangu taarifa aliyoipata kuwa Kanumba amefariki dunia.
Meseji hiyo ilinishtua sana na ndiyo ilikuwa ya kwanza kunijulisha kuhusu kifo cha Kanumba. Nilichukua simu na kumpigia lakini simu yake ikawa busy kwa muda mrefu, nadhani tayari alishaanza kuwasiliana na wasanii wengine ili kufuatilia undani wa jambo hilo.
Nilifanya mawasiliano na waandishi wenzangu ili kujua ukweli wa taarifa hizo lakini wengi hawakuwa na taarifa zozote huku wachache wakisema hata wao wamepata meseji kama mimi ila bado hawajathibitisha.
Ilibidi nifupishe mazungumzo yangu na Liva Hassan Sultan ili niweze kurudi Sinza kufuatilia taarifa hizo kwa sababu nyumbani kwa Kanumba nilikuwa napafahamu.
Majira ya saa nne na nusu nikawa nimefika Sinza, mtaa aliokuwa akiishi Kanumba. Uthibitisho nilianza kuupata kutokana na mazingira niliyoyakuta nyumbani hapo.
Tayari watu walishajaa kwenye mtaa huo hadi kwenye nyumba aliyokuwa akiishi Kanumba. Nilikuta baadhi ya wasanii wa filamu wakiwa wameshawasili eneo hilo huku taarifa za kifo hicho zikimtaja Lulu kama muhusika mkuu.
Lakini kulikuwa na stori nyingi sana za matukio kabla ya kifo cha Kanumba kutokea.
Kama ilivyo ada ya kazi ya uandishi wa habari nililazimika kuwahoji watu niliowakuta eneo hilo kwa ajili ya kupata taarifa za awali juu ya tukio hilo.
Baadhi ya majirani walieleza kuwa kulikuwa na mtiririko wa ugomvi baina ya Kanumba na Lulu hali iliyosababisha Kanumba kumkimbiza Lulu mtaani akiwa na panga mkononi huku akiwa amejifunga taulo kiunoni.
“Ugomvi wao ulianza mapema, majira ya saa moja hivi tulisikia Kanumba akifoka sana ndani kwake, baadaye tukaona akimkimbiza Lulu akiwa na panga mkononi, yeye alikuwa na taulo tu,” alisema jirani mmoja niliyemuhoji siku hiyo ya tukio.
Wengine walieleza kuwa kulikuwa na mabishano yaliyohusu wivu wa kimapenzi. Inasemekana wakati Kanumba akiwa bafuni anaoga alimsikia Lulu akiongea na simu ya mwanaume mwingine ndiyo sababu ya Kanumba kutoka bafuni na kuchukua panga kisha kuanza kumkimbiza mtaani.
Hizo ni baadhi ya stori zilizokuwa zikitrendi eneo la tukio mara baada ya kifo cha Kanumba.
Baada ya kupata dondoo hizo chache niliwasiliana na kikosi kazi changu na kumpangia majukumu kila mmoja kisha nikaondoka eneo hilo.
Usiku majira ya saa sita na ushehe hivi, nilimpigia simu muigizaji Jacob Stephen maarufu kwa jina la JB ambapo yeye na Ray ndiyo walitajwa kuupeleka mwili wa Kanumba Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuhifadhiwa na kumuuliza juu ya kifo hicho.
JB alinithibitishia kwamba kweli Kanumba amefariki na wao wako Muhimbili wakishughulika kuuingiza mwili wa nguli huyo mochwari.
Kwa ushahidi wa mazingira Kanumba alikufa tarehe 6 Aprili, 2012 lakini kwa sababu kifo huthibirishwa na daktari ndiyo maana inatajwa kuwa alikufa tarehe 7 Aprili, 2012 muda ambao daktari alithibitisha kifo hicho.
Basi baada ya JB kunithibitishia kwamba walikuwa wakiuingiza mwili mochwari, nami ndipo nikawa na jeuri ya kuwasambazia wenzangu taarifa za uthibitisho wa kifo cha Kanumba.
Kwanini ghafla? Kanumba alimuaga nani kule Shinyanga wakati hakuonana na baba yake?
USIKOSE KUFUATILIA SEHEMU YA SABA YA MAKALA HII YENYE MAFUNDISHO MENGI.