RIPOTA PANORAMA
MWENENDO wa mambo katika Sekta ya Bima si shwari baada ya kubainika kuwa Kamishna wa Usimamizi wa Bima (TIRA), Abdallah Baghayo Saqware ameshiriki kuanzisha Chuo Kikuu cha Bima na Mifuko ya Jamii barani Afrika, ambacho kwa jina la kimombo kinaitwa Africa College of Insurance and Social Protection (ACISP.)
Tayari baadhi ya wadau wa Sekta ya Bima wameanza kupasa sauti zao kulalamika kuwa baada ya kuanzishwa kwa chuo hicho kumekuwa na vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa maadili katika utendaji wa soko la Bima hapa nchini.
Nyaraka ambazo Tanzania PANORAMA Blog imeziona zinaonyesha kuwa Chuo cha Africa College of Insurance and Social Protection kimesajiliwa Brela kwa nambari 140997609, Oktoba 2, 2020 kikiwa na Ofisi zake Mikocheni, Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa nyaraka hizo, wana hisa wa chuo hicho wako wanne akiwemo Saqware mwenye hisa 250. Mtaji wa hisa za kampuni hiyo ni Shilingi milioni 50 na thamani ya kila hisa ni Shilingi 1000. Wana hisa wote ni raia wa Tanzania.
Tanzania PANORAMA Blog imedokezwa kuwa chuo kikuu hicho kinaendesha shughuli zake katika chumba kimoja kilichopo eneo la Mikocheni mkoani Dar es Salaam na taarifa zaidi zimedai kuwa Saqware amekuwa akitumia madaraka ya ukamishna aliyonayo TIRA kukiwezesha kifedha chuo chake hicho.
Alipotafutwa leo kupitia simu yake ya kiganjani kuzungumzia madai hayo, Saqware alisema yupo eneo baya atafutwe baada ya muda mfupi na alipotafutwa baadaye hakupatikana, simu yake haikuwa hewani.
Tanzania PANORAMA itaripoti zaidi sakata hili.