Tuesday, December 24, 2024
spot_img

UNDANI KIGUGUMIZI CHA TRA KWA NINE FIVE GROUP

RIPOTA PANORAMA

WAKATI Mamlaka ya Mapato (TRA) ikitoa majibu ya kujichanganya na pia ikishindwa kujibu baadhi ya maswali iliyoulizwa kuhusu nyaraka zenye utata za usafirishaji mizigo nje ya nchi za Kampuni ya Nine Five Group Limited, wakala wa usafirishaji na upokeaji mizigo wameelezwa kuwa nyaraka hizo zina kasoro.

Haya yameelezwa ikiwa ni siku chache baada ya Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo kutoa kauli za mkato na zenye kujichanganya wakati akijibu kuhusu utata wa nyaraka hizo lakini pia akilalamika kuwa anaulizwa maswali mengi kuhusu sakata hilo.

Uchunguzi wa Tanzania PANORAMA Blog kuhusu sakata la utata wa nyaraka hizo umeonyesha kuwa Kampuni ya Nine Five Group kwa kushirikiana na kampuni ya uwakala wa usafirishaji na upokeaji mizigo (jina linahifadhiwa kwa sasa kwa sababu haijapatikana kuzungumza) imekuwa ikitumia nyaraka zenye dosari kusafirisha kontena zake.

Kwa mujibu wa uchunguzi, Kampuni ya Nine Five Group ambayo imesajiliwa kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (Brela) Oktoba 4, 2017 ina wakurugenzi wawili ambao ni Jiugang Yang na Yuanyuan Yang, wote raia wa China.

Uchunguzi umebainisha kuwa kampuni hiyo inazo ofisi zake katika makutano ya barabara ya Rufiji na Nyamwezi, Karikoo na ina wana hisa wawili ambao ni Jiugang Yang mwenye hisa 900 na Yuanyuan Yang mwenye hisa 100. Kampuni hiyo inajishughulisha na usafirishaji wa mazao ya chakula kwa muda mrefu.

Ingawa taarifa rasmi zilizoko serikalini zinaonyesha kuwa Kampuni ya Nine Five Group Limited, ofisi zake ziko makutano ya mtaa ya Rufiji na Kariakoo, uchunguzi umebaini kuwa shughuli zake ilikuwa ikizifanyia katika moja ya maghala yaliyoko eneo la Tazara ambako nako ilihama siku chache baada ya Tanzania PANORAMA Blog kufika ikisaka ukweli wa madai na tuhuma inazoelekezewa.

Tanzania PANORAMA Blog ilifika katika ofisi za Kampuni ya Nine Five Group huko Tazara ili kupata kauli ya kampuni hiyo kuhusu madai na tuhuma inazoelekezewa ambako ilikutana na msaidizi wa mkurugenzi aliyekataa kutaja jina lake huku akieleza kuwa bosi wake yuko nje ya nchi lakini amemuagiza kuondoa vifaa vyote vilivyo kwenye ofisi hiyo avipeleke nyumbani kwake.

Alisema ameelekezwa kutojibu chochote iwapo atafikiwa na waandishi wa habari na badala yake aliomba aachiwe maswali kwa maandishi aliyoahidi kuyafikisha kwa bosi wake ili ayajibu kwa njia ya simu, jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa licha ya Tanzania PANORAMA Blog kumwachia maswali kwa maandishi.

Nyaraka zenye utata zinazodaiwa kutumiwa na Kampuni ya Nine Five Group kusafirisha kontena zake nje ya nchi, kwa lugha ya kimombo zinaitwa release order, tansad, loading permission na invoice.

Upekuzi wa nyaraka hizo umeonyesha kuwa invoice na tansad zilizotolewa kwa ajili ya kusafirisha kontena moja kwenda nje ya nchi zinataja namba ya kontena husika kuwa ni moja tu wakati release order ya kusafirisha kontena hiyo iliyotolewa na TRA ikiwa haionyeshi idadi yoyote ya kontena inayosafirishwa.

Uchunguzi zaidi wa nyaraka umeonyesha kuwa wakati invoice na tansad zikionyesha kontena inayosafirishwa ni moja nyaraka nyingine moja ambayo kwa lugha ya kimombo inaitwa loading permission inaonyesha kuwa kontena zinazosafirishwa ni kumi ikiwemo hiyo kontena moja inayoonyeshwa kwenye invoice na tansad.

Afisa mmoja wa wakala wa usafirishaji na upokeaji mizigo (jina limehifadhi) aliyezungumzia utata huo alisema nyaraka hizo tatu ni muhimu katika kutambua mzigo wa msafirishaji kama umezingatia taratibu zote zinazopaswa kufuatwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za TRA.

“Kwa kawaida mimi kama wakala, anapokuja mteja kutaka nimfanyie utaratibu wa kusafirisha mzigo wake nitaanza na shipping line ili kupata gharama za meli, baada ya hapo nitafanya booking kwa ajili ya shipping order.

“Shipping order ikishakaa sawa kinachofuatia ni kufanya stuffing, yaani kuandaa sehemu ya kupakilia mzigo na baada ya hapo ndipo maafisa wa TRA hufika kwa ajili ya kuukagua mzigo na kuandika remarks zao ndipo release order inapotoka.

“Release order inapotoka, wakala huwafahamisha watu wa shipping line ili waangalie ratiba ya meli ikoje na wao wakishapata ratiba ya meli huwafahamisha TRA siku ambayo mzigo wa mteja utapakiwa kwenye meli.

“Huo ndio utaratibu tunaofuata nikiwa na uzoefu katika kazi hii kwa miaka mingi. Na hizo nyaraka tatu nilizozitaja mwanzo lazima zionyeshe kwa uwazi kile kinachokusudiwa kusafirishwa bila kusahau namba na idadi ya kontena,” alifafanua.

Akizungumzia release order kutolewa bila kuwa na namba wala idadi ya kontena alisema hilo linawezekana endapo tansad itakuwa haijataja namba za kontena.

“Mteja anaweza akawa hajapata kontena za kubebea mzigo wake wakati anaomba release order ndiyo maana unaweza kukuta release order haionyeshi namba za kontena, hivyo endapo tansad haionyeshi namba ya kontena na kwenye release order huwezi kuiona lakini ikiwa tansad inataja namba ya kontena lazima release order nayo itaje.

“Haiwezekani tansad iwe na namba ya kontena halafu release order isiwe nayo, mimi ninayojua ni hayo lakini TRA kwenye hicho kitengo  mlichokiuliza maana na mimi nimesoma majibu yao nadhani waulizeni zaidi walizungumzie lakini inavyoonekana suala lenyewe lilivyo hili ndiyo maana wanajibu kwa mkato wakijua watawachanganya nyie lakini haiwezekani invoice na tansad ziwe na namba ya kontena halafu release order isiwe nayo.

“Na kwa miaka yote niliyokuwa kwenye kazi hii sijawahi kuona invoice na tansad zinataja idadi tofauti na ile iliyopo kwenye loading permission, ndiyo naona leo haya mambo,” alisema.

Tanzania PANORAMA inaendelea kumtafuta Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba ili pamoja na mambo mengine asaidie kujibu na kutoa ufafanuzi wa maswali ambayo TRA ilijichanganya kuyajibu kwenye sakata hili.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya