Wednesday, December 25, 2024
spot_img

KITENDAWILI CHA BABA BORA NA BABA MBEGU

MAUREEN MALLYA

MIAKA kadhaa iliyopita, nikiwa binti mbichi wa miaka kumi na tisa nilimchokoza baba yangu. Nia au dhumuni langu kubwa ilikuwa kupata nafasi ya mimi na yeye kukaa chini na kuzungumza. Nilitamani sana kuwa na uhusiano wa kirafiki na baba, nilikusanya nguvu nikamwambia, “baba nina boyfriend mwenye miaka 27.”

Nilitaka hii kauli imstue kwa kuona mwanangu anapotea na huu uhusiano sio mazuri kutokana na umri wangu kwa wakati ule; magonjwa, shule na mambo kadha wa kadha hivyo akae chini na mimi kunipa usia. Lakini kwa bahati mbaya, akasema tutaongea baadaye. Baadaye haikuwahi kufika mpaka umauti wake miaka kadhaa mbele.

Najua unajiuliza kwa nini ninayazungumzia haya hapa. Lengo langu kuu ni kukujuza au kukumbusha umuhimu wa baba katika maisha ya mtoto.

Katika jamii zetu za kitanzania tumezoea kuona akina mama ndio wenye majukumu ya kulea watoto na akina baba kazi yao ni kutafuta. Lakini katika ulimwengu wa sasa haya mambo hayapo hivyo, akina baba wengi wamesahau majukumu yao, kwenye utafutaji hawapo na kwenye malezi ndio kabisa watoro sugu.

Akina mama wamejikuta wakivaa kofia zote mbili za baba na mama katika familia. Mama ndio mtafutaji, mlezi, mwalimu, daktari, nesi, mshauri, mlinzi, kiongozi nakadhalika. Akimama hawawezi kususia majukumu yao na wanapambana sana kwa ajili ya watoto na ndio maana watoto wanakuwa na upendo mkubwa sana na mama zao kuliko baba zao.

Watoto wakishakuwa watu wazima, unakuta wanawajali zaidi wazazi wao wa kike kuliko wa kiume. Rafiki yangu mmoja ameshajiandaa kisaikolojia, akizeeka wanawe watamjali mama yao kuliko yeye. Swali langu moja kwake ilikuwa anafanya nini kubadilisha huo mtazamo?

Mimi kama binti wa kike natamani sana ningekuwa na uhusiano wa karibu na baba yangu. Baba ndio mwanamume wa kwanza katika maisha ya mtu na kama akina baba wakijua na kutumia nafasi zao vizuri watoto wao wataishi vizuri sana.

Matatizo mengi yanayoendelea sasa ya matumizi ya dawa za kulevya, sonona na matatizo mengine ya afya ya akili yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na wazazi wa kiume kutokuwa na muda na watoto wao. Upendo unaponya mambo mengi sana na kurudisha afya ya familia.

Mdogo wangu mmoja alijiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na hii ikanifanya niwaze kwa kiasi kikubwa inakuaje mtu anasoma shule nzuri, anaishi vizuri na ana kila kitu anachokitaka anajiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na makundi yasiyofaa?

Baba ni zaidi ya mbegu zako za kiume. Baba una nafasi kubwa sana katika maisha ya wanao na wanao wanatamani sana kuwa na ukaribu na wewe. Mazoea mazuri ya kudumu yanatengenezwa utotoni. Mtu akishakuwa mtu mzima inakuwa ngumu sana kuanzisha uhusiano wa baba na mtoto kuliko kipindi cha utoto.

Ndiyo, unapambana kutafuta pesa kutunza familia lakini maisha ni zaidi ya pesa. Uhusiano mzuri na wa kudumu haujengwi na fedha. Fedha inasaidia kuendesha maisha kama kulipa kodi, ada, kununua bidhaa na kadhalika lakini pesa hainunui malezi. La sivyo watoto wengi wangewalipa wazazi kwa muda wao ili wapate muda wa kuwa pamoja nao. Ushiriki wa baba kikamilifu katika malezi una mchango mkubwa sana katika afya na ustawi wa mtoto.

Ni vema ukipata muda wa kukaa na watoto wako mkajadili mambo kwa pamoja. Hii inajenga uaminifu baina yenu. Mtoto akishakuamini anakuwa huru kukueleza yale yote yanayojiri katika maisha yake. Hii inampa baba wasaa wa kurekebisha mambo mapema kabla hayajawa makubwa. Hii inawapa watoto wako uhakika wa upendo wako na uthamini wako kwenye maisha yao.

Wasikilize watoto wako, jadiliana nao na wawezeshe kupitia sauti zao. Mambo mengi mabaya yanawatokea watoto kama kulawitiwa na kubakwa na watu baki au watu wa karibu. Sasa kama mtoto hana ukaribu na wewe baba yake hawezi kukuambia anayotendewa na madhara yake ni kwamba ukija kugundua unakuwa umeshachelewa na mtoto anapata majeraha makubwa sio ya kimwili tu bali ya kisaikolojia pia ambayo hayaponi mpaka utu uzima.

Usisahau kama baba kuwaambia watoto wako unawapenda sana na unawathamini. Wasikie hizi kauli kutoka katika ulimi wako la sivyo watazisikia kwa mbwa mwitu wenye ngozi za kondoo mbeleni.

Tafuta muda wa kucheza na watoto wako au kutoka nao kwenda sehemu mbalimbali za mapumziko. Wajengee ‘standard’ za maisha watoto, sio lazima kuwapeleka sehemu za gharama kubwa nenda nao sehemu wanazopenda na ambazo mtakuwa na muda wa pamoja.

