RIPOTA PANORAMA
LICHA ya Serikali kueleza bayana udanganyifu uliofanywa na mwana hisa mkubwa wa Kampuni ya Mwananchi Engeenering and Contracting Company Limited (MECCO) ambaye ni Kampuni ya SISI Construction Company Limited (SISICOL) wa kupora ardhi na mali za umma kisha kuzitumia kuchukua mkopo wa mabilioni ya Shilingi katika benki mbili kubwa za hapa nchini, Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Kwabhi Maungo amesema wanajiandaa kujibu mapigo.
Akizungumza na Tanzania PANOTAMA mapema wiki hii, Maungo alisema atajibu hoja zote ambazo menejimenti ya MECCO imeelekezewa kwenye mkutano na waandishi wa habari ambao hata hivyo hakusema utafanyika lini.
Maungo aliyasema hayo baada ya kuulizwa na Tanzania PANORAMA Blog ni lini mkutano wa wana hisa wa Kampuni ya MECCO unatajiwa kufanyika ili kuweka sawa dosari zilizojitokeza katika uendeshaji wa kampuni hiyo.
“Tumetuhumiwa sana, tumechafuliwa sana na ninyi mkaandika hayo waliyoyasema. Sasa siwezi kusema lolote kwa sasa, siwezi kusema kama kuna mkutano wa wana hisa au vinginevyo. Tunachokifanya sasa tunajipanga kujibu yote hayo yaliyosemwa, na wewe siwezi kukwambia lolote kwa sababu ndiyo walikwambia ukaandika, nitaitisha mkutano mkubwa wa waandishi wa habari wote ndiyo ntasema hapo kila kitu,” alisema Maungo.
Alipoulizwa mkutano huo atauitisha lini, alisema; “Siku yoyote, bado tunajipanga, wewe kama unataka habari kutoka kwetu ukisikia tu tunafanya mkutano na waandishi wenzake njoo, utapata habari zetu hapo,” alisema.
Serikali ambayo ina hisa asilimia 25 kwenye Kampuni ya MECCO imekwishatamka kuwa Kampuni ya SISICOL ambayo ndiye msimamizi wa shughuli za kila siku za Kampuni ya MECCO ilipunguza kinyemela hisa zake na kuibakizia hisa asilimia 2.6 tu.
Tamko la Serikali ambalo lilitolewa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, lilieleza kuwa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliweka wazi hila hizo za Kampuni ya SISICOL na ilichukua hatua ya kurejesha hisa zake hizo.
Sambamba na hila hiyo, Serikali imekwishaeleza bayana kuwa Kampuni ya SISICOL ambayo ndiyo mbia mkubwa kwenye MECCO ilifanya hila kubadilisha kinyemela hati za viwanja viwili, kiwanja namba 2 na kiwanja namba 3B vilivyopo barabara ya Nyerere, Manispaa ya Temeke, ambavyo ni mali ya MECCO kutoka kwenye umiliki wa MECCO kwenda kwenye umiliki wa Mas Holding and Container Depot Limited ambayo ni kampuni dada ya SISICCOL.
Kwamba kwa mujibu wa masharti ya mkataba wa uendeshaji wa Kampuni ya MECCO baina Serikali ya mbia wake huyo, yeye ndiye mwenye jukumu la kusimamia shughuli za kila siku za kampuni lakini hilo halimpi ruhusa ya kuhamisha mali.
Sehemu ya kauli ya Serikali iliyoitoa katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog inaeleza hivi; “Serikali baada ya kulibaini hilo kama nilivyokwambia baada ya kufanyika kwa ukaguzi, iliamriwa mali za MECCO ambazo zilikuwa tayari zimefanyiwa mabadiliko ya hatimiliki na kusomeka jina la MAS Holding and Container Depot Limited zirejeshwe katika umiliki wa MECCO.
“Msajili wa Hazina aliisimamia kazi hiyo ya utekelezaji wa uamuzi huo na hatua za kubadilisha umiliki wa hati ya mali hizo kurudishwa kwenye umiliki wa MECCO zilianza hadi kufika hatua ya kufanya malipo ya stamp duty na capital gain ili kukamilisha taratibu za kubadilisha umiliki.
“Katika hilo MECCO ilifanya malipo ya stamp duty kisha ikaomba kupatiwa msamaha wa capital gain tax lakini Mamlaka ya Mapato (TRA) ilitoa maelekezo kuwa hesabu za Kampuni ya MECCO na zile za Kampuni ya MAS Holding and Container Depot Limited ni lazima ziwasilishwe kwa mamlaka hiyo ili ifanye makadirio ya kodi kabla ya kuangalia huo msamaha.
“Hao jamaa hawakufanya kilichosemwa na TRA na badala yake wakakimbilia kwa Waziri wa Fedha na Mipango ambako nako walirudishwa TRA kwani aliwaambia watekeleze walichoambiwa na TRA. Hapa nikwambie tu kuwa hawajatekeleza hayo maagizo ndiyo maana kuna mkwamo lakini Serikali inafuatilia kwa karibu sana.
Serikali pia imeishazungumzia mkopo wa mabilioni wa Shilingi uliochukuliwa na Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited kwa kutumia hati za viwanja namba 2 na kiwanja namba 3B vilivyopo barabara ya Nyerere, Manispaa ya Temeke ambavyo ni mali ya MECCO baada ya kubadilisha umiliki wake kinyemela.
“Hata hilo Serikali inalifahamu na imeishachukua hatua. Msajili wa Hazina alifanya mawasiliano na Benki ya NBC na hatua za kurejesha umiliki wa hati hizo zilianza lakini kama nilivyoeleza kulitokea mkwamo kidogo baada ya hawa jamaa kutowasilisha hesabu zao TRA.
Aidha ilieleza zaidi kuwa mkutano wa wanahisa unatarajiwa kufanyika mwaka huu ambapo kasoro za uendeshaji wa kampuni hiyo zinatajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.