HIVI NDIVYO NINAVYOMFAHAMU DIAMOND PLATINUMZ – 6
HAMEES SUBA
ILIPOISHIA
Diamond na Vespa
BAADA ya Diamond kuanza kuzishika noti, siku moja nikiwa naendesha gari katika barabara ya Tandale kuelekea Sinza, nikiwa maeneo ya Tanesco ghafla pikipiki aina ya Vespa ‘iliniovateki’ kwa mwendo wa kasi sana hali iliyosababisha niitazame kwa jicho la hasira.
Haikwenda mbali sana ikapunguza mwendo na kukata upande wa kushoto kuelekea njia za uswahilini. Kwenye gari nilikuwa na marehemu Boni ndugu yake na Papaa Misifa, yule anayeonekana kwenye video ya nenda kamwambie. Alinisikia nikisonya kutokana na kutofurahishwa na kitendo cha mwendo kasi ya ile Vespa. Akanitazama na kucheka kisha akasema; “Unakasirika nini? haya yote umeyasbabisha mwenyewe.”
Sikumuelewa alichomaanisha lakini kabla sijamuuliza chochote akaniongeza neno hili; “mwanao huyo ndio anakufanyia vurugu barabarani.” Alimaanisha kuwa aliyepita na ile Vespa kwa mwendo wa kasi alikuwa Diamond.
Sikuamini alichosema, nikamuuliza; “kaanza lini kuendesha Vespa na mbona mwendo anaokwenda nao ni wa hatari Sana?” Akajibu, “mambo ya ujana hayo, Vespa ni ya kwake kainunua.”
SASA TIRIRIKA NAYO…
Ghadhabu iliyokuwa imenishika kutokana na ile ‘ovateki’ ya Vespa ya Diamond niliyoishuhudia ilianza kupoa baada ya kusikia kwamba amenunua pikipiki. Nilicheka kidogo kisha nikamwambia Boni; “Mkionana mwambie dogo awe makini barabarani, vyombo vya moto havina uswahiba.” Boni akasema; “sawa mkuu ujumbe utafika.”
Pale kwenye ile kona aliyoingia Diamond na Vespa ndipo nilipomuacha Boni kisha mimi nikaendelea na safari yangu kuelekea Sinza.
Baada ya miezi kadhaa mambo yaliendelea kuwa mazuri, nikiwa kwenye kambi ya Aljazeerah Entertainment, Sinza Palestina nikapata taarifa kuwa Diamond ameachana na usafiri wa Vespa na kununua gari aina ya Toyota Celica iliyokuwa ikimilikiwa na mtangazaji wa Televisheni, Ben Kinyaiya.
Ilikuwa gari kuu kuu lakini kimjini mjini ilitosha kusafishia nyota hasa kwa msanii aliyekuwa anachipukia. Gari hiyo ndiyo ile inayoonekana kwenye video ya Mbagala ambapo kuna sehemu ndugu yake na Diamond, Rommy Jones anaonekana akishusha mguu toka ndani ya gari hiyo akiwa amevaa viatu vyekundu.
Wakati maendeleo ya Diamondyakizidikusonga mbele, nikasikia amepata show ya kutoka nje ya Dar es Salaam. Nadhani ilikuwa ndiyo show yake ya kwanza kufanyika mkoani, ilikuwa show ya Morogoro ambapo kwa mujibu wa Aljazeera walilipwa shilingi laki tano.
Baada ya show hiyo Diamond akapata show nyingine ndani ya Jiji la Dar es Salaam katika kitongoji cha Mbagala. Inasemekana kuwa show hiyo Aljazeerah waliipata kupitia mgongo wa Dj Nelly aliyekuwa mfanyakazi wa Clouds FM.
Nimeitaja show hiyo kwa sababu haiwezi kufutika kwenye kumbukumbu za Aljazeereh Entertainment na Diamond mwenyewe kutokanaa na kilichojiri. Ilikuwa ni show ya maumivu makubwa sana kwani licha ya kwamba jina la Diamond lilishaanza kuingia masikioni mwa mashabiki wa muziki, lakini show hiyo haikupata watu kabisa.
Yaani ukichukua idadi ya watu walioingia kwa kiingilio, walioingia kishkaji, Diamond na madensa wake, ‘kruu’ ya Aljazeerah, Dj Nelly na watu wake, wahusika wa ukumbi nk, hawakufika watu hamsini. Ilikuwa ni show ya hasara kweli kweli, lakini baada ya show Diamond alibaki akicheka na kusema: “dah imetupiga kweli.”
Labda nizungumze kidogo kuhusu tabia nilizozisoma kwa Diamond tangu awali mpaka kufikia kipindi ninachosimulia hapa. Katika kipindi hicho nilishagundua tofauti kubwa kati ya Diamond na wasanii wengine wengi niliokuwa nawafahamu au niliowahi kufanya nao kazi. Na hiyo tabia naamini ndiyo iliyomfikisha Diamond hapo alipo.
Jambo la kwanza, Diamond alikuwa jasiri na mtu asiyekata tamaa kwa matokeo yoyote aliyokutana nayo katika kazi. Hebu chukulia mfano mdogo huo, anapata show inaandaliwa kwa gharama kubwa na matangazo lakini unafika ukumbini watu hakuna.
Kuna wasanii wengi nimewahi kuwashuhudia wakishindwa ‘kupafomu stejini’ mara baada ya kuona idadi ya mashabiki walioingia ukumbini hairidhishi. Hii imewahi kutokea hata kwa wanamuziki wakongwe kama Muumini Mwinjuma ambaye wakati fulani alipokuwa akizindua albam zake mbili pale Diamond Jubilee Hall na kukosa mashabiki alishuka stejini akaenda kwenye chumba cha kukatia tiketi kuangalia hali ya kapu la hela ikoje na alipoona noti ni chache sana alishindwa kurejea stejini, akalala kwenye benchi na kupitiwa na usingizi mzito mpaka watu walipoanza kupiga kelele wakimuhitaji stejini.
Hata hivyo, licha ya kulazimishwa kurejea stejini, show hiyo ya uzinduzi ulimalizika kabla ya muda na Muumini Mwinjuma alitoweka ghafla stejini bila kufanya ‘arenjimenti’ zozote za kuwarudisha wanamuziki majumbani kwao wala kurudisha vifaa vya bendi, baadhi vikiwa vya kuazima.
Baada ya tukio hilo mmmoja wa wanamuziki wakongwe nchini, Mafumu Bilali ‘Bombenga’ alilalamika kwenye vyombo vya habari kuhusu Muumini Mwinjuma kutelekeza vifaa vyake vya muziki alivyomuazima kuvutumia kwenye shoo yake iliyofanyikia Ukumbi wa Diamond Jubilee Hall, akidai Muumini alimpigia simu na kimtaarifu avifuate vifaa hivyo mwenyewe.
Nimetoa mfano huo ili kuona ni jinsi gani Diamond alivyokuwa jasiri na asiyekata tamaa tangu kitambo.
Lakini pia Diamond alikuwa mtu wa kujituma sana (hili nilishalizungumza sana huko nyuma,) na pia aliyependa kuthubutu. Jambo la mwisho na ambalo lilikuwa gumu sana kwa wasanii wengine wengi hasa kipindi cha nyuma ni kuhusu skendo. Diamond alikuwa hogopa skendo hata kidogo, habari mbaya na nzuri kwake ilikuwa sawa.
Kipindi cha nyuma wasanii hawakupenda kabisa skendo, nadhani walikuwa wakitekeleza ule msemo wa ‘msanii kioo cha jamii.’ Wanamuziki kama Ambwene Yesaya ‘AY,’ na Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’ ni miongoni mwa wanamuziki ambao ilikuwa ukikosea kidogo kuwaandika au ukawabumbia skendo basi mwandishi na na wahariri wake wajiandae kufikishna mahakamani.
Kuna wakati AY hata ukosee jambo dogo tu atapiga simu kulalamika na hapo ujue amekuheshimu sana. Hakupenda kabisa skendo lakini tangu ujio wa Diamond kukazaliwa kizazi kingine ambacho bila skendo mambo hayasongi.
Ingelikuwa show ile imefanywa na msanii legelege labda angeweza hata kupoteza fahamu lakini mwamba aliangusha tabasamu akatingisha kichwa na kusema; “imetupiga kweli kweli.’
UHUSIANO NA WEMA SEPETU
Siku moja nikiwa kwenye kikao na viongozi wa Aljazeerah Entertainment nikasikia taarifa mpya. Mmoja wa wakurugenzi wa Aljazeera akatoa siri kwamba Wema Sepetu ‘amem-request’ Diamond kwenye facebook. Alisema kwamba Diamond alimuonyesha facebook yake na kuona request ya Wema ambapo naye ali-confirm kisha wakaanza kuchati.
Chati za mwanzo toka kwa Wema zilikuwa zikimsifu Diamond kwa muziki wake. Diamond hakuamini jambo hilo ndipo akaamua kumuonyesha bosi huyo huku akimtambia kuwa lazima ‘amnyooshe’ Wema. Kipindi hicho Wema alikuwa nchini Marekani na ikumbukwe kuwa aliondoka nchini akiwa ni mpenzi wa mwanamuziki wa African Stars ‘Twanga Pepeta,’ Chalz Baba.
Kwa upande wangu suala hili halikunistua kwani nikijua muda si mrefu nitakuwa na ‘breking news” zitakazonisaidia kuuza gazeti. Nilimsikiliza bosi huyo kwa umakini ili siku ‘dili’ litakapotiki’ niwe na ‘full details’ za kuwapa wasomaji wa magazeti yetu.
Nilikumbuka jinsi Chalz Baba alivyokuwa amezama kwenye penzi la Wema Sepetu na kuvuta picha atakaposikia yuko kwa Diamond itakuwaje. Nikakumbuka pia jinsi watu walivyokuwa wakitabiri mwisho mbaya wa penzi la Wema na Chalz Baba kutokana na Wema kuwa tayari alishakuwa na rekodi ya kutodumu kwa wanaume.
Nikavuta picha zaidi nikakumbuka jinsi Chalz Baba alivyojitoa Muhanga kumsindikiza Wema Sepetu uwanja wa ndege na wakaagana kwa mabusu mazito huku kamera za mapaparazi zikishuhudia, akisikia yuko na Diamond sura yake ataificha wapi?
Nikamuuliza mtoa taarifa wangu: “Unaamini anayechati na Diamond ni Wema kweli au kuna mtu amejifanya ni yeye ili kumpima imani dogo?” Akanijibu, “ni Wema kweli kwa sababu akaunti ya facebook ya Wema naifahamu vizuri.” Nikayahifadhi maneno hayo akilini mwangu.
Siku zikaendelea kukatika huku ukaribu wa facebook kati ya Diamond na Wema ukiongezeka. Kama wanenavyo wahenga ya kuwa lisemwalo lipo, kama halipo laja. Siku Wema Sepetu alipotua jijini Dar es Salaam, akatua mikononi kwa Diamond.
Mapokezi makubwa yakafanyika Airport, picha zikapigwa na mapaparazi walioalikwa. Baada ya kutoka Airport safari ya Wema na Diamond ikaishia Sinza Madukani mitaa ya Namnani Hoteli alipokuwa akiishi Diamond.
Tetesi zikaanza kuzagaa mjini kuwa Chalz Baba kapigwa chini na Wema Sepetu. Kesho yake habari zikachapishwa kwenye magazeti ili zimfikie vizuri Chalz Baba. Mji ukachafuka, stori ya mjini ikawa ni Wema na Diamond, Chalz Baba akawa haelewi amekosea wapi
Alichokumbuka ni kwamba waliachana vizuri na Wema na yeye ndiye aliyemsindikiza Airport wakati anakwenda Marekani. Hawakuwahi kugombana, sasa imekuwaje mpaka apokewe na Diamond? Kila alilowaza hakupata majibu.
NINI KILIENDELEA?
USIKOSE KUFUATILIA SEHEMU YA SABA YA SIMULIZI HII YA KWELI NA YENYE MAFUNZO MENGI