Tuepuke kuwa na watoto ambao wakija kubalehe na kukutana na mapanya buku wa mtaa wanaona kila kitu kipya kwao na inakuwa rahisi kuhadaiwa.

Wewe baba ndio mfano na uishi kwa mfano ukijua watoto wana jifunza kupitia wewe. Watoto wana tabia za kuiga mambo ambayo watu wazima wanafanya. Hata utotoni tulikuwa tunacheza kibaba na mama. Tulikuwa tunaiga yale ya nyumbani kwetu, mazuri au mabaya yote tuliiga, najua wahenga wenzangu mnayajua haya.

Tengeneza tamaduni katika familia yako. Baba ndio kichwa cha familia. Zamani tulikuwa na desturi za kwenda vijijini mwezi Disemba, huko tunakutana na mabibi na mababu na ndugu wengine, tunafurahi na kujifunza mambo mengi sana. Zilikuwa tamaduni nzuri lakini sasa kwa kiasi kikubwa hazipo tena.

Ni vema kama familia kuwa na taratibu au tamaduni zenu. Kula pamoja kila siku, kusali pamoja, kuwa na safari za kifamilia na mitoko ya baba na watoto. Hizi ni taratibu nzuri zenye kujenga familia yenye furaha na upendo.

Baba si dhambi kusaidia kazi za nyumbani, usitake mtoto azimie siku akikuta baba anaosha vyombo, fanya kazi za nyumbani na watoto wako, sio lazima kila kitu wafanye na mama.

Watafurahi sana watoto wakifanya kazi na baba yao, unawafundisha watoto kwa vitendo lakini pia unapata muda wa kuwa na watoto wako. Maisha yana jengwa na ‘experiences’ tunazotengenez, hata ukifiwa unalia na kusikitika kwa sababu unakumbuka ‘experiences’ zako na mwenda zake. Maisha yanaenda kasi sana lakini umauti utakapokuwa umekusogelea utatamani sana ungetumia muda wako kuwa na wale uwapendao.

Akinababa mkumbuke kwamba mpenzi wa kwanza wa mtoto wa kike ni baba yake. Jitahidi kuwa mfano bora kwa binti yako, mpende sana mama wa watoto wako kwa sababu utawajengea mfano mzuri watoto watakapokuwa kwenye familia zao.

Kuwa mfano wa kuigwa na watoto wako. Ukimpenda wa mama watoto kisawasawa utakuwa na uhakika wa binti yako kuchagua kilicho bora kama baba yake. Je, wewe baba unayesoma hii makala unadhani ungetamani binti yako aolewe na mtu kama wewe? Tafakari na uchukue hatua.

Ukiwa karibu na watoto wako ni rahisi kuepusha jahazi kuzama maana unawakunja wakiwa wabichi. Maji yakishamwagika hayazoleki na ni vema kuziba ufa usije jenga ukuta mbeleni kwa gharama kubwa.

Huu ni mtazamo wangu kwa yale niliyoyaona katika maisha yangu na yale ambayo pia ningetamani wazazi wangu wangeyafanya kwangu. Nashukuru kabla baba yangu hajafariki aliniambia; “I am very proud of you” na haya maneno yanaishi kwenye nafsi yangu na ndio urithi wangu mkubwa kutoka kwa baba.

Busara, imani, tabia njema, kujiamini, chaguzi sahihi, kufanya kazi kwa bidii, utawala, kutii mamlaka nk yanafunzwa na baba aliye bora. Na baba mbegu yeye kazi yake ni kupanda mbegu wala asipalilie na hataki kujua atavuna nini.

Yeye akishapanda amepata na kuwaachia wengine wapambane na mbegu zake japo kwenye fikra zake anatarajia mazao mazuri. Akina baba wengi wapo hapa kwenye baba mbegu, wanawatunga mimba wanawake kisha wanawaacha walee watoto wenyewe na kwa bahati mbaya akina mama nao wapo ‘busy’ kutafuta maisha, mwishowe hatma ya watoto inadondokea kwenye mikono ya wafanyakazi wa nyumbani na bado tunategemea kuwa na watoto bora.

Nakuomba kwa niaba ya watoto wote wadogo na wakubwa, jitahidi kuwa baba unayekimbiliwa na watoto ukirudi nyumbani na sio baba unayekimbiwa na watoto. Tamani watoto wako wapende kuwa na wewe kila wakati, wakutamani ukiwa mbali nao.

Huu sio ulimwengu wa kale, mambo yamebadilika sasa. Tusilete ukale sasa. Ooh mbona baba zetu walikuwa hivi au walifanya vile? Hizo ziliku enzi zao na hizi ni za kwako. Waliandika historia zao na zingine zimewaacha watu ni wazee sasa lakini hawajui mapenzi ya baba na wanatamani hata wazee wao wangewaambia wanawapenda na wanapendezwa nao.

Tubadilishe historia, tubadilishe mitazamo na tuwe akina baba bora. Hata mimi baba alinipenda, ni vile tu hakuwa na uwezo wa ‘kuexpress’ mapenzi yake kwangu kama nilivyotamani.

Inawezekana tukiamua.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

1 COMMENT

  1. Having grown up without my father being there as much as he’s very much alive my biggest prayer and gift to my future children is to get them a good father figure someone my future children will be proud of free with him I can’t wait to see them bond do almost everything together .They say what makes you a man is not the ability to make a child it’s the courage to raise one

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